Yah: Mheshimiwa Rais tunaomba yafanye yafuatayo:

Siku chache zilizopita baada ya kuapishwa, umefanya yale ambayo wengi hatukutarajia kama kweli ungeweza kuthubutu kuyafanya pamoja na kaulimbiu yako ya ‘hapa kazi tu’. Wengi hatukuamini kwa sababu tulijua ni walewale wa kunadi visivyotekelezeka kama ilivyokuwa kwa miaka mingine ya huko nyuma.

Wengi waliamini unafanya propaganda za kisiasa wakati ukinadi sera za Serikali na utendaji wako, wapo waliosema hukuweza zamani utawezaje sasa, na wapo waliosema ulikuwamo ndani utawezaje kutoka. Sasa walioimba na walioimbishwa wote ni mafi kanyanga yaani wanacheza muziki kwa mirindimo yake na siyo maneno.

Mheshimiwa Rais, huku mitaani umepewa majina mengi sana, mengine mazuri mengine mabaya, huku mtaani una sura nyingi sana, sura ya upendo na sura ya ukatili, huku mtaani una roho nzuri na una roho mbaya, huku mtaani unapendwa na unachukiwa sana, huku mtaani unafahamika sana sasa hivi tofauti na zamani.

Mheshimiwa Rais, kundi linalokuona kwa maana ya ubaya ni dogo sana lakini lina nguvu kutokana na ushawishi wa pesa, sijui wanazitoa wapi kuweza kuzitumia katika propaganda zao za kuwaaminisha watu kuwa wewe ni mbaya. kundi hili lina nguvu ya kuwanunua maskini wachache ambao kula yao na maisha yao yapo mikononi mwao, hawa nao ni wananchi hewa wanaishi kwa kutegemea watu wengine wawalishe na kuwalaza.

Mheshimiwa Rais, katika utekelezaji wa majukumu yako ya kila siku, sisi wananchi wengi tunakubali uamuzi wako, tunakubali utendaji wako na Serikali yako. Wengi wetu hatukubali kulishwa maneno ya kipuuzi na uongo ili tukuone mbaya baada ya kuwabana hawa wachache waliokuwa wakiishi peponi kwa kutumia rasilimali zetu wote.

Tuna mambo machache ambayo tunaweza kutoa ushauri uyafanyie kazi lakini pia itategemea na utashi wako na maono ya mbali kama unaweza kuyafanyia kazi. Mosi, hatuamini sana katika utendaji kazi bila moyo wa dhati na dhamira ya kweli ya mtu kwa Taifa lake pasi na kutokuwa mzalendo. Taifa hili limefikia hapa tukiwa na wasomi wengi na katika nyadhifa mbalimbali.

Kama Mzee Zuzu, nashauri usiamini sana katika elimu ya mtu na kwamba elimu hiyo inasaidia kutuletea maendeleo, wengi wenye elimu kama hizo ndiyo waliotufikisha hapa kwa ujuzi wa elimu zao, wengi wao wametumia elimu hizo kutumaliza sisi wananchi wa Taifa hili, uwe na kigezo kikubwa cha uzalendo kabla ya kuangalia uwezo wa darasani, naamini uwezo wa darasani si uwezo wa kuongoza, uongozi ni karama zaidi na elimu inasaidia kuboresha karama hiyo.

Ukiangalia wasifu wa mtu unaweza kuogopa kwa ukubwa wake lakini jiulize alikuwa wapi na amefanya nini na mchango wake ni upi katika kutatua migogoro na changamoto katika Taifa lake, jiulize  alipokuwa kabla ya uteuzi wako ametoa mchango kiasi gani cha kuweza kukuridhisha kwenda na kasi yako.

Mheshimiwa Rais, kuna mambo mengi ambayo ni kama bado kuna sintofahama yalianzajeanzaje na hatima yake ni ipi. Nitajitahidi kuweka machache machache ili uyaangalie kwa jicho la tatu zaidi kama Rais.

Pili, kuna suala la ajira za pikipiki kwa vijana, suala hili lilikuja kisiasa zaidi pasi na kutizamwa kwa jicho la tatu athari zinazotokana na ajira hiyo,  ni ajira ambayo hatukujiandaa kama Taifa kuipokea kwa wakati huu, ni ajira ambayo ina makwazo mengi kuliko faida inayopatikana kwa vijana hawa.

Angalia ajali zinazopatikana na athari katika jamii, vijana wengi ni walemavu na vijana ndiyo Taifa la leo, ambalo tunahitaji nguvu kazi yao kuweza kulipeleka mbele gurudumu la maendeleo, kuna watoto wengi wamepoteza maisha na kupewa ulemavu kutokana na ajira hii ya kisiasa. Naomba uliangalie kwa jicho la tatu zaidi suala hili.

Mheshimiwa Rais, pikipiki zimerahisisha usafiri lakini pia zimerahisisha vifo vya wapiga kura wako wengi, wapo waliopoteza maisha kwa kukosa damu kwa kuwa sasa mahitaji ya damu ni makubwa kuliko wakati mwingine wowote.

Wapo waliopoteza maisha kwa kukosa dawa kwa kuwa mahitaji dawa baada ya ajira hii yalizidi nguvu ya upatikanaji wa dawa, wapo waliokosa huduma ya afya iliyo bora zaidi kwa kuwa idadi ya wagonjwa na wajeruhiwa ni kubwa kiasi cha kushindwa kudhibiti ajali na kuongeza mzigo mkubwa katika huduma za utabibu.

Ukiangalia kwa jicho la tatu, utaona mengi zaidi kutokana na ajira hii ya pikipiki tofauti na ufanisi wa vijana kupata kazi ambayo si rasmi na salama. Kuna suala la kuvunja sheria, kuna suala la msongamano, kuna suala la biashara na fedha za vipuri, kuna suala la uzidishaji wa majukumu kwa vikosi vya usalama barabarani. 

Tuliingia kisiasa bila kuangalia athari na uelewa wa vijana wetu. Leo naomba uangalie hayo mawili, wasomi na uongozi na ajira ya pikipiki.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo