url-2Katika siku za hivi karibuni umekuwa ukifanya uteuzi kuziba nafasi nyingi za majipu ambayo umeyatumbua, kwa ufupi  umeifurahisha jamii ya walalahoi wengi walioteseka katika kipindi kirefu ndani ya nchi yao.

Majipu mengi ambayo yalikuwa yakitegemea majipu makubwa yamewanyanyasa sana wananchi kiasi cha wengi wao walikuwa wakijiuliza maswali yasiyokuwa na majibu juu ya mapato  ambayo wenzao walikuwa wakiyapata, wapo walalahoi ambao walidiriki kujiona ni wajinga mbele ya wenye nazo, ambao walikuwa wajinga pia kwa namna ambayo wanapata fedha hizo.

 Majipu ambayo uliyatumbua yana elimu kubwa na majipu mengi yaliyobakia yana elimu kubwa pia, yapo majipu mengine ambayo siyo majipu lakini yanaonekana majipu kwa sababu za kiuongozi, sheria za zamani na hatima za siasa zinawakwamisha kufanya majukumu yao.

Leo nitatoa ushauri ambao siyo lazima kiongozi wangu uufanyie kazi lakini ni vema nikatoa maoni yangu kama mwananchi ambaye pia nina uchungu na nchi yangu kama wewe, kiutekelezaji ningeweza kufanya mimi kama ningekuwa na mamlaka uliyonayo wewe lakini kwa sasa natoa ushauri tu kama ambavyo wengine wanatoa ushauri kwako.

 Mheshimiwa Rais, kwangu mimi uongozi nauchukulia kama ni weledi wa kujua kutatua matatizo yanayowakabili wananchi anaoawaongoza na si vinginevyo, viongozi ni watu ambao wanatakiwa kuigwa kwa matendo yao, kiongozi ni kioo cha jamii.

Ulipoingia Ikulu kwa mara kwanza kama Rais, siku chache tulianza kuona matokeo ya watu kukimbia rushwa, nikaamini tunahitaji mtu mmoja tu mwenye mamlaka ambaye akisema rushwa

 basi kinachofuatani utekelezaji, kwa ufupi sasa hivi wapokea rushwa wamepungua kwa asilimia kubwa sana kiasi cha kumfanya mtoa rushwa kujiuliza maswali mengi sana kabla ya kutoa.

Mheshimiwa kwangu mimi siamini sana uongozi katika elimu, wasomi wetu walipaswa kutoa ushauri wa kiujuzi zaidi badala ya ushauri wa kiuongozi, kwanza tuna wasomi wachache lakini

 pia msomi ana msimamo wa kuamini kile anachokijua zaidi kuliko kutafuta mbadala wake, wasomi ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa lolote lakini uongozi pia ni karama ya

 mwenyezi Mungu ambayo hampi kila mtu.

 Ni ukweli kwamba taifa letu limeongozwa na wasomi tangu tunapata uhuru wetu, na bado taifa linapiga hatua za kuruka na siyo za kutambuka, hii inatokana na ukweli kwamba tulikuwa na wasomi viomngozi ambao hawana karama ya uongozi, ni vigumu kunielewa lakini ukweli ndio huo, usomi na uongozi ni vitu viwili tofauti.

 Jambo la pili ambalo ningependa nishauri kwa ufupi lakini sina hakika nalo sana ni jinsi ambavyo majipu mengine yanavyoponzwa na watu wa chini yao wasio waadilifu lakini walikuwa wakilindwa na watu, hili najua unalijua vizuri sana kwa kuwa umekuwepo serikalini kwa muda mrefu.

Wapo ambao bila shaka yoyote maamuzi yao ya kiutendaji yalitekwa  na nguvu za kisiasa, wawekezaji wenye mkono mrefu, wenye nguvu za kimadaraka ya kukasimishwa na hata nguvu ya fedha, hawakuwa na namna yoyote ya kupingana nanguvu ya wenye meno. 

Katika utumbuaji ni vema vijana wako wakafanya uchunguzi wa  kina na kutoa taarifa sahihi, hiyo itasaidia waliokuwa waaminifu kiutendaji wasikate tamaa na jamii kuwatenga na kujiona wamelikosea sana taifa na kumbe siyo hivyo.

 Majipu ni mengi na wala siyo kila mahala ni wakuu, sehemu nyingi ni zile ambazo viongozi wa zamani waliwekeza ajira kwa watu wao na wakawa Miungu watu wasiogusika, hili halinaubishi kila mtu analijua na iwe siri yake.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri