Huwa napenda sana kuingia katika vikundi vya watu vinavyojadili hoja mbalimbali za siasa, michezo, jamii na utamaduni. Kuna wakati pia huwa najihusisha hata katika makundi yanayofanya majadiliano ya utani ili niweze kucheka.

Mtu akibaki kimya ni vigumu kuelewa uwezo wake wa kutafakari mambo, kwa kuwa haongei na huwezi kujua anawaza nini katika hoja ambayo iko mezani kwa wakati huo, inawezekana aliyebaki kimya akawa hajui chochote katika yale yanayozungumzwa au akawa na upeo wa juu kuliko wote mnaojadili jambo hilo.

Nakubaliana na wanafalsafa ambao walinena kauli hiyo, mimi binafsi ni mwoga sana kuanza kuropoka ninachojua mbele ya wajuvi kwa kuwa labda yupo mjuaji anayejua ninachoongea kwa kujiamini kuliko mimi, na pengine nikawa nimemwaga mchele wa ujinga wangu kwa kuku wajuvi.

Hivi karibuni tumeshuhudia watu wengi wakiwa katika midahalo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa wakijinasibu kwa kile wanachokijua, baadhi yao wanajua wanachoongea na wengine wanakisia jambo ambalo wanaongea, pasi na aibu huwa wanaamini kwa kile wanachokijua wao kwa uelewa wao na ujuvi wao.

Katika midahalo na majadiliano hayo, wakati mwingine hujadili hatima ya maisha ya watu, hujadili hatima ya maendeleo ya watu, hujadili mambo ya msingi kwa mustakabali wa mwananchi, hujadili mizozo mikubwa katika jamii ambayo huleta athari kubwa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni na kadhalika.

Kuna watu wanapewa nafasi ya kutoa mawazo yao, wakati mwingine siyo lazima kuipokea nafasi hiyo kama unaona maji yamezidi kipimo, kuongea upewapo nafasi siyo lazima na inaweza ikakupa heshima zaidi kuliko kuongea pumba kwa kigezo cha kutumia nafasi uliyopewa.

Nchi yetu sasa hivi imevamiwa na wimbi la kila mtu kuwa mwanasiasa, mwanaharakati, mwanasheria na kila aina ya taaluma, inanipa wakati mgumu kuona mtu anazungumzia masuala ya afya wakati yeye kitaaluma ni injinia wa madaraja, unazungumzia masuala ya kihistoria wakati wewe kitaaluma ni mpishi, unazungumzia masuala ya kiuchumi wakati wewe ni mbobezi katika masuala ya ukunga.

Huku ni kuvamia taaluma za watu na kutaka kuleta maafa badala ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayotukabili, kibaya zaidi ni pale unapozungumza kama mhitimishaji katika jambo ambalo hulijui kama kiza cha manani.

Kwa kuwa waongeaji hudhani kwamba kutumia muda mrefu kuzungumzia jambo fulani asilolijua ni sifa, basi hujinasibu na kutoa mifano ambayo inakera kwa mtu ambaye anajua kitu unachokizungumzia kwa kubahatisha-bahatisha.

Kama ni mwanasiasa, anatakiwa kujua anachozungumza katika siasa lakini lazima ajue hakuna siasa bila uchumi, utamaduni, afya, teknolojia, historia na kadhalika. 

Hakuna siasa ya kuropoka usichokijua, hakuna siasa ya kudanganya dunia ya leo, hakuna siasa ya kusifiwa bila kujua unachokizungumza, siasa ni pamoja na kuwa na mwanga wa unachozungumza. Kwa ufupi, unatakiwa utoe mawazo ya kile ambacho una ujuvi nacho katika kipengele cha siasa.

Mimi namheshimu sana anayeweza kusema hajui kitu kwa maana ya kutaka kuelekezwa, namsifu sana anayesikiliza zaidi kuliko kuongea jambo ambalo halijui, namsifu sana anayesema anaongea kitu anachokijua kidogo na kama yupo anayeelewa zaidi anaomba afafanue vizuri, kutojua siyo upumbavu ni ujinga kwa sababu ukijua ujinga utakuondoka.

Hivi sasa kila mtu anajua kila kitu, sijui ni kutokana na maisha magumu au ni maslahi ya kimaisha, muuzaji anajua anachokiuza hata kama hajawahi kukitumia au kukimiliki, mgonjwa ni daktari mzuri anajitibu kwa kumshauri daktari, mwizi ni mwanasheria na polisi yeye mwenyewe, kwa hiyo kazi yake ni kuelekeza kile anachokijua.

Hivi sasa kila mwanasiasa anatoa maelezo anayopima kwa uwezo wake kuwa ndiyo sahihi kwa wakati anaotoa maelezo, hivi sasa kila mtu anazungumza mambo kutokana na mazingira aliyopo na yanayomzunguka bila kujali athari ya kesho au jana.

Hivi sasa kila anayependwa ni mwanasiasa anataka aajiriwe na siasa hata kama kupendwa huko kunatokana na michezo, unyange, umaarufu na kadhalika. Hili silipingi, ninachopinga ni kutoa mawazo bila kuzingatia taaluma usiyoijua, athari zake ni za milele kwa kizazi kingine.

Chondechonde midomo na maisha ya watu, siyo lazima lazima uongee ndiyo tujue uwepo wako, unaweza ukawapo hata kwa kusikiliza mambo ya shule za watu, kuongea sana unaweza ukapitiliza ukadhani unaongea kijiweni kumbe uko na watu makini.

Ni mawazo yangu tu, siyo lazima uyakubali.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo

By Jamhuri