Nimejifungia hapa ndani wiki ya tatu sasa, ninadhani kwa sababu ninaelewa kauli za viongozi wangu juu ya afya na kujikinga dhidi ya maradhi haya yaliyojitokeza nchini. 

Tumeambiwa kabisa wazee tuko kwenye hatari zaidi ya kuumwa na kupoteza maisha kama tukishikwa na corona. Sababu kubwa ni kwamba kinga zetu ni dhaifu kuliko za kundi la kuchapa kazi.

Kwa hiyo pamoja na kukaa karantini, binafsi nikiri kwamba maisha ni matamu. Hakuna anayekubali kufa kwa sababu za kujitakia tu, ikitokea inaitwa isivyo bahati katangulia mbele ya haki kwa makosa mbalimbali ya kuchekesha.

Wiki hizi tatu nimekumbuka mambo mengi sana, na katika kipindi hiki nimegundua kuwa wenzangu wengi sana wametangulia mbele ya haki kwa sababu suala la kukaa nyumbani kama karantini halijapitiwa na walio wengi.

Waziri Mkuu alipotangaza karantini na wanafunzi kufunga shule kwa siku zaidi ya 30 kuna watu walianza kuhoji na kuleta siasa nyingi sana. Kwa sisi wazoefu wa matatizo ya majanga kama haya tulielewa mara moja, lakini kwa hawa vijana wa Dotcom ulikuwa mtihani na ikabidi nijiulize, hivi kizazi hiki ni cha mwaka gani?

Wakati nikitafakari haya nikagundua kuwa watu wanaoitwa wazima leo hii ni wale ambao walizaliwa wakati tukimaliza vita ya kukomboa eneo letu la Kyaka na kuwasaidia Waganda kumwondoa nduli Idi Amini katika ardhi yao. Kwangu hiyo ni kama juzi, ninahisi nimelala na kuamka tu.

Tuliozaliwa zamani kuna vitu vingi sana tumeviona na kuvipitia. Kwa hiyo karantini hii si kitu kwetu, bali ni jambo la maana na la kimaendeleo kwa taifa letu, kwa sababu moja, kati ya vitu vinavyoweza kufanya taifa likaendelea ni pamoja na idadi ya watu. Leo China ina mtaji mkubwa wa watu kuliko fedha labda.

Sina kumbukumbu vizuri, lakini ninakumbuka mafungio kama haya yaliwahi kutokea miaka michache baada ya uhuru kwa tatizo la kiafya. Ulikuwa ni ugonjwa wa ndui kama sikosei, tulikaa ndani mpaka tulipopewa chanjo ya ugonjwa huo. 

Hakuna aliyekwenda shule na hakuna aliyeonekana akizurura ovyo mitaani. Sina hakika kama ilitokana na kutoishi katika vijiji vya ujamaa au la! 

Lakini wakati huo kila mtu alikuwa na makazi yake na huduma za jamii zilikuwa zikitolewa kwa shida sana kutokana na kila mtu kuishi anakotaka. 

Tulikaa majumbani tukiwa hatuna taarifa za mara kwa mara juu ya ugonjwa huu mpaka pale tulipotangaziwa kutoka kwa ajili ya chanjo. Shule zilifungwa, makanisa na misikiti ilifungwa, kulikuwa hakuna gulio tena, ni neema tu ilitufikisha kwenye chanjo na maisha haya ya leo.

Baada ya sekeseke lile kupita ilituchukua miaka kadhaa kukabiliana na sekeseke jingine linalokabiliana na hili nalo lilikuwa homa ya matumbo, hili ndilo lilikuwa tatizo kubwa katika kipindi chetu. 

Ninadhani tatizo hili haliwezi kufananishwa na corona hata kidogo, hili ndilo tatizo ambalo liliwahi kufyeka idadi kubwa ya wazalendo wa taifa hili.

Shule zilifungwa na mipaka ya nyumba na nyumba iliwekwa, kila familia ilijitegemea mpaka tulipojua kwamba ugonjwa huu unasababishwa na kujisaidia nje na kwamba unaambukiza kwa haraka. Iliitwa harambee ya kuchimba vyoo kila nyumba na kutumia majivu kuua wadudu. Kwa jinsi hali ilivyokuwa hakuna aliyeweza kwenda kuchimba kwa mwenzie au kufanya kibarua, kila mtu alichimba yeye na familia yake, kila nyumba ilijua thamani ya kuchemsha maji ya kunywa, Homa ya matumbo ikaondoka kama ambavyo ndui ilivyotutesa.

Tukahamia katika vijiji vya ujamaa huku tukiwa na amani, tukiamini tumepambana na vita kubwa mbili ambazo haziwezi kuja tena, ndui na homa ya matumbo, lakini haya ni majanga ya kawaida katika maisha. Hatukuamini kama kuna lolote linaweza kuja tena kutikisa Tanzania yetu hadi pale tulipokuja kuingia katika vita na kujikuta kila mtu anatakiwa kupigana pale alipo.

Nayo ilipita, lakini kilikuja kindumbwendumbwe kingine cha asiye na mwana kueleka jiwe, sijui tatizo la ugonjwa wa kichaa cha mbwa ulitokea wapi. 

Shule zilifungwa, watoto tulijisaidia ndani, wananchi hawakulima ili mradi mambo yalikuwa tafrani, vijibwa vyenye kichaa vilijaa kila kona, watu wa mifugo, polisi, mgambo, wanyamapori na maliasili walijaa mitaani na kuwapiga risasi mbwa wote waliokuwa wakizagaa.

Hapa shule zote zilifungwa na dawa pekee iliyofanikiwa ni kuunga mkono jitihada zote za ushirikiano katika mapambano, suala la corona kwangu mimi ni dogo ila tatizo ninaliona kwa vijana na ugeni wa maradhi na kila mtu kuwa mwanasiasa na daktari katika hili.

Naamini nalo litapita na shule zitafunguliwa.

Wakatabahu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

677 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!