Mara nyingi nimekuwa nikishuhudia sifa
nyingi sana za mtu pale ambapo ndiyo
kwanza tumemaliza kutupia chepe la
mwisho la mchanga katika kaburi lake.
Huwa inakuwa hotuba nzuri ya kutia
simanzi juu ya uwepo wake alipokuwa hai
na jinsi ambavyo nafasi yake itapata tabu
sana kuzibika. Ni maneno yenye faraja
ambayo kama mfu angepata nafasi ya
kuyasikia, nadhani angeelewa umuhimu wa
maisha yake pasipo ukweli alioondoka nao.
Nayasikia maelezo mengi ya wanandoa
ambao wameachana na jinsi ambavyo sasa
kila mmoja anajaribu kumzungumzia
mwenzie huku akiwa katika ndoa nyingine.
Anazungumzia mambo mema ambayo
anashindwa kuyalinganisha na mambo
mapya aliyonayo katika ndoa nyingine
mpya. Kwangu hili nadhani ni adhabu nzuri
ambayo binadamu anaipata hapahapa

duniani. Pia ni faraja kwa mtalaka ambaye
labda alipewa hukumu kubwa na sasa
anasikia mwenyewe mambo mema
yanayomhusu tofauti na mfu aliyefumba
macho na masikio.
Leo nimeamua kuandika waraka huu ili sisi
binadamu wanafiki tunaotoa sifa kwa mtu
aliyetangulia mbele ya haki tujirekebishe na
ikibidi tutumie fursa tulizonazo kusema
mazuri ya watu wakiwa wangali wazima na
wao waone kwamba jamii inakubali ukweli
wa mema waliyotenda.
Lakini ni binadamu hawa hawa waliokithiri
unafiki kwa kuwapandikiza mema hata wale
waliotenda maovu na kuonekana ni watu
wema na kuondoka kwao ni pengo kubwa
kwa jamii inayowazunguka, mathalani mtu
amepigwa kwa kosa la wizi na katika
mazishi yake linazungumzwa pengo lake
kama vile haliwezi kuzibika! Huu ni unafiki
wa hali ya juu, ni vema nyeupe tukaiita
nyeupe na nyeusi tukaacha ikawa nyeusi na
si vinginevyo.
Naandika barua hii nikiwa najua mazuri
mengi ya watu walio hai na sijawahi kusikia
watu wakienzi mema yao. Wapo viongozi

ambao kwa namna moja ama nyingine
katika utumishi wao wamefanya jambo
kubwa kwa jamii, tunasubiri nini au chepe la
mwisho ndipo tuyaseme? Hatuoni kwamba
itakuwa faraja kwao iwapo wataona
tukizungumza sasa mbele yao bila
kuumauma maneno?
Leo hii tunayakumbuka mambo mengi ya
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
tunamkumbuka katika haki na usawa, lakini
ni huyohuyo tuliyempa majina mengi ya
‘Haambiliki’ na ‘Mchonga’

, nafsi zetu sisi
wanafiki zinatusuta kwa kuona msingi mzuri
ambao upo na uliasisiwa na yeye, leo
pengo lake tunaliona kwamba haliwezi
kuzibika kwa sababu kujitoa kwake kule
ilikuwa ni zaidi ya kuuza roho yake.
Leo kuna viongozi wengi ambao wanafanya
kazi nzuri sana lakini hatutumii fursa hii
tuliyonayo kuwapongeza kwa kusema
bayana yale mema ambayo wanayafanya.
Tumefumba midomo tukisubiri ama
wastaafu au wapoteze maisha yao ndipo
tuzungumze kwa hisia.
Leo tuna wahalifu wengi ambao tunajuta
kuishi nao mitaani kwa hofu ya maisha yetu

kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi na
kadhalika, lakini siku ikitokea wametangulia
mbele ya haki, tutaanza kuwasifia kwa
mema na si mabaya yao wanayotenda, huu
ndio unafiki uliokubuhu.
Mimi nadiriki kusema taifa letu limegubikwa
na idadi kubwa ya watu waongo, waoga na
wanafiki, wapo wanaosema mabaya ya mtu
lakini kwa chinichini, hawataki kupaza sauti
wakasikika kutokana na hofu kwamba
kufanya hivyo kutawasababishia matatizo,
kwangu mimi mtu wa namna hiyo ni
mchawi kwa unafiki huo.
Wapo watu wengi, tena wengine wakiwa si
watumishi wa kada yoyote, lakini
wamefanya na wanafanya mambo
makubwa katika jamii yetu na tumebaki
kimya bila kutamka. Wapo ambao
wamefanya na wanafanya kimyakimya
mambo yanayoisaidia jamii yetu kwa moyo
mkunjufu, lakini tumenyamaza ili tutamke
wema huo siku tutakayomalizia chepe la
mwisho makaburini, hii si sawa, ni unafiki
uliopitiliza.
Najua pia kwamba wapo ambao kazi yao
kubwa iliyowaleta duniani ni kujibatiza

mambo ambayo wao hawawezi kuyafanya
lakini wanatumia vizuri fursa ya waliofanya
kujitangaza kwamba wao ndio wakamilishaji
wa kila kitu. Hawa wanafiki tunawajua lakini
kwa unafiki wetu tunanyamaza, hatusemi,
tunakuja kusema kwa unafiki baada ya
chepe la mwisho.
Leo nimeamua kuandika waraka huu kwa
kuwa najua siri za watu mioyoni mwao
kuhusu kila tunayemzika au kustaafu,
tuseme ukweli tu hata kama unauma kwa
wachache.

Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.

1406 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!