Inawezekana huwa sipati usingizi, ninaota huku nikiwa macho makavu lakini naamini ninachokiona katika njozi zangu kina nasaba na ndoto ya maisha halisi yanayonigusa mimi na Watanzania wengine wengi.

Hii ndiyo Tanzania hata kama ni ya ndoto lakini ndiyo Taifa langu ambalo najivunia kuwa mzalendo kwayo, nauona uzalendo uliopotea unarudi kimya kimya katika damu yangu na ninaweza kutamka mahali popote kwamba mimi ni Mtanzania.

Ni kama ndoto kuamini kuwa sasa hivi kuitamka rushwa ni kama kupiga hodi kituo cha polisi na kuwatukana askari wakiwa katika mavazi ya kazi, ni ndoto tu kwamba Mtanzania niliyekuwa namjua mimi miaka kadhaa iliyopita, anaweza akahoji kwanini unamshawishi kupokea rushwa wakati yeye ni mtumishi wa umma na madaraka aliyonayo ni dhamana tu.

Kama naota ninapoona vurugu za kushindana kunywa pombe kwa maana ya kuchafua meza zimeanza kupotea na kuonekana kama ulimbukeni, au kichaa kufanya matumizi ya fedha kuwa ya kudadisiwa, hii ni ndoto kwa sababu maisha hayo yaliwezekana wakati ule ambao kila mtu alijitwalia mali za umma na kujimilikisha kwa amri zao wenyewe.

Naota lakini ni kweli kwamba madereva sasa wanafuata sheria, wanajua wajibu wao baada ya kuvunja sheria za barabarani kwamba ni faini na kufungwa, ule ujinga wa zamani kila mtu kutembea na sheria zake kichwani umeanza kupotea, sasa hivi barabarani tunaanza kuheshimiana na kupeana nafasi kama madereva tuliopitia vyuoni.

Unaweza ukafikiri kuwa si ndoto, lakini usiku mmoja wa mwaka jana na leo unaleta hadithi nyingi za kufikirika, kwamba yule tajiri wa jana ambaye utajiri wake ulikuwa wa shaka sasa haonekani, na kama anaonekana basi zile mbwembwe za kutishana hazipo tena, kuulizana majina na kudharauliana kumekwisha.

Ni kama usiku wa jana na kuamkia leo umewafanya Watanzania kuelewa umuhimu wa kulipa kodi, zamani ikitajwa kodi ilikuwa ni kwa ajili ya mtu wa chini, baadhi ya matajiri wetu wasio waaminifu walikuwa hawalipi kodi na walijipatia faida kubwa kwa kipindi kifupi, hii kwangu mimi ni ndoto.

Inawezekana kweli nikawa naota nikiwa macho, lakini ni muujiza gani uliotokea kiasi cha kuwafanya watoto wetu wakae katika madawati badala ya kukaa chini ambako tulizowea kwa muda wote? Ni ndoto tu ninapobaini kwamba baadhi ya mashirika ya umma sasa hivi yanaweweseka kufanya hesabu za fedha zikae vizuri kabla ya mkono wa sheria haujapita na sindano ya kutumbua jipu. Kuweweseka huku ni kama ndoto ya mkubwa kuguswa na nguvu ya mnyonge.

Ni ndoto kabisa naiona japo inawezekana nikawa macho, kwamba muda mfupi ujao Serikali hii itakuwa imehamia Dodoma, na kwamba Dar es Salaam tutaachiwa wazee wa mjini tupigane kibiashara, ni ndoto lakini inawezekana kwa sababu sasa hivi ofisi nyingi zipo wazi na gharama za kupanga ofisi zikiwa  zimeshuka sana.

Naona Watanzania waliokuwa wamezowea kukaa vikao vya bia na kahawa baada ya kazi wakibadilika na kuanzisha utaratibu mpya wa kuwahi nyumbani au kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimarisha afya zao, ni jambo jema kwa taifa lolote kuwa na wananchi wenye siha njema kiuchumi.

Ni kama naota ninavyoona maisha ya kufikirika kwa Watanzania, mafanikio bila kufanya kazi, mafanikio ya dili yakiwa yanapotea, na wengi wetu kufikiria kufanya kazi na kuwa maisha ya ratiba kama mataifa mengine yaliyoendelea, naota maisha ya kubweteka yanaanza kuwakimbia watu wavivu.

Ni ndoto kwamba kila Mtanzania anafikiria kilimo na ufugaji kama njia pekee ya kujiongezea kipato, anafikiria shamba kama miaka ile ya kilimo cha kufa na kupona, ndoto ya ajabu leo kumsahau mkulima kama mtu mshamba, ni ndoto kuamini kuwa jembe halimtupi mkulima.

Ni ndoto kwangu japo sioti, lakini ndiyo uhalisia kwamba masuala ya bajeti yametamalaki katika nyumba nyingi za Watanzania waliozowea kutumia bila kufanya hesabu, ni ndoto kwa kuwa ni juzi watu walikuwa wakicheza na hela lakini sasa wanaitafuta kwa jasho.

Sijui hii ndoto itanifanya niamke nikiwa katika taifa lenye maendeleo au taifa lenye umaskini mkubwa kuliko ule, nasubiri niamshwe kukicha kama kweli nimelala.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo. 

983 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!