Yah: Siasa za wanasiasa baada ya uchaguzi, ni dhambi

Nianze kwa kuwapa hongera wananchi wote kuyakubali mabadiliko yaliyotokea pasi na mnadi mwingine ambaye inasemwa na wanasiasa kuwa kadandia ajenda yao mbele, lakini pia inawashughulikia kama wengine waliokuwa na maisha ya kujiongeza binafsi.

Hii dhana ya mabadiliko imekuwa ngeni kivitendo, japokuwa kikauli ni kama wimbo uliozoeleka kwa watu wengi wanaotaka kujulikana kwa maana ya umaarufu, walianza wanasiasa kuinadi kwa nguvu kwa ahadi kuwa; ili nchi iweze kupata maendeleo hatuna budi kuyakubali mabadiliko ya kimfumo ndani ya Serikali.

Walipokuwa wakisema kaulimbiu hii, umati wa waathirika na utawala wa Serikali waliunga mkono hoja hiyo wakiamini kuwa  matokeo ya mabadiliko hayo ni maendeleo binafsi – wanyonge kuneemeka, matajiri, wala rushwa kufilisiwa, wanaoishi kwa magendo kukiona, watumishi wa umma kubadilika namna ya utumishi wao na mengine mengi.

Ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais Magufuli inawezekana alivamia ajenda yao kwa mbele na utekelezaji wake inawezekana ikawa umepita malengo ya wale wenye ajenda, kutokana na machungu ambayo yametofautiana baina ya wenye ajenda na aliyeichukua ajenda yao, watu wengi wamekubali matokeo na wengi wanapinga juu ya utekelezaji wake wakiwamo wenye ajenda.

Misukosuko hii ya wanasiasa inaonekana pale wanapodai demokrasia ya kuwa na muda mwingi wa kuzungumza siasa badala ya kufanya kazi, aliyedaka ajenda yao alikuwa na kaulimbiu ya ‘hapa kazi’, huenda alisema hapa kazi tu baada ya siasa za uchaguzi kufikia ukomo wake, anatutaka tufanye kazi ili tuondokane na umaskini.

Katika barua zangu kadhaa, niliwahi kuhoji juu ya kauli hizi ambazo niliona kama ni kauli tata, kwamba nchi yetu ile ya uwajibikaji na ujamaa wa kweli inawezekana ikarudi? Niliwahi kuuliza ule uzalendo wa kweli kwa Taifa letu uliishia wapi? Nilisema sana juu ya uhujumu uchumi ambao tuliupiga sana vita, imekuwaje sasa umeshika kasi ya ajabu?

Katika barua zangu niliwahi kusema juu ya wananchi na siasa za leo na juu ya wachache kugeuza siasa kuwa jukwaa la ajira, niliwahi kuhoji uhalali wa nguvu kazi kubwa kuteketea katika mfumo wa mageuzi ya kisiasa, kwa kigezo cha mfumo wa vyama vingi na haki ya kidemokrasia ya kutoa mawazo na kushiriki katika siasa.

Huyu aliyedandia hoja ya wengine katika uchaguzi ameamua kuchukua wajibu wa kutekeleza hoja yake ya hapa kazi tu kwa mabadiliko, cha moto tunakiona kutokana na ukweli kwamba tulizowea siasa ya maneno na siyo vitendo, cha moto tunakiona kwa kuwa hatukuwa tayari kuyakabili mabadiliko ya kweli na siyo ya mdomoni.

Baadhi ya wanasiasa wetu wameshindwa kwenda na kasi ya mabadiliko kutokana na mazowea ya kuongea mabadiliko midomoni. Ili kuweza kuipata kasi hiyo wanatupia lawama wananchi ili wawabebe katika kipindi cha mpito wa mabadiliko, wanawapelekea lawama viongozi wa Serikali ambao siyo wanasiasa, wanataka siasa iendeshe Serikali badala Serikali kuiendesha nchi.

Sasa hivi ajenda kubwa kisiasa ni kupata fursa ya majukwaa na kuwashawishi wananchi – iwe kwa heri au kwa shari – lakini muda wa siasa za uchaguzi umeshapita na wanasiasa wanapaswa kuacha kunadi sera na badala yake wanapaswa kuwasisitiza wananchi kutekeleza sera za chama ambacho kilishinda katika uchaguzi.

Kuendelea kutumia sera mpya ambazo kamwe hazitatumika katika kipindi cha miaka mitano, ni sawasawa na kupoteza muda wa maendeleo kwa miaka mitano, hivi sasa sera za chama kilichoshinda ndizo zinazoongoza nchi, wanasiasa wote walioko bungeni wanapaswa kusimamia utekelezaji wa sera ambazo zilikiingiza chama katika utawala.

Bila kuzingatia itikadi za kisiasa na chama, wote tunapaswa kufuata sera za chama kilichoshinda, hiki siyo kipindi cha kuendelea kubishana kwa kuwa kimsingi miaka hii mitano ni ya chama kilichoshinda na tunapaswa kufuata sera hizo na kuzitekeleza hadi hapo uchaguzi mwingine utakapowadia na wananchi kuchagua sera nyingine zitakazonadiwa katika majukwaa ya siasa.

Baada ya miaka mitano, wale ambao hawakutekeleza ahadi za sera zao tutawahoji na kuwanyima kura ili tuwape wengine ambao nao tutawaangalia utekelezaji wa sera zao kwa kipindi cha miaka mitano. Siasa baada ya uchaguzi ni ugaidi kwa wananchi wanaosubiri maendeleo yao.

 

Wassalaam, 

Mzee Zuzu,

Kipatimo.