Nianze kwa kuwapongeza vijana ambao kwa mara ya kwanza wametambua kwamba ni wawakilishi kwa maana ya mabalozi wetu waliokuwa wakipigania mafanikio ya taifa.

Nawapongeza sana na tumeona ni jinsi gani ambavyo pamoja na jitihada zote kubwa walizokuwa nazo tumeshindwa kufanikiwa kuendelea kupeperusha bendera yetu kimataifa. Si jambo baya kwa sasa kwa kuwa bado tu wachanga katika vita ambayo wengine wameizoea kila wakati.

Nawapongeza kwa sababu wameonyesha kuwa ni wazalendo, kila walichokifanya kwa kila mmoja alikuwa anawakilisha taifa. Wapo ‘waliopigana’ uwanjani na wapo ‘waliopigana’ nje ya uwanja, wote hao nia yao ilikuwa moja, kuhakikisha taifa letu linafanya vizuri na kujulikana uwepo wake katika dunia ya michezo.

Sifurahii sana maneno ya baadhi ya wenzetu ambao wanaona kama walikwenda kufanya utalii na wapo waliofikia kukebehi juhudi za wenzetu kwa kusema wamefungwa michezo yote mitatu. Nadhani hiyo si kauli nzuri na haina afya kwa mustakabali wa umoja wetu na juhudi za kuendelea kuwa wamoja.

Taifa hili halikujengwa hivyo, lilijengwa kwa uzalendo zaidi hadi tukafikia hata watu wengine wasio wa taifa hili kujiona wana fahari ya kuwa Watanzania.

Katika miaka ya nyuma taifa liliwahi kuingia katika vita kubwa ya kutetea ardhi yake, katika kutetea kule tulituma wanajeshi wachache wakapigane na wengine tulikuwa tukipigana kuhakikisha hatuwashushi moyo walioko mstari wa mbele na tulihakikisha tunaandaa chakula kwa ajili yao na tuliwapongeza waliorudi katika majeneza kama watetezi wa taifa letu.

Huo ndio ulikuwa Utanzania ambao mimi nilikuwa naujua vizuri, tofauti na huu wa kejeli na matusi ambao ninauona leo. Sijapenda, kwakuwa wapiganaji wetu hawakwenda kwa nia ya kushindwa, pamoja na kwamba ulikuwa ni mchezo lakini machozi na jasho lilikuwa ni kwa ajili ya kutetea taifa. Maumivu waliyoyapata baadhi yao ilikuwa ni kwa ajili ya Tanzania, huo ndio uzalendo ambao tunatakiwa kuufanyia kazi na kuwapongeza wenzetu ambao wamerejea na uchungu wa kushindwa kufika mbali katika mashindano hayo.

Tatizo ambalo limesababisha kutofika mbali linajulikana, lisiwe la kisiasa, bali liwe la kisera. Katika nchi hizi za ukanda wetu miaka ya nyuma kidogo tulikuwa tunafanya vizuri sana katika michezo mingi kutokana na sera ambazo tulikuwa nazo katika michezo. Tulikuwa na walimu wa michezo kwa ngazi zote, kuanzia elimu ya msingi mpaka maeneo ya kazi. Tulikuwa na mashindano mengi katika kila rika na tuliweza kuibua vipaji vingi sana katika michezo mbalimbali.

Tanzania tulikuwa mabingwa wa dunia katika riadha, tulifika AFCON kwa mapambano hasa ya makundi na tuliweza kuonekana katika michezo mingine kama ya kutupa tufe, hii ilitokana na sera ya ukuzaji michezo katika viwango vyote.

Zamani serikali ilitenga maeneo ya michezo mingi, watoto walicheza na kukuza vipaji vyao, ilikuwa ni aina ya vituo vya ukuzaji vipaji kwa watoto ambavyo leo tunaona katika mataifa mengine kama vitu vya ajabu. Kila kijiji kilikuwa na uwanja au viwanja, kila umri waliweza kujifanyia michezo baada ya kazi, kila shule ilikuwa na uwanja wa mpira wa miguu, netiboli, mbio, kutupa tufe, kuvuta kamba na michezo mingine, lakini zaidi kila shule ilikuwa na mwalimu wa michezo na hata wilayani tulikuwa na ofisa michezo. Hiyo ndiyo ilikuwa nguzo ya kufanya vizuri katika michezo kwa ukanda wetu ambao kwa umri wangu niliamini miaka hii tungekuwa tunashiriki mashindano ya Kombe la Dunia, hata katika mbio labda Kenya wangekuwa nyuma yetu na ndondi tungekuwa na vijana wazalendo ambao wana mikanda kadhaa ya ubingwa.

Nadhani tumejifunza jambo kubwa katika michezo hii. Kuna mahali pakubwa sana tumekosea, tumepoteza vipaji na walimu wa michezo, tumepoteza hamu ya michezo kwa Watanzania na zaidi tumekuwa tukiokota vijana wanaojaribu kutokana na juhudi zao binafsi bila mchango wowote wa kusaidiwa na waendeleza vipaji.

Hawa waliorudi na heshima hii tuwapongeze kwa kiasi chao cha juhudi, tumejifunza kitu kutokana na makosa haya, tusiwe na sababu yoyote huko mbele wakati tukijua sababu zinazotukwamisha leo, turudishe michezo shuleni, vyuoni, jeshini, kazini na vijijini, michezo si kwa ajili ya mashindano tu, ni kwa ajili ya afya pia.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo. 

348 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!