Wakati tunatawaliwa, wakoloni wote kwa awamu zao yaani Wajerumani, Waingereza na hata Wareno na Waarabu, wakati wakipita kwa biashara zao sisi Wazaramo na Wandengereko tulikuwa tunawasiliana kwa shida sana. Kuna wakati tulikuwa tunatumia lugha ya alama kuwasiliana. Baada ya kuanza kutafuta uhuru wetu na kukataa kutawaliwa tuligundua kuwa kikwazo kikubwa cha uhuru ni mawasiliano. Hivyo, kwa busara za watu wachache wakaona ni vema tukawa na lugha moja ya mawasiliano ili tuweze kuelewana na kuweka mipango mkakati ya pamoja kwa nia moja. Tanzania ilikuwa na makabila madogo madogo zaidi ya 120 na makabila haya madogo yalikuwa na machifu wenye nguvu katika himaya zake.

Lakini kwa busara zao bila kuwa na elimu ya kisasa waliona ni jambo jema kuwa na lugha moja ya mawasiliano ili kupata uhuru wetu. Ni hekima ambayo haikuhitaji elimu ya dot.com. Leo tumepata uhuru wetu kwa amani na mshikamano wetu wa wakati ule, jitihada zilizofanywa na Julius na wenzake akina Shaweji, Bomani, Kawawa na kadhalika tumezisahau.

Haikuwa kazi rahisi kama ambavyo wengi wanadhani. Ilikuwa kazi ngumu kupokewa na watu wachache waliokuwa na mtazamo wa kuona kama bado wanatawaliwa na utamaduni mwingine. Leo nimeamua kuzungumzia utamaduni ambao tunaelekea kuununua huku tukijua kuwa unaturudisha tulikotoka. Unaturudisha katika utumwa tuliokataa, tunarudishwa na kundi dogo la malimbukeni ambao kwa yamkini na sina shaka kuwa hawakupata kuona madhila ya kutawaliwa. Lugha ni nyenzo ya mawasiliano na wakati huo huo, lugha ni kielelezo cha utamaduni wa mtu. Tupo katika wakati ambao tunatakiwa kuwa na mawasiliano ya jamii kubwa kwa wakati mmoja na mawasiliano hayo yanafanywa kwa jamii yenye utamaduni mmoja. Tunapaswa kuheshimu hilo. Makosa yaliyofanyika awali, tena makosa ya kupitiwa tu na baadhi ya wenzetu kushindwa kutambua lugha ya Kiswahili katika Katiba yetu, tunapaswa kuyasahau na kuenzi yale ambayo sasa yanajadiliwa ikiwa ni pamoja na kuheshimu mawazo ya wenzetu kufanya lugha hii ya Kiswahili kuwa tunu ya Taifa. Hivi sasa tunajadili mambo mengi ya kitaifa, mambo hayo yanajadiliwa na viongozi wetu ambao baadhi yao ni wasomi. Wanajadili mambo hayo kwa manufaa ya Watanzania na sisi Watanzania ambao ni Waswahili tunataka kujua kitu ambacho kinajadiliwa kwa manufaa yetu. Bahati mbaya sana viongozi wetu wanasahau kuwa wao ni wawakilishi wetu kwa kujadili kwa lugha yao, hawajadili mambo ya nchi za Ulaya. Imekuwa ni jadi kutuchepusha na kutuacha njia panda tusijue kinachoongelewa kwa lugha yao na hatima waliyofikia katika majadiliano yanayotuhusu sisi. Mataifa mengi duniani yanatafuta suluhu ya lugha moja ya mawasiliano ili waweze kuwa wamoja, wanashindwa kutokana na kasumba ya watu wachache kudai lugha yao ya kikabila kuwa ya Taifa.

Tanzania tuliweza hilo na kuua makabila makubwa ya Tanzania ambayo yalifikiri yanaweza kutawala nchi kwa lugha yao na utamaduni. Juhudi hizi zilifanywa na watu wachache mashujaa ambao duniani wanaheshimiwa kwa kazi hiyo. Mataifa mengine yanashindwa na yapo yaliyothubutu kukitaka Kiswahili kuwa lugha ya mataifa yao kama Kenya, Kongo na Afrika Mashariki kwa jumla. Nchini Kenya waliweza kuthubutu kuiingiza katika Katiba kabla yetu. Makosa yaliyofanyika ya kutindikiwa na kuacha matumizi ya Kiswahili kwa kasumba ya watu wachache tunapaswa kuyakataa na kuwaona wanaotumia lugha ya kigeni katika mambo yetu ya kitaifa kuwa ni maadui zetu wa utamaduni na kitaifa. Nawaomba wanangu mkumbuke kuwa lugha yetu ni hazina tosha ya maendeleo na wanaokataa hawatutakii mema katika Taifa letu.

Wanaochepuka  na lugha yao tuwaache katika safari yetu ya maendeleo na ikiwezekana tuwatenge katika jamii yetu kwa kuwa wanaturudisha katika utumwa ambao tuliukataa. Ningependa kuona Kiswahili kinatumika bungeni kiufasaha kwa kuwa ndiyo lugha yetu. Ningependa kuona Kiswahili kinatumika katika Katiba kwa kuwa ni Katiba ya nchi yetu. Ningependa kuona majadiliano ya Katiba na kanuni zake yakijadiliwa kwa Kiswahili.

Wasalamu, Mzee Zuzu, Kipatimo.

1886 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!