Salamu zangu za mwezi Januari lazima ziwe za upole, kwa sababu ni hizi Januari za miaka ya hivi karibuni ambazo zimekuwa zina matatizo mengi kwa kizazi hiki. 

Sina hakika na sababu zake, lakini labda ni kwa sababu watu hawalimi au ni wafanyabiashara tu. Enzi zetu hatukuwa na tofauti ya mwezi Januari na miezi mingine, kwa sababu tulikuwa na bajeti nzuri na mishahara midogo. Hatukuwa malimbukeni wa sikukuu, lakini pia sikukuu zilikuwa za kwetu sote, kwa maana ya ushirikiano.

Wakati huu wa mwanzo wa mwaka katika miaka yetu kulikuwa na matukio makubwa machache sana. Awali yalikuwa matokeo ya darasa la saba. Ndicho kipindi ambacho wengine walijua wamekwisha kuondoka kijijini kwenda mjini kusoma, na ndicho kipindi ambacho wengi walikuwa wanajua wanatakiwa kuanza kuishi maisha ya uanakijiji au kurudia darasa la saba. Hawa walikuwa maarufu kwa jina la ‘ma-repeaters’.

Kwa mnaokumbuka, hasa wale wa umri wangu, mtakubaliana nami kwamba ninadhani kulikuwa na tatizo katika miaka yetu kwa kutotoa alama na matokeo ya mtu mmoja mmoja katika mitihani yetu. Nakumbuka kulikuwa na ‘vipanga’ wa hatari, lakini utasikia darasa la saba wamefeli. Walikuwepo waliokuwa wanarudia hata mara nne lakini wapi, matokeo yalikuwa yanavuruga kijiji.

Enzi zetu ilikuwa shule tatu au nne zinafanikiwa kuwakilishwa na mwanafunzi mmoja tu ambaye alikuwa anafaulu. Wapo waliosema kwamba mwanafunzi huyo alikuwa anachaguliwa kutokana na kuamini kwamba wenye bongo kali walikuwa wengi lakini cha ajabu alikuwa anachaguliwa mmoja. Sina uhakika na hilo, na siwezi kulisemea hilo, kwa sababu sina uhakika na sijawahi kulifanyia utafiti.

Miaka ya hivi karibuni kumekuwa na matokeo tofauti kabisa na miaka yetu. Kuna madarasa ambayo wanafunzi wote wanafaulu kiasi kwamba tunabaki na maswali mengi kuliko majibu. Tunajiuliza, hawa wanaofaulu darasa zima ni bora kuliko wale wa miongo minne iliyopita au ni wingi wa shule na nafasi zilizopo ziweze kujazwa?

Alipohitimu mwanangu wa kwanza, ninasikia walimaliza wanafunzi zaidi ya mia tano katika wilaya yetu wakati huo na hakuna aliyebahatika kuchaguliwa kuendelea na masomo mpaka aliporudia mwanangu na wenzake kadhaa katika shule nyingine na mwaka uliofuatia kati ya wanafunzi mia nane ni sita tu ndio walipata nafasi ya kwenda katika shule ya upili.

Hii inaweza ikawa ni hadithi kwa wengine wa kizazi cha miaka ishirini iliyopita na wasinielewe ninazungumzia nini katika dhana ya ufaulu. 

Lakini jambo kubwa ambalo nimejifunza ni hili la mabadiliko ya mitaala ambalo linashindwa kumtofautisha mwanafunzi wa darasa la nne au la saba wakati huo na huyu ambaye leo amehitimu mafunzo ya chuo kikuu.

Kuna mambo mengi ya kujifunza hapa. Kwanza, zamani ili ufaulu ni kama ilikuwa ikijulikana kama una akili kijiji kizima, ni mtu ambaye alionyesha dalili zote za kufaulu na si kuchaguliwa. Lakini pia mitaala ilitufundisha kujitegemea, hasa katika masomo yetu. 

Nakumbuka masomo kama kulima shamba na bustani, kujipikia, kuchonga, ufundi stadi wote na mafunzo ya kuishi porini.

Leo ni tofauti kabisa na zamani. Leo mtu anamaliza elimu ya juu lakini hawezi kuandika barua ya kuomba ajira pamoja na kwamba amesoma ili aje aajiriwe. Amesoma lakini hawezi kujitegemea wala kutatua changamoto ndogondogo zinazomkabili. 

Amesoma lakini hawezi kubuni mradi wa kufanya ili aweze kujitegemea na kuwasaidia wenzake ambao hawajasoma. Amesoma lakini hawezi kulea familia yake na kujilea yeye mwenyewe. Huu ndio mtaala mpya ninaoushuhudia ukiendelea kumwaga kundi kubwa la wahitimu mtaani.

Leo si ajabu kusikia darasa zima wamefaulu. Ni jambo la kawaida, lakini upande wa pili tunalaumu kwamba hatuna walimu. Leo vijana wanajua zaidi teknolojia lakini si mambo muhimu yanayowazunguka. Ninajua umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya taifa, lakini pia ninaamini elimu bora ndio ufunguo wa maendeleo ya taifa lolote.

Umefika wakati sasa tuangalie mitaala yetu kama inatufikisha mahali muhimu. Kama mitaala hii haiwezi kumfanya mtu aliyehitimu elimu ya juu kuishi na mke na watoto wake, basi tuifute tuanze upya. Mitaala yetu ilikuwa ukimaliza darasa la nne au la saba tuliweza kuishi na familia zetu na hatukuwa na watoto wa mitaani.

Tumekwama wapi?

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

81 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!