Nimesikiliza hotuba nyingi  na za viongozi wengi walionona sura zao kwa maisha ya hali bora, wakijaribu kutuzungumzia walaji wa matunda ya umaskini na jinsi  tunavyoteseka. Wote nawakubali lakini ni vema nikatoa tahadhari kuwa hayo maisha magumu wanayotuzungumzia wamehadithiwa hawayajui kabisa.

Mimi ni mwananchi wa kawaida kabisa, mwananchi ninayejua machungu ya ugumu wa maisha, maisha ambayo hao wanaotuzungumzia kamwe hawawezi kuthubutu kuishi hata kwa siku kadhaa. Mimi ni mwananchi ninayeishi maisha ya chini ya dola moja kwa siku, mwenye familia inayonitegemea — familia tegemezi ya mke na watoto. Mimi ni mwananchi ninayepaswa kulipa kodi kwa kile kidogo ninachokipata yaani chini ya dola moja.

Wastani huo wa chini ya dola moja natakiwa nihakikishe familia yangu imekula na kushiba bila kujali virutubisho vya vyakula, lazima nihakikishe wanatibiwa magonjwa ili familia yangu ninayoipenda iishi pamoja nami.

Ni lazima watoto wangu wasome japo elimu ya msingi wajue kuandika na kusoma, naogopa watakuwa wageni wa nani miaka ijayo, katika suala la elimu ambalo limeshindwa kudhibitiwa na hao walionona na kunizungumzia matatizo yangu ndiyo wameachia suala la ada kuwa la mafisadi wachache waendelee kuninyonya hako ka nusu dola kangu.

Wameshindwa kunisaidia kuweka ruzuku katika shule zetu kama ilivyokuwa zamani. Zamani enzi za mwalimu wa watu, enzi ambazo kalamu, daftari, rula, chaki, vitabu vilikuwapo bure shuleni, enzi ambazo mwalimu alilipwa vizuri na akafundisha vizuri, enzi za kufuta ujinga ambapo hata watu wazima walifundishwa bure elimu ya ngumbaru.

Wanasiasa walionona na kunisemea matatizo yangu hawajui jinsi ninavyohangaika kufanya bajeti ya nusu ya dola ninayopata kwa siku, kwamba hiyo naigawa kwa ajili ya chakula, elimu, afya, huduma za jamii kama maji, umeme na maendeleo ya nyumba za nyasi. Hawa ndiyo wanaozungumzia Dira ya 2025 bila kujua kama nitafika mimi pamoja na familia yangu.

Nusu ya dola ninayopata ndiyo ninayotakiwa kununua dawa ya mseto ambayo nilidhani kwa kodi yangu ninayotozwa na ahadi ya Serikali kuweka ruzuku yake katika dawa hiyo, ili nipate kwa bei nafuu, imeshindwa sasa pamoja na kuchangia kwa Serikali bado dawa ya mseto nanunua katika maduka yao kwa bei ya juu zaidi.

Hawa ndiyo wanaozungumzia maisha yetu ambayo kwa asilimia mia yana ubia na malaria kutokana na Serikali kushindwa kudhibiti mazalia ya mbu, ambayo yana kitengo maalum kikubwa na mbwembwe za wataalamu cha malaria, tunahitimishiwa maisha yetu kwa kaulimbiu ya ‘malaria haikubaliki’.

Mimi nawazungumzia wananchi ninaowajua kwa maana ya mimi kuwa miongoni mwao, wananchi tunaokula mlo mmoja kwa siku pamoja na watoto wetu, wananchi tunaomuomba Mwenyezi Mungu atupishilie mbali maradhi yanayoweza kukwepeka kwa nguvu za Serikali, wananchi ambao tunadhani kwenda kwa waganga wa kienyeji ni bora kuliko hospitali kwenye gharama tusiyoimudu. Hivyo basi, ugwadu na utamu wa tunda aujuae mlaji.

Mimi ni mwanachi ambaye najua maana halisi ya ugumu wa maisha kivitendo na siyo kinadharia, siimbiwi wimbo nauimba mwenyewe, kula yangu shida, matibabu Mungu nisaidie, elimu bora liende, afya kazi ya Mungu, kupata ni majaliwa, na kulala na njaa ni funzo kwa watoto wetu kujua maisha yakoje.

Mimi kwa niaba ya wenzangu tunawaona nyie kama watu makatili, mnaozungumzia urahisi wa maisha bila kujua uhalisia uko wapi, mbwembwe za suti, posho, misafara, ulinzi, vikao vya kutafuta suluhisho la matatizo yetu, rushwa, kukwepa kodi na matatizo yasiyotatulika kama ya maji safi, nishati ya umeme ni fadhaa kwetu.

Tulidhani Katiba ni suluhisho, tukalishadidia sana, tukaamua kodi yetu itumike huko ili tupate Katiba mpya itutoe hapa tulipo na tuwe na maisha ya afadhali kiasi, jitihada za mwenye nchi kiongozi wetu zimegonga mwamba. Kuna Usimba na Yanga lakini pia kuna kutugawanya kwa mawazo ya wachache kupata madaraka, zoezi limeshindikana, posho wamepata na kodi imetumika, huduma za jamii zimedorora, huo ndiyo mtihani wa mwanachi wa Tanzania mpenda amani na maendeleo.

Aluta kontinua Tanzania ya zamani tunaitaka hii yenu endeleeni nayo.

Wasaalam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri