Kweli nimeamini kama hawa Watanzania wakipata ufunuo wa kutumia demokrasia yao ya kutoa uamuzi, basi wanaitumia kama ipasavyo. Leo wanaweza wakaamua kitu kutokana na mazingira na kesho wakabadilika kutokana na mazingira shirikishi, hii ndiyo demokrasia iliyopo sasa bila kujali kama ina athari za kiutendaji ama laa.

Nimeipenda hii demokrasia ya sasa kuamua kama niendelee na chama hiki ama nihamie chama kile, katika mtiririko wa kuhama na kuhamiwa umekumbwa na vyama viwili tu, wengi wanatoka CCM na kwenda Chadema, na vyama vingine havipati wanachama wapya kutoka katika vyama vingine.

Sijasikia mtu akitoka chama kidogo na kwenda katika kimojawapo ya vyama hivyo, lakini pia sina hakika sana na wanachama wa kutoka Chadema kwenda CCM japokuwa najua kuwa wapo walioamua kufanya hivyo na wamefanya.

Kwa maoni yangu hii ni demokrasia nzuri sana, imefikia kiwango cha juu sana hapa nchini, haikupata kutokea tangu nchi hii ipate uhuru wake, demokrasia hii pia inapaswa kuhojiwa kwa mapana yake kujua uhalali wa wanachama wanaoingia na kutoka, miaka ya nyuma kulikuwa na usemi wa ‘pandikizi’ ambao kwa miaka ya sasa suala hilo imeonekana halina mashiko katika uhamaji huo.

Hivi sasa tuko katika mchakato; mchakato wa wagombea uongozi ngazi mbalimbali. Imekuwa kama ada fulani kuona kila anayekataliwa katika ngazi yake kupitia chama alichokuwamo awali kuhama na kwenda kutafuta malisho mapya kupitia chama kingine, naipenda hiyo demokrasia japokuwa baadhi yao hawajui kuwa kukataliwa na chama ulichokuwamo ni ishara tosha kwamba kwa sasa hutoshi kwa sifa zinazohitajika.

Japokuwa ni haki ya msingi ya kila mwananchi lakini katika hili tunapaswa kujiuliza maswali machache ili kubaini ukweli wa mtaka nia ya uongozi. Wengi wao ni viongozi wastaafu kwa maana ya muhula wao kwisha, swali tunalotakiwa kujiuliza ni jambo gani jema sana ambalo wanataka kulifanyia kazi kwa nguvu na maarifa waliyonayo?

Lakini pia si vibaya tukajiuliza, hivi haitoshi kuonesha kwamba uongozi ni kupokezana vijiti na siyo urithi na kufia madarakani? Pia ni vyema kujiuliza hatuoni labda tumepitwa na wakati kifikra na kwamba tunahitaji damu changa katika kukabiliana na changamoto mpya za kimaendeleo? Hapa msamiati wa kung’atuka una maana sana hata kama tumejikita katika uhalali wa kutumia demokrasia yetu.

Nijuavyo mimi tangu zamani, enzi zile za uchaguzi wa jembe na nyumba, kila mgombea alikuwa na muda wake wa uongozi na tulikuwa tukimpima kutokana na uwezo na utendaji wake kwa kipindi ambacho amekaa madarakani. 

Iwapo hukuweza kutekeleza majukumu yake tulikuwa tunamkataa kugombea kipindi kingine, lakini pamoja na yote hayo hakuna aliyehama chama au kususa chama labda kutokana na kutokuwapo kwa vyama vingine vya siasa kwa mfumo wetu wa chama kimoja.

Hali ninayoiona sasa hivi katika huu mchakato naona kama inapingana na demokrasia ya kukataliwa katika kura ya maoni, wapo ambao wanadhani wao walibatizwa kuwa viongozi wa kudumu, na pia ni kama wanakinzana na dhana ya kubadilishana vijiti katika uongozi, wanaona wao ndiyo wanaofaa na wengine hawafai. 

Ule utaratibu wetu wa kumuomba mgombea atuongoze ni kama sasa umekwisha na wagombea hawasomi alama za nyakati.

Inanipa taabu sana mtu anapotafuta uongozi wa jamii yetu kwa kutumia kaulimbiu ya vyovyote iwavyo lazima niongoze hata kama jamii unayoing’ang’ania haitaki uiongoze tena katika kipindi kijacho. Sina hakika kama ni suala la kuaminishwa kuwa wanaweza au ni suala la wapambe wachache wenye nia mbaya ya kuchumia tumbo kupitia wagombea hao.

 Uhuru wa kuamua kutokana na maslahi au matakwa binafsi ni suala muhimu lakini muhimu zaidi ni nchi siyo wao, naamini mpaka siku ya mwisho tutaona sura mpya kwa sera zilezile, na matarajio ya wapigakura ni mabadiliko ambayo hawajayapata kwa miaka mingi.

Wanataka maendeleo, wanataka serikali sikivu, wanataka huduma za jamii na kama sisi tulikuwamo katika uongozi hatukuweza kufanya hayo ni dhahiri sasa hatutaweza kufanya tena, tupishe damu mpya labda itaweza, na sisi tujifunze kutoka kwao.

 

Wasaalamu, 

Mzee Zuzu

Kipatimo.

1079 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!