Tangu zamani umekuwapo usemi kuwa: “Hayawi, hayawi, yamekuwa!” Ni usemi maarufu unaonesha msisimko wa watu pale tukio au mgeni waliyemsubiri kwa muda mrefu hatimaye anawasili. Mara tu anapowasili, wangojeaji wale kwa pamoja wanafurahi, wanashukuru na ndipo usemi huo wa “hayawi hayawi sasa yametimia” hutumika. 

Ndugu zangu Wayao kule Masasi na Tunduru wameutungia wimbo maalum usemi huo. Baada ya kusubiri kwa muda mrefu yule wanayemtarajia au lile jambo wanalolingojea kukamilika, wananchi hapo wanalipuka kwa furaha na bashasha na ndipo wanapocheza na kuimba kilugha, wimbo wenyewe una maneno haya: “Atite Nngaika, Aiche Lelo, wanya mmwe watite ngaika, aiche lelo...na kuendelea kucheza.

Maana ya maneno haya ya Kiyao ni kuwa: Mlisema hafiki, Huyu Hapa Kafika Leo! Usemi au wimbo huo unafanana kabisa na ule usemi hapo juu “hayawi hayawi yamekuwa sasa.” Watani zangu Wamakonde (kule Pwani, Lindi, Mikindani na Mtwara) pengine wanaitwa Wamaraba na kule ng’ambo ya Mto Ruvuma- Msumbiji kabila hilo hilo wanaitwa Wamawia, nao katika tukio lililongojewa namna hii likitimia tu nao hucheza kwa furaha huku wakiimba: “Lichewe, lichewe lndila Inichumuka”, wakimaanisha hoi hoi, njia (barabara) imefunguka (road is open). Sina shaka Malendego walifika na Sindimba na Midimu yao kupokea barabarani. 

Sisi wa Kusini- mikoa ya Lindi na Mtwara, tunashukuru, na tUnafurahia sana kukamilika kwa barabara hii kuu ya Dar– Kilwa – Lindi hadi Mtwara. Na tuna kila sababu na kwa haki kabisa na kwa furaha kubwa kupokea uzinduzi wa kipande kile cha barabara ya Muhoro – Somanga kama ishara ya ukamilifu wa barabara yetu. Ndiyo maana tunakaribisha ufunguzi ule kwa mikono miwili huku tukiimba WATITE NGAIKA JIICHE LEO barabara ya Dar – Lindi – Mtwara.

Ni miaka mingi mno tumengojea kukamilika kwa barabara hii. Ni muda mrefu tumesumbuliwa na kero kubwa kwa ukosefu wa miundombinu ya uhakika kati ya mikoa ile ya Kusini na mikoa hii ya Kaskazini ya Mto Rufiji. Ndiyo sababu sasa tunaona fahari kusema ile ndoto ya Kusini kupata barabara ya uhakika ya lami sasa imekamilika (a dream come true – wasemavyo Waingereza).

Tukio la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Kikwete kwenda pale Malendego juzi juzi  Agosti 7, mwaka 2015 na kuifungua rasmi barabara hii kuu ya Dar – Kilwa – Lindi hadi Mtwara ni la kihistoria kwa sisi wa Kusini. Wananchi walikusanyika pale Malendego kushuhudia historia hii ikiandikwa. Rais Kikwete alikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa barabara hii ya kihistoria. Sasa barabara imekamilika wala siyo ndoto tena, bali ni barabara halisia. 

Naamini, ingawa sikukaribishwa kuona mambo yalikuwaje pale Malendego, lakini niliona kwenye runinga “live” tukio lote lile lilifana sana. Wananchi waliokusanyika pale walionekana kufurahishwa sana na tukio lile.

Huu sasa ni ukombozi kwa wana Kusini. Ni ukombozi mkubwa kwa maendeleo ya mikoa ya Lindi na Mtwara kupata barabara nzuri namna hii. Kuwa na miundombinu ya uhakika (proper infrastructure) sina shaka biashara itafumuka kama uyoga msituni kwenye rutuba asilia.

Itakumbukwa nadhani kuwa Agosti 2, 2003 siku Daraja la Mkapa likifunguliwa pale Rufiji. Wananchi wa mikoa yote ya Kusini tulikaribishwa kushuhudia tukio lile. Wengi wetu tulijawa matumaini ya kuwa sasa “KUCHELE” -kumepambazuka kwa mikoa ya Kusini kupata maendeleo ya haraka haraka. Kizingiti kimoja kikubwa kilikuwa uvukaji wa huo Mto Rufiji. Tukajitumainisha sana kuwa kipande cha barabara kutoka Rufiji darajani hadi Somanga kwenye lami ya Kusini (kiasi cha kilometa 60 hivi) kingekamilika baada ya muda si mrefu tangu ufunguzi wa Daraja la Mkapa. 

Kamwe hatukufikiria eti Serikali itachukua miaka 12 kukamilisha kipande kile cha kilomita 60 tu wakati lami kutoka Mingoyo – Somanga imekamilika upande wa Kusini na hii ya Barabara ya Kilwa lami kutoka Dar – darajani Rufiji tayari.

Kumbe kipande chenyewe cha kutoka Darajani Rufiji mpaka Nyamwage na hasa cha kutoka Nyamwage kuelekea Somanga kilijulikana kuwa ni sehemu “korofi” sana. Kimemtoa jasho jembamba Mheshimiwa Dk. John Magufuli, Waziri wa Ujenzi. Sisi hilo hatukulitarajia na kusema kweli halikuingia akilini mwetu. Sisi tulingojea tu watukamilishie hiyo barabara yetu, mengine hayo hayakutuhusu.

Tukasikia, Dk. Magufuli wakati anamkaribisha Rais Kikwete, akate utepe kuashiria huo uzinduzi wa barabara, akitamka maneno haya: “Kipande hiki cha barabara kilikuwa ni kero kubwa kwake, na kimekuwa na changamoto mbalimbali ikiwamo hata ya kufa mkandarasi!” 

Hapo, sisi wa Kusini tukasema, kumbe sehemu ile ilikuwa ni moto wa kuotea mbali, ndiyo maana kimechukua muda mrefu kukamilika. Basi, sisi wa Kusini kero za barabara hiyo hasa maeneo ya Muhoro – Somanga tumezijua tangu enzi zile za magari ya TITIKO!

Sasa tumetiwa moyo sana kwa ukamilifu wa barabara hii. Tumefurahi sana. Rais wetu, akionekana mwenye furaha ametuonya watu wa Kusini kwa maneno haya: “Nawaombeni wananchi, muitunze barabara hii. Imegharimu fedha nyingi sana na imechukua muda mrefu kukamilika. Itunzeni msiruhusu magari yenye uzito kupita kiasi, wala magari yabebayo mafuta (tankers) yasimwage mafuta ovyo juu ya barabara hii”. 

Na aliwaomba wananchi waishio kandokando ya barabara kutunza alama za barabarani, wasiziharibu. Haya nimeyaona kuwa maagizo muhimu na ya busara sana kwa watumiaji wote wa barabara hii. 

Sote tumeona athari za kupakia magari makubwa mizigo zaidi ya uwezo wake – tunaita “overloading”. Athari zake zinaonekana hapa Dar es Salaam katika barabara ya Kilwa kipande cha Mivinjeni-Mtoni Mtongani ilivyobonyea na kuwa na manundu. Wengine tumeona barabara kuu ya Dar es Salaam – Morogoro sehemu za Mlandizi kile kipande cha barabara kuanzia Polisi Mlandizi – Ruvu darajani na tena kipande cha barabara sehemu za Chalinze pacha na Morogoro – Segera barabara imekuwa na manundu na magari madogo yanapata tabu kupita! Wafanyabiashara waroho wa utajiri wa haraka haraka ndio wanaopakiza magari yao mizigo kupita ngama ya magari yenyewe. Tumeonywa na Rais tusiharibu hiyo barabara yetu ya Dar – Kilwa – Lindi – Mtwara. 

Hapa ningeona vizuri niwarudishe wasomaji wa Makala zangu (to refresh their minds) kwenye Makala niliyoandika katika JAMHURI mwaka jana yenye kichwa “KILIO CHA BARABARA YA DAR – LINDI” toleo No. 137 la tarehe 20 – 26 Mei, 2014 uk. 14). Mle nilieleza kwa kirefu kilio chetu sisi watu wa Kusini juu ya kuchelewa kukamilika kwa lami katika barabara ile kipande kile cha Muhoro-Somanga. Nilisema nimeona kwenye runinga abiria wengi wakiwamo watoto wamebeba vifurushi vyao kichwani wanatembea kwa miguu kwenye matope sehemu ya Muhoro. Magari kadhaa yakiwamo ya mizigo, ya abiria na madogo yamekwama katika matope na yametapakaa pande zote mbili za barabara. Maji yameonekana kutuama katika lambo (swamp) eneo kubwa tu la barabara wala hapakuonekana alama mahali barabara ilipopita. 

Niliendelea kuandika kuwa kero ya barabara hii sehemu za Muhoro – Somanga ni janga la kujitakia lililotengenezwa na wanadamu (a man-made disaster) wala halikuwa lambo la asilia sehemu zile (not a natural geographical phenomenon).

Mwishoni mwa maelezo yangu katika makala ile niliuliza wahusika wa barabara imekuwaje Serikali kushindwa kukamilisha zile kilometa 14 tu katika barabara yote ile ya Dar – Lindi – Mtwara yenye urefu kilometa zaidi ya 500? Kweli Serikali iliyomla ng’ombe mzima sasa inashindwa kuutafuna mkia kale ka-kipande ka kilometa hizo 14 kwa zaidi ya miaka 10 tangu kukamilika kwa Daraja la Mkapa? Ndipo kwa masikitiko na maombolezo sana (lamentably) nikamuomba Mheshimiwa Magufuli- Waziri wa Ujenzi aliyehitimu mafunzo ya JKT Makutupora kwenye uchimbaji wa mitaro ya zabibu, atuondolee kero ile ya mahali pale Muhoro – Somanga. 

Sasa nimegundua kuwa kumbe hata yule mtaalamu mkuu wa barabara (National Tanroads Boss) ni mhitimu wa JKT Makutupora- Operation Mapambano. Hapo nikapata faraja ya kumwambia naye, we serviceman, hebu pambana na kipande kile cha Muhoro – Somanga ukamilishe lami bwana kutuondolea kero hii! 

Leo hii nilipoona mwenye runinga barabara ile imekamilika na Rais Kikwete anazindua nimepagawa kwa furaha na moyo wa shukrani kwa Serikali. Ninaona fahari kwa wahitimu hawa wa JKT Makutupora kukamilisha barabara ile. Ndipo nikajisemea kwa sauti “DEOGRATIAS” – Tushukuru Mungu!

Ualimu unayo tabia ya kukemea wanafunzi wanapoboronga masomo darasani, lakini pia anayotabia ya kuwasifu watoto wanapofaulu vizuri katika uhawilishaji (assignment) wao (blame and praise accordingly). Kwa tabia hiyo ya ualimu nimejikuta nachukua kalamu na kuandika makala hii ili niishukuru Serikali niliyoilaumu mwaka jana kwa kushindwa kumaliza kipande kile cha barabara- sasa wamemaliza kwa nini tusiwape stahili yao ya shukrani? Tuwaambie Asante kwa wahusika wote.

Basi, mimi namshukuru sana Rais Kikwete kwa kwenda Malendego kuzindua barabara hii. Ametujali sana sisi watu wa Kusini. Pale Malendego Rais alisema maneno haya juu ya Dk. Magufuli: “Kama mkakumbuka Dk. Magufuli aliahidi kuunganisha mtandao wa barabara ambao unaweza kutembea kwa gari kutoka Mtwara mpaka Mwanza, lakini sasa hata kwa bajaji unaweza kwenda” (Rais Kikwete Malendego tarehe 07/08/2015, katika Mzalendo toleo No. 2306 la Jumapili tarehe 09 – 15 Agosti, 2015 uk. 3 chini ya kichwa cha habari: Magufuli ni wa kauli na vitendo). Haya maneno ya Rais yanatosha kuelezea uchapakazi wa Dk. Magufuli. Yeye ni kauli na vitendo, basi! 

Aidha, naye Dk. Magufuli wakati akimkaribisha Rais Kikwete kukata utepe kuashiria uzinduzi wa hiyo barabara hapo Malendego alikiri kwa kutamka hivi: “Kipande hiki cha barabara kilikuwa kero kubwa, lakini kukamilika kwake kutanyanyua uchumi wa mikoa ya Kusini (soma Mzalendo huyo huyo uk. huo wa 3).

Ikumbukwe hapa kuwa enzi zile za ukoloni kule Kusini kuliitwa “CINDERELLA PROVINCE”, yaani jimbo duni. Uduni ule ulitokana na kuwa na miundombinu mibovu, elimu duni hasa pale Kilwa, Lindi, na Mikindani na uchumi haukuwa na tija kabisa (poor infrastructure poor educational facilities and poor economic development. Hivyo, tulionekana watu duni kweli. Sana sana tulijulikana kwa kuleta manamba mikoa ya Tanga, Morogoro na Dar es Salaam. 

Ufunguzi wa barabara hii mimi na wenzangu wenye mtazamo wa kisasa tunashangilia kwa sababu ni ukombozi wa maendeleo yetu. Kule Kusini hivi sasa Wazungu wangesema “a sleeping giant awakens”, yaani pandikizi la mtu lililolala linaamka! Kwa nini? Kusini kuna gesi asilia kibao, kuna korosho, ufuta, mbao, wanyama (vipusa), madini na kunaletwa viwanda mbalimbali. Kwa mtaji huo wa barabara ya uhakika sioni sababu tuzidi kupuuzwa eti sisi tu watu wa Cinderella! Hatustahili kabisa kuitwa hivyo. 

Kwa kuona hali hiyo ndipo Rais wa Jamhuri ya Muungano alituonya pale Malendego kwa kutuambia: “Wananchi msishawishike kwa barabara hii sasa na mkaanza kuuza ardhi yenu”. Kwa hili namshukuru sana. Kwa vile tumekuwa nyuma muda mrefu kimaendeleo, basi kwa kutaka tuharakishe tutahitaji fedha za haraka haraka. Ndugu zangu Wamakonde wakitaka kuhalalisha kitafunwa chochote kile wasema hivi: “Chinumbile Nnungu cha kumemena tu” yaani “kilichoumbwa na Mungu cha kuliwa tu”. Kwa usemi namna hii hawa jamaa wanaweza hata kusema ardhi ya Mungu kila mtu anaweza kuishi popote pale, maana kule Kusini Wamakonde wakivamia ardhi utawasikia wakisema: “Chilambo chake Nnungu pohe pohe kuikala tu” maana yake, ardhi ya Mungu we popote pale kaa tu. Mtazamo huo utahatarisha sana ardhi yetu kule Kusini. Ni mageuzi makubwa kuharakisha maendeleo ya mikoa yetu hiyo alimradi tusiuze mashamba yetu kwa wageni eti tupate pesa kwa maendeleo.

Mimi katika uzee wangu huu nikiangalia tulikotoka enzi zile za ukoloni, sisi tukisoma Tabora, basi la TITIKO kutoka Lindi kwenda Dar es Salaam likichukua siku mbili hadi tatu. Sasa kwa barabara yetu iliyofunguliwa juzi juzi mabasi ya Mtwara yanachukua saa nane tu kufika Dar es Salaam wakati yale ya kutoka Lindi yanachukua saa sita hivi. Hayo peke yake ni maendeleo kwa Kusini. 

Tuone tokeo hili la kihistoria ni kichocheo cha maendeleo ya haraka kule Kusini. Tuwe tayari kwa changamoto mbalimbali za maendeleo sasa. Serikali imeshafanya wajibu wake nasi tufanye wajibu wetu – KUTUNZA, KULINDA, na KUTUMIA vizuri barabara hii.

Ile ndoto ya barabara ya lami kutoka Dar – Kilwa – Lindi hadi Mtwara sasa ni halisia. Tujivunie hilo. Si ndoto tena, bali ni reality – ni halisia. 

Mkereketwa wa Maendeleo ya Kusini.

 

Mwandishi wa Makala hii, Francis Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.

1870 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!