Ernest-ManguWiki iliyopita, kwa ufupi sana nilieleza kwamba mtaji mkubwa wa ushindi wa kishindo kwa vyama tawala katika baadhi ya mataifa yasiyotaka demokrasia ya kweli ni rushwa, ujinga na umaskini wa wananchi.

Nilieleza pia mtaji mwingine wa watawala hao waliojihakikishia kwamba watawatawala wananchi milele kama watakavyo, ni ubabe wa kutumia vyombo vya dola pengine kuwatia hofu wananchi wanaoona ukombozi wao ni kubadilisha mifumo ya utawala.

Katika makala hiyo, niliielezea Serikali ya CCM kwamba inatia aibu kwa kukithiri kwa rushwa ndani ya Serikali yake na ndani ya chama, hasa kila tunapoelekea katika uchaguzi iwe mkuu au wa serikali za mitaa.

Sikukitolea mfano chama kingine cha siasa zaidi ya CCM kama chama kilichopaswa kuonesha mfano mzuri kwa vyama vingine, ambavyo vina muda mfupi wa kuwako nchini tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992 ikilinganishwa na chama hicho kikongwe.

Baadhi ya wasomaji wetu walinitumia ujumbe mfupi wa maandishi (sms) wakiniunga mkono kwa kile nilichokuwa nimekielezea na wengine wakinipigia simu wakieleza kwamba sasa wamefunguka na kwamba katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, hawatakubali kufanya makosa kwani nia yao ni kutaka mabadiliko.

Pia namshukuru msomaji mmoja aliyenitumia sms katika simu yangu ya kiganjani akinituhumu kuwa nimehongwa na mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) / Ukawa, Edward Lowassa, kwa sababu nimekitaja chama chake (CCM) kuwa kimekithiri kwa rushwa ambayo ni sehemu ya mtaji wake wa kununua madaraka kutoka kwa wananchi wanaozongwa na umaskini na kutojitambua, na kwamba itaanguka mwaka huu. Namshukuru sana.

Huyu nilimhesabu kuwa miongoni mwa watu wasiojitambua na kwamba bila shaka anaweza kuwa miongoni mwa Watanzania wanaofikiri kwamba hakuna maisha ndani ya Tanzania na CCM kama mtu hatapokea wala kutoa rushwa!

Hawa tuwaache na sasa twende kuangalia hili la leo kuwa hofu kubwa imewakumba watawala wetu ambao utawala wao umefitinika, hawana hoja tena zaidi ya kutumia mabavu kwa kuthubutu kuwatisha wananchi ili wasifikie lengo lao la kuhitaji mabadiliko ya mfumo.

Mfumo (system) unahusu watu wenyewe ama utawala mzima ukianzia ngazi ya rais hadi mjumbe wa mtaa, ukionesha uimara au udhaifu wa serikali yoyote duniani kutokana na utaratibu unaotumika katika kuwatawala wananchi wake.

Serikali dhaifu mara nyingi hukosa nguvu ya hoja kuwashawishi wananchi waikubali, na kinyume chake itatumika nguvu bila kujali kukubalika kwake au kukataliwa kwake na wananchi na hili limeanza kujitokeza hapa nchini.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, alipiga marufuku maandamano nchi nzima hadi Uchaguzi Mkuu utakapomalizika, kwa madai kuwa sababu za kiusalama zimewasukuma kufanya hivyo.

Kauli hiyo ya Jeshi la Polisi imetolewa zikiwa zimepita siku nne tu tangu mgombea wa urais wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa, kusindikizwa kwa maandamano makubwa sana na wafuasi wake kuelekea Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo ya urais.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, aliwapongeza Ukawa kwa maandamano hayo makubwa yaliyofanyika kwa amani. Pia mwingine aliyepongeza vyama vinavyounda Ukawa na CCM kwa kuwasindikiza wagombea wao wa nafasi ya urais kwa amani na utulivu bila kuwapo kwa matukio ya kihalifu, ni Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.

  Wakati hao wakipongeza kufanyika kwa maandamano hayo bila kuwapo kwa matukio ya uvunjifu wa amani, Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi yeye akawa anatoa tamko la kupiga marufuku maandamano ya vyama vya siasa kwa niaba ya bosi wake.

  Hapa nathubutu kusema kupiga marufuku maandamano ni hofu waliyonayo watawala kwamba wananchi wamewachoka kinyume na matarajio yao, sasa ni kuwanyima haki ya kuwasilisha hisia zao.

Polisi wanapaswa kuelewa kwamba nchi yoyote huru duniani ambayo wananchi wake wanaamua kubadilisha utawala (mfumo) na kukiweka madarakani chama wanachokitaka kwa njia ya kidemokrasia, hawaji na jeshi lake wala idara zake za kiusalama.

Kukubali kutumika kama kete ya kuwafanya watawala walioko madarakani waendelee kutawala watakavyo hata kama wananchi wamewachoka, ni kukoleza hasira za wananchi dhidi ya CCM. Jeshi la Polisi lisitumike kisiasa wala kuegemea upande mmoja tu, vinginevyo litakuwa ni sehemu ya wavuruga amani ya nchi.

1987 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!