Ni dhahiri kuwa sasa kila mtu anajua haki za msingi za kuweza kuishi maisha ya furaha na amani ndani ya nchi yetu bila kujali tofauti zilizopo katika dini, kabila, jinsia na hata umri. Hii ni tunu ambayo tunapaswa kuiendeleza kwa faida ya vizazi vijavyo vya watoto wa Kitanzania.

Nimeamua kuandika waraka huu siku ya leo kwa sababu nyingi sana, leo nitaainisha chache ambazo kimsingi zilianza kupata nyufa nyingi kutokana na uzembe wa watu wachache waliotaka kugeuza maadili ya Mtanzania yule aliyepaswa kuwa Mtanzania na kuwa maadili ya watu wengine wasio Watanzania.

Ulianza kuja utaratibu wa maisha tuliyozowea kuyasikia katika vyombo vya habari na siyo kutokea katika nchi yetu. Siku za hivi karibuni kulikuwa na watu wanaoamini kwamba wao ndiyo wamiliki wa nchi kwa sheria zao, walikuwa wanaweza kutoa amri kwa yeyote hata kwa mwenye mamlaka kamili ya kulinda sheria. Hii ndiyo Tanzania iliyokuwa imeanza kujengeka kwa nguvu ya fedha na siyo nguvu ya sheria halali za nchi.

Tulikuwa tukisikia mtu akijinadi kwa maneno kama ‘unanijua mimi ni nani? Nitakuweka ndani, au nenda mahali popote na kadhalika’. Hii ndiyo Tanzania iliyoanza kupotea na kwamba kuwa kiongozi katika nchi hii ni kuwa nje ya mamlaka za kisheria, kwamba unaweza ukavunja sheria bila kuulizwa.

Kulikuwa na kundi ambalo kimsingi liliishi bila kufuata kanuni na sheria za nchi yetu, walalahoi na tusio na madaraka tuliamini katika nguvu ya fedha na kwamba suluhu pekee inaweza ikapatikana kwa kutoa mlungula mahali popote na ilikuwa ikikaribia kuwa sheria kufanya hivyo.

Sasa ni furaha pande zote kujua kwamba nchi inaongozwa kwa sheria na hakuna aliyejuu ya sheria katika kutekeleza majukumu ya kila siku. Kama ni kiongozi unapaswa kufuata sheria na kama ni mwananchi wa kawaida unapaswa kufuata sheria za nchi ili sote tuishi kwa amani.

Wito wangu kwa viongozi na watu wengine ni kuhakikisha tunajiwekea misingi imara ya kuheshimu utawala wa sheria mahala popote, na viongozi wakionesha mfano ni dhahiri kuwa tunaweza kufika mahali ambapo sheria ndiyo itakayotamalaki Taifa.

Nchi ikigubikwa kwa  rushwa haki haitakuwapo, na haki ikipotea amani ni lazima itoweke na ndiyo maana wazee tunapenda amani itawale tuweze kumalizia maisha yetu kwa upendo zaidi, nchi ikiwa na amani ni dhahiri kuwa maendeleo yatapatikana na kuwafanya Watanzania wafurahie matunda ya uhuru wa nchi yao na maendeleo yaliyopatikana.

Watanzania tunapaswa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wetu hivi sasa, za kutokomeza matumizi mabaya ya madaraka na jeuri ya fedha kwa watu wachache wasiotaka turudi katika maisha ya haki ya Mtanzania, tunapaswa kuwa nyuma ya viongozi ambao wapo tayari kushirikiana na sisi katika kutokomeza adui wa utawala wa sheria.

Hii dhana ya utawala bora ilikuwa ni kama hadithi miongoni mwetu, tukiona watu wakidhulumiwa mashamba yao, mifugo, haki katika vyombo vya dola na kadhalika, sasa isiwe hadithi iwe ni jambo la msingi kwetu na tulidumishe.

Tusikubali kununuliwa na kuwapoza wanaolenga kutusaidia kupigania haki hii, baadhi yetu tutatumika na kutuaminisha kwamba kinachoendelea sasa ni udikteta, tutajengewa dhana potofu ili tuliwe ujinga na kurudi katika zama zile za fedha ndiyo kila kitu, zama za madaraka ya miungu watu.

Sasa tusimame kidete na viongozi ambao wameamua kujitoa muhanga kwa ajili yetu, ni vita ngumu tunayopaswa kushirikiana nao kikamilifu kuweza kupigana nao.

Mahali popote ambapo sheria hazifuatwi, anayeumia ni maskini na siyo tajiri, nchi yetu maskini ni wengi kuliko matajiri, kwa hiyo ni haki yetu sisi maskini kupigania maisha ya amani na upendo ili yaweze kutupa maendeleo.

 

Wasaalam

Mzee Zuzu

Kipatimo

992 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!