Kama kawaida lazima nianze na salamu, ndio uungwana ambao sisi tuliozaliwa zamani tulifundishwa bila viboko wala matusi. 

Tulifundishwa na mtu yeyote aliyekuzidi umri lakini pia tuliwasikiliza na kuwatii waliotuzidi umri kama wazazi wetu, lakini pia tulipokea adhabu kutoka kwa yeyote.

Jiulizeni kizazi chenu mmekosea wapi sasa hivi? Imefikia hatua hata kumwamini mtu inakuwa mtihani, kwa sababu ya haya mnayoita maendeleo. Leo mtoto wako ni mwanao na si mtoto wa mwingine kama ilivyokuwa zamani, inasikitisha sana.

Tumekosea pakubwa sana kiasi kwamba hatuwezi kurekebisha kwa siku chache tukaweza kufikia hata nusu ya wakati wetu, wakati ambao tulikuwa tunaweza kupiga hodi nyumba yoyote kuomba chakula au maji ya kunywa, wakati ambao ulikuwa ukisindikizwa nyumbani na mtu usiyemjua kwa lengo la kukufikisha salama.

Sina hakika kama ni Tanzania tu hali hii ndiyo ipo, lakini pia sina hakika kama waliozaliwa sasa wanawiwa na hali tuliyokuwa nayo miaka michache tu iliyopita, miaka ya neema, isiyokuwa na taarifa za kutisha au mambo yasiyokuwa ya kibinadamu, miaka ambayo watoto hatukuona kaburi wala kuhudhuria misiba.

Leo nijikite katika mambo ambayo yanaweza kuwa yanashabihiana na hiki ninachokizungumza lakini kwa upande mgumu kidogo au mambo ambayo yanachukuliwa kama vichocheo vya kuharibu maadili yetu badala ya maendeleo.

Teknolojia ni kitu kizuri sana na huenda kikawa ni kichocheo cha maendeleo bila kujua, teknolojia inakuwa kichocheo cha maendeleo hata pale maendeleo yanapokuwa hayaonekani moja kwa moja kwa macho. Najua wengi wetu dhana ya maendeleo bado haijawakaa sawa, hasa sisi wazee wa zamani.

Katika nyaraka zangu mbalimbali ambazo nimeandika huko nyuma nilijaribu kuwakumbusha sana juu ya hali ambayo wengine tuliishi na wengine hawakupata bahati ya kupitia maisha hayo, wapo waliodhani ni hadithi za kufikirika na kwa kweli ninadhani kuna haja ya kuweka katika somo la historia.

Kuweka katika historia miongo minne iliyopita itawafanya vijana wengi wa leo waelewe tulikuwa wapi na tupo wapi. 

Kiufupi ni kama tumeruka kwa kutambuka mahala pakubwa sana, ni vigumu kwa kijana wa leo kuelezwa kwamba sisi wengine tumejifunza kuhesabu kwa kutumia vijiti badala ya vidude vya soda ambavyo vilikuwa adimu sana kupatikana.

Itakuwa hadithi nzuri ya kufikirika kwa vijana wa leo kwamba karibu wote tulisoma shule umbali wa kilometa kumi na bado tulikuwa tukirudi kufanya kazi za nyumbani. 

Ni vigumu pia kuamini kwamba tulikuwa hatuna school bus kama ambavyo wao leo wanachukuliwa magetini.

Ni historia nzuri ambayo watajua kwamba sisi tulitumia vifaa vya kufundishia kutoka Shirika la Elimu Kibaha, tulipata madaftari, rula za mbao, mikebe na vitabu bure, ikiwamo na chanjo zote muhimu zilizotolewa na serikali wakati huo shuleni.

Si lengo langu kuzungumzia hayo leo, ninachotaka kuandika leo katika waraka huu ni hii adhabu ya teknolojia katika kizazi chetu. 

Leo teknolojia haitufundishi vitu vya maana kama ambavyo sisi tuliweza kujifunza bila teknolojia.

Teknolojia ni muhimu sana katika maendeleo iwapo itatumika kwa malengo hayo, inatupa fursa ya kujifunza hata tukiwa nje ya mazingira ya shule, teknolojia inatupa taarifa mapema na taarifa zilizopita kwa ajili ya marejeo.

Najua jinsi ambavyo teknolojia imekuja na kudakwa na kundi kubwa la vijana kwa mambo ya ovyo kabisa, hawana kitu cha maana cha kujifunza kwa kutumia teknolojia, bali wanatumia kuharamisha matumizi ya uhalifu.

Uvumi wa mambo kwa teknolojia ndiyo habari muhimu sana katika mitandao, namna ya uwasilishaji umeonyesha ni wajinga kiasi gani katika matumizi yake. 

Tumepokwa maadili na kutumia mitandao kama sehemu ya maisha yetu, mitandao imekuwa sehemu ya kujidhihirisha ujinga wetu.

Najua sisi ni washamba sana, kwa sababu tumetoka katika atlas na kuja katika viganja, tumetoka katika barua na kuvamia sms, tumetoka katika picha halisi na sasa tupo katika picha mjongeo, tumetoka katika redio na kuja ulimwengu wa televisheni, haya ni maendeleo lakini tujiulize yanatusaidia au yanaturudisha unyamani?

Miaka arobaini iliyopita tulikuwa mbali na teknolojia, lakini kimaadili tulikuwa wapi? Je, miaka michache ijayo tutakuwa wapi? Yangu macho na masikio.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

874 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!