Kuna wakati nafikiria kama hii Tanzania niijuayo mimi inaweza ikarejea na kuwa ile ya neema ya kula asali na maziwa, ni kama mawazo potofu ambayo kimsingi yanaweza kuwa kweli, huwa naikumbuka sana Tanzania ya kima cha chini Sh 250/- ambayo leo ni gharama ya sigareti moja.
Ni kweli kwamba siyo rahisi sana kurudi kule lakini dalili na nikinusa harufu naona kama kunarejea kwa kasi ya ajabu, nayakumbuka majaribu mengi ambayo yaliipata Serikali ile lakini mkono wa Serikali uliweza kuyadhibiti. Nani anayekumbuka maji ya Mto Kilombero kunoga sukari zaidi ya mwezi? ilikuwa ni vita ya aina yake ambayo tulishirikiana wote katika ngazi zote.
Taifa lolote linakutana na watu wanaoitwa wakubwa kwa maana ya kumiliki fedha nyingi, na wakati mwingine wakubwa hawa kwa kumiliki fedha nyingi wanawekeza katika miradi mikubwa ambayo ni kama njia kuu za kiuchumi kwa taifa, kwa kigezo hicho huwa kama vile wameshika madaraka pia ya kuongoza nchi watakavyo.
Kiuchumi uwekezaji ni jambo zuri sana kwa mustakabali ya maendeleo ya taifa, na wawekezaji ni wadau wakubwa wa maendeleo ya taifa lolote, lakini inapotokea mtu mmoja akamiliki sehemu kubwa ya uchumi wa taifa anaweza akafanya jeuri ya fedha kwa kuumiza watu wengi.

Taifa moja hapa Afrika lilimruhusu mwekezaji kumiliki leseni ya kuingiza mafuta na kuwanyima watu wengine kupata fursa hiyo ya kutoa huduma ya mafuta, matokeo yake mwagizaji alikuwa akipanga namna ambayo anahitaji faida kwa wakati huo, taifa hilo liliyumba sana kiuchumi na ni kudra za wanasiasa wenye moyo wa subira na utendaji kazi bora ndiyo uliosalimisha serikali ya nchi hiyo kushindwa kutawanyika.
Leo nimeamka na mawazo mbadala mengi, yamegonga kichwa na kuanza kujiuliza maswali ambayo labda nisingeweza kuuliza kama mambo yangelikuwa yaleyale, nimejiuliza wale wateule wachache ambao walikuwa wakihonga magari na safari za chakula cha mchana na jioni ughaibuni wako wapi.
Nimejiuliza wale ambao baadhi ya viongozi wa Serikali walikuwa wakiwasujudia na kuwaomba misaada kana kwamba wao ni serikali na walikuwa wakitoa kwa kigezo cha kuwa wageni rasmi na tukawaimbia nyimbo za kuwashukuru na kuwasifia wako wapi katika karne hii?

Nawakumbuka vijana wadogo waliofanya kufuru katika Taifa hili na wapo waliowahi kunadi kuzitandika fedha ardhini nasi tuziokote kama vile hazina thamani hii tuliyonayo leo, nawakumbuka waliotaka kutungiwa nyimbo na kuimbwa kwa masharti ya vigezo visivyozingatia sheria na kanuni za kutunza tuzo za fedha kama makaratasi yasiyo na maana.
Wapo waliokuwa wakipigiwa simu kuombwa msaada na viongozi wa Serikali na baadhi ya viongozi kutokana na dhiki zao walidharauliwa na kubezwa na kuonekana ni vibaraka katika utawala wao, haya ndiyo yanayonifanya nianze kusikia harufu ya ladha ya sukari katika Mto Kilombero.

Hii vita haikuanza leo, awamu zote ilipiganwa sana lakini nguvu ya umoja wao iliweza kushinda nguvu ya utengano wetu, ilifika mahali kwa umoja wao hao wenye nguvu ya fedha waliamua kuingia kabisa katika utumishi wa umma na vyama, kwa kipindi hicho kifupi tulishuhudia mikataba ya dhuluma na tenda kubwa zikiendelea kushikwa na wao huku tukidanganywa na kauli za umoja ni nguvu na viongozi ni mfano kwa jamii.
Nakumbuka kuna wakati, enzi zile za mwanzoni kabisa tukipata uhuru na kuandika kanuni zetu za uongozi, kwamba uongozi na biashara ni vitu viwili tofauti na tuliamua hivyo kwa nia njema kabisa tukijua kuna watu wanaweza kutumia madaraka yao vibaya na kutuingiza katika shimo la umasikini.
Tukaweka mipaka ya mtu kuwa kiongozi na tukaweka mipaka ya mtu kuwa mfanyabiashara kwa nia ya mfanyabiashara afanye biashara na asiwe kiongozi na kiongozi asimamie haki kwa niaba ya wananchi, miaka michache nahisi zile kanuni zilipotea na kitabu chake kilichomwa moto.

Tanzania ninayoijua mimi ilitawaliwa na viongozi wengi wakiwa ni wafanyabiashara, Tanzania ninayoijua mimi ilichagua viongozi wafanyabiashara, Tanzania ninayoijua mimi ilijikabidhi mikononi mwa wafanyabiashara.
Sasa kitabu kimeonekana na kanuni inasomeka, wenye nia ya biashara na wafanye biashara, wenye nia ya uongozi na wajue kuwa uongozi ni dhamana siyo mahali pa kujilimbikizia tena, vita hii haiwezi  kutuacha salama ni lazima watu wamwage sukari mitoni.

Wasaalam
Mzee Zuzu
Kipatimo.

865 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!