Home Makala Je, katiba inanyumbulika? -(2)

Je, katiba inanyumbulika? -(2)

by Jamhuri

Naam, hii ni sehemu ya pili na ya mwisho ya mjadala kuhusu kauli ya Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya pili nchini, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, aliyoitamka katika salamu za Idd el Fitr, Jumatatu, Juni 26, 2017 Jijijni Dar es Salaam.
Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1987 na kuendelea, mnong’ono wa wazo la Rais aliyekuwa madarakani aendelee, ulikumbana na mnong’ono wa pili wa kumtaka Rais awe na kikomo cha kushika madaraka. Ukweli minong’ono yote hiyo ilikuwa na mashabiki wake.

Mnong’ono wa kwanza ulishabikiwa na baadhi ya wananchi na haukuwa na kiongozi bayana, lakini ulitingisha nchi. Ule wa pili pia ulikuwa na baadhi ya mashabiki nchini na kiongozi bayana; Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na uliweka dhana ya usultani na ufalme kujengeka.
Si hivyo tu, hata dhana ya atakayekuwa madarakani asije kujiona ndiye bora na mwenye uwezo pekee wa kutawala nchi, ilhali nchi ina watu wengi wenye sifa kama hizo. Kwani kila jambo linalotendwa linatokana na ujasiri wa haki au wa dhuluma.

Minong’ono ikawa dhahiri shahiri na kuweka kampeni iliyopamba moto na kufuzu kulishawishi Bunge Maalumu la Jamhuri ya Muungano kuweka sheria na ukomo wa kushika kiti cha Rais kwa muda maalumu. Sheria hiyo ilianza kutumika katika utawala wa Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977,  ibara 42 ibara ndogo ya (2) anayoizungumzia Mzee Alhaj Ali Hassan Mwinyi inaeleza ifuatavyo,  nanukuu.
“Isipokuwa kama atajiuzulu au atafariki mapema zaidi mtu aliyechaguliwa kuwa Rais, bila kuathiri masharti yaliyo katika ibara ndogo ya (3), atashika kiti cha Rais kwa muda wa miaka mitano tangu siku aliyochaguliwa kuwa Rais,” mwisho wa kunukuu.

Mkazo wa mazungumo yetu na ushauri uliotolewa ni pale – ‘…atashika kiti cha Rais kwa muda wa miaka mitano tangu siku alipochaguliwa kuwa Rais.’ Usultani au ufalme au uwezo wa mtu (Rais) utajipambanua katika kipindi hicho au zaidi cha utawala wake na uamuzi kuchukuliwa na wananchi wenyewe.
Ukomo huo wa miaka mitano haumzuii Rais aliye madarakani kuomba na kuchaguliwa tena kuwa Rais. ‘Mazoea’ yanaturuhusu miaka 10 tu kumpa Rais madaraka hayo. Je, wananchi hatuwezi kubadili utaratibu uliopo kumpa muda zaidi Rais?

Mzee wetu Alhaj Ali Hassan Mwinyi ameshauri wala hajatoa wito. Ushauri huo uwe unakubalika au kukataliwa ni juu ya wale walioshauriwa kuujadili na kujenga hoja za kukidhi kauli hiyo. Ni busara katika hili jambo kuzama na kuibuka na jawabu kamilifu.
Katiba yoyote hunyumbulishwa na watu wanaoitumia katika kukidhi mahitaji yao ya kila siku kwa mujibu wa taratibu walizokubaliana za kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Lengo na madhumuni ni kuweka haki, usalama na umoja wao kwa manufaa ya maendeleo yao.

Je, fikira zilizotolewa kwenye mnong’ono wa pili bado unakidhi na hali halisi ya sasa ya utamaduni wetu? Au fikira zilizotolewa kwenye mnong’ono wa kwanza leo unarudishwa au unatoa mwanga zaidi kwa watu kutafakari?
Zama hubadilika na humfanya mwanadamu kubadilika katika kupambana na mazingira yanayomzunguka. Nguvu ya mabadiliko huanzishwa na binadamu mwenyewe katika matumizi bora na yakini ya fikira zake.
Binafsi nakomea hapa na kuwashauri Watanzania wenzangu katika kupima utendaji mwema wa mtu au kiongozi, tusizame katika mema tu au kasoro tu. Tuangalie na wakati uliopita na uliopo – upi una maslahi na salama kwetu. Maendeleo yetu yataletwa na kujengwa na sisi Watanzania wenyewe.

You may also like