Mfahamu mchoraji asiye na mikono

Ni siku ya Jumamosi, saa tano asubuhi, ninaikamilisha safari yangu kwenda nyumbani kwa Abdul Urio, mlemavu ambaye ameweza kupambana na changamoto za maisha bila kukata tamaa, huku akichukia vitendo vya kuomba.
Ili kufika kwake, ilinilazimu kutoka nyumbani kwangu Kimara Mwisho, na kuelekea Mbezi kwa Musuguri, hapo nikapanda Bajaji kuelekea Msingwa, mtaa wa Singida, mtaa ambao Urio ni maarufu sana, kutokana na nidhamu ya kazi ambayo amejiwekea.
“Unakwenda kwa Urio? Yule jamaa ni mtata sana…huwa hapendi mabishano, kwani wewe ni ndugu yake? Kuwa makini kaka, tena nisingependa kukufikisha pale…” ananiambia kijana dereva wa Bajaji ambaye hakutaka nitaje jina lake gazetini.
Baada ya kufika nyumbani kwa Urio, napokewa na binti aliyejitambulisha kama Susan Urio, ambaye ni mke wa mwenyeji wangu. Pale nikajitambulisha kwake, bila kuchelewa nikamweleza azma yangu ya kuwatembelea katika makazi yao.
Mke wake alinieleza nisubiri kidogo maana alikuwa bado amepumzika, dakika chache baadaye Urio akaja akiwa katika baiskeli yake maalum (wheelchair). Mazungumzo yetu yakaendelea, huku akinieleza changamoto kadhaa za maisha.

Safu hii imeanzishwa ili kuwapa fursa wananchi kuelezea historia zao za maisha, changamoto na mafanikio waliyoyapata katika kipindi chote cha maisha yao. Kwa kuanza, safu hii ambayo itaendelea kila toleo la gazeti hili, leo inaanza kwa kuangaza maisha ya Urio ambaye ni mlemavu.
Urio ambaye amezaliwa miaka 27 iliyopita, mkoani Arusha, pamoja na ulemavu aliozaliwa nao huwezi kumtofautisha na watu wengi ambao wana viungo vyote vya mwili kutokana na jinsi anavyojishughulisha kutafuta riziki na kujiepusha kuwa katika kundi la ombaomba.

Aongea siku moja baada ya kuzaliwa
Kinachomtofautisha Urio na watu wengine ni tukio la kushangaza ambalo pengine ukielezwa unaweza kuhisi ni uongo. Tukio lenyewe ni kwa Urio kuongea siku moja tu baada ya kuzaliwa kutoka tumboni mwa mama yake aitwaye Magdalena Efata Nanyaro.
Amesema, alivyozaliwa tu aliongea siku hiyo hiyo na kuleta mshangao mkubwa kwa wazazi wake pamoja na ndugu, jamaa na majirani ambao hawakuamini kilichotokea kwa mtoto mchanga kuzaliwa na kuongea.
“Niliongea siku hiyo baada ya kuzaliwa tu na kuomba aitwe mjumbe wa nyumba kumi ili niweze kuongea naye, alivyoitwa niliongea naye na nilimuuliza kama anawaongoza vizuri watu wake,” anakumbuka Urio, alivyokuwa akisimuliwa na wazazi wake.

Amesema, baada ya kuzaliwa, mama yake alipoteza fahamu kwa muda wa siku mbili na kuzua hofu kwa ndugu na ilibidi akimbizwe katika Hospitali ya Mount Meru iliyopo Jijini Arusha kwa matibabu zaidi.
“Wakati mama yangu yupo hospitalini amelazwa, sikuweza kunyonya badala yake nilikuwa napewa maziwa ya kopo ambayo ni maalumu kwa watoto,” amesema Urio.
Ili kujiridhisha na habari hizi, chanzo cha habari hii kilimtafuta mama yake mzazi ili athibitishe ukweli huo lakini hakupatikana kwa wakati kwa sababu anaishi kijijini ambako mtandao ni tatizo.

Anavyochora ramani za nyumba
Licha ya ulemavu wake, Urio anao uwezo wa ajabu wa kuchora ramani za nyumba za aina mbalimbali tena kwa kutumia kalamu ya wino na rula japo kazi hiyo hajasomea lakini amekuwa na kipaji hicho tangu alipozaliwa.
Anachoraje ramani za nyumba huku hana mikono? Ni swali unaloweza kujiuliza ikiwa hujapata bahati ya kukutana naye au kumuona mlemavu huyo.
Akisimulia jinsi anavyochora ramani za nyumba amesema; “Huwa nakaa chini kwenye mkeka harafu mbele yangu nawekewa meza au kiti, karatasi inawekwa juu yake na kalamu ninayochorea inakuwa bega langu la kulia na huwa naibana kwa kutumia kidevu ndipo naanza kazi ya kuchora.”

Amesema kazi ya kuchora alianza wakati akiwa darasa la tatu ambapo ramani ya kwanza aliyochora ilitumiwa na jirani yao aitwaye Baraka anayeishi mtaa wa Chai Mbunguni Shambalai, Mererani Arusha katika kujenga nyumba yake.
Urio anaeleza kuwa ramani ya nyumba anayoishi iliyopo mtaa wa Singida Mbezi kwa Musuguri jijini Dar es Salaam, ameichora mwenyewe na ameijenga kutokana na kipato anachokipata kutokana na kazi ya uchoraji.
Changamoto zinazomkabili kwenye kazi yake anasema ramani anazochora hazina soko la uhakika, anachora tu kwa sababu anachukia kuitwa ombaomba, lakini hana uhakika wa soko la kuuza ramani zake.
Urio, ambaye ana mke na anaishi na wadogo wake watatu wanaomtegemea, amesema amekata shauri la kujikita katika kufanya kazi hiyo apate fedha za kumsaidia kutunza familia yake.
“Kama unavyoona hapa, nina familia ya watu watano na wote wananitegemea mimi kupitia uchoraji huu, nisipofanya kazi hii hakuna wa kunisaidia si Serikali wala Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) kinachoweza kunisaidia,” amesema Urio.

Pamoja na kwamba hana mikono, lakini anao uwezo wa kutumia simu kwa ufasaha mithili ya mtu mwenye mikono yote miwili.
“Huwa naandika ujumbe mfupi wa maandishi, napiga na kupokea simu kama kawaida, natumia bega kushikilia simu huku meno na pua vikitumika kubofya vitufe vya simu,” amesema Urio.
Akishutumu Chama cha Walemavu
Amesema CHAWATA hakina msaada wowote kwake ambapo viongozi wa chama hicho wanakitumia kwa manufaa yao wenyewe.
Ametoa mfano kuwa kuna Bajaji zilizotolewa kama msaada kwenye kikundi chao ‘HAPA KAZI DISABLED GROUP’, ulipigwa juu kwa juu na viongozi wa chama pasipo wao kupewa taarifa yoyote ingawa hakueleza zilitolewa na nani.
Mwenyekiti wa CHAWATA, John Mrama, amesema chama hicho hakipati ruzuku kutoka serikalini kwa muda mrefu kutokana na viongozi waliokuwapo kabla yake kutofuatilia.
Lakini amehoji kwa nini Serikali isitoe ruzuku kwa chama wakati nchi inazingatia sera ya maendeleo na huduma kwa watu wenye ulemavu ya mwaka 2004? Na pia imeridhia mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu (UNCRPD) ya mwaka 2009.

Naibu Kamishna Ustawi wa Jamii Dar es Salaam, Radikila Mushi, anasema Chama cha Walemavu Tanzania hakipati ruzuku kutoka serikalini kutokana na hali ya uchumi kuwa ngumu.
Mushi amesema Serikali baada ya kuzindua Baraza la Taifa la Walemavu, fedha za ruzuku zitaanza kutolewa na Serikali kupitia baraza hilo.
Kelvin Donald, mkazi wa Buguruni ambaye ni mlemavu wa miguu anayetembelea magongo, amesema CHAWATA kilishakufa muda mrefu wala hakina msaada kwake, anasikia Serikali haitoi ruzuku na wala haelewi wafanyakazi wa chama wanalipwa na nani mishahara.

Urio ni nani?
Abdul Abiel Urio amezaliwa Mbuguni Shambalai, Mererani, Arusha mwaka 1990. Ni mtoto wa mwisho kwenye familia ya Magdalena Efata Nanyaro yenye jumla ya watoto watano (5), na kati yao wawili walifariki.
Urio amefanikiwa kusoma Shule ya Msingi Tuvaila na baada ya kumaliza darasa la saba mwaka 2007, alifaulu na kujiunga kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Makumira ambako alisoma hadi kidato cha tatu (3).
Amesema hakubahatika kufika kidato cha nne kutokana na mazingira ya shule kuwa magumu, shule haikuwa na choo maalumu kwa ajili ya walemavu kama yeye.
Huku akitaja sababu nyingine zilizomfanya asihitimu kidato cha nne ni kitendo wafadhili waliokuwa wakimsaidia kumsomesha kurudi kwao nchini Finland, hivyo akakosa msaada wa kumwendeleza kimasomo.
Baba yake Urio, Mzee Abiel Urio, alifariki wakati Urio akiwa na umri wa miaka minane, Anasema kabla ya kuja Dar es Salaam ameishi katika mikoa ya Mwanza, Bukoba na Shinyanga.
Amesema huu ni mwaka wa saba tangu ahamie jijini Dar es Salaam. Mbali na kujishughulisha na uchoraji wa ramani za nyumba, Urio pia anakipaji cha uchekeshaji pamoja na uimbaji, anasema ndoto yake kubwa ni kuigiza vichekesho na kufanya muziki.

Urio amesena anatamani sana kukutana na Rais John Magufuli, ili amuombe kuanzisha taasisi ya walemavu wenye vipaji ambayo itasaidia kuwaibua walemavu wengi wenye vipaji ikiwa ni pamoja na kusimamia na kuratibu kazi zao.
“Wapo walemavu wenzangu wengi wenye vipaji…tatizo ni fursa za kuonekana. Ikitokea nimekutana na Rais Magufuli, nitamuomba atusaidie kuanzisha taasisi ambayo itawaunganisha walemavu wote wenye vipaji na hakika tunaweza kuonesha maajabu,” amesema Urio.
Huku akiwa mwenye bashasha, Urio, ambaye wakati akizungumza na JAMHURI, pembeni yake alikuwapo mkewe ambaye alimtambulisha kwa jina la Susan Urio, ambaye sasa wamekamilisha miaka miwili ya kuishi katika kiapo cha kufa na kuzikana.
Akiongea kwa kujiamini, Urio, ambaye ni aghalabu kuchukia namna alivyoumbwa na Mwenyezi Mungu, amesema yeye si mlemavu, bali ana upungufu wa viungo vya mwili.
“Ninajua Rais Magufuli ni mtetezi wa wanyonge…ikitokea amesoma makala hii, ninaomba anisaidie namna ya kuweza kujikwamua kimaisha…maana familia yangu inanitegemea, huku kazi yangu ikiwa ni kuchora ramani za nyumba tu.
“Ujira ninaoupata katika kazi yangu ni kidogo sana, kutokana na ukweli kwamba wenye kipato cha chini ndiyo wamekuwa wanafaidi matunda ya kazi yangu, kazi inayotokana na kipaji nilichojaliwa na Mungu,” amesema Urio.
Urio anashauri walemavu wengi kabla ya kujishusha na kuwa ombaomba, wajichunguze wanaweza kumudu kufanya nini na wasiogope kujaribu kufanya ambacho wanahisi wanaweza kufanya.