Home Makala Tahadhari kuhusu anemia

Tahadhari kuhusu anemia

by Jamhuri

Kama una anemia, damu yako haiwezi kusafirisha hewa ya kutosha ya oksijeni kupeleka katika sehemu mbali mbali za mwili wako. Sababu kubwa la tatizo hili ni ukosefu wa madini ya chuma mwilini. Mwili unahitaji madini ya chuma kutengeneza ‘hemoglobin’.
Hemoglobin ni chembe chembe zilizopo kwenye seli nyekundu za damu ambazo kazi yake ni kuruhusu seli hizi nyekundu kusafirisha hewa ya oksijeni. Damu inasafirisha hewa safi ya oksijeni kutoka kwenye mapafu kupeleka sehemu mbali mbali za mwili. Damu inaposhindwa kupeleka hewa safi ya oksijeni ya kutosha katika sehemu mbali mbali za mwili, unaweza kuhisi hali ya kuchoka na hata kukosa nguvu za kawaida. Unaweza pia kupatwa na dalili kadhaa kama kushindwa kupumua vizuri, maumivu ya kichwa na kuhisi akili imechoka.

Anemia ni ugonjwa unaosababishwa na kiasi hafifu cha seli nyekundu za damu kwenye damu. Ugonjwa huu ukidumu kwa muda mrefu na kuwa mkubwa mwilini, unaweza kusababisha matatizo ya moyo, na matatizo ya ogani mbali mbali mwilini lakini pia anemia inaweza kusababisha hata kifo kama ikiwa kali sana mwilini.
Anemia inasababishwa na matatizo makuu matatu ambayo ni upungufu wa damu, uzalishwaji hafifu wa seli nyekundu za damu, na uharibifu wa seli nyekundu za damu kwenye damu.
Sababu hizi mara nyingi zinachangiwa na magonjwa mbalimbali na matatizo mengine ya kiafya. Tofauti na sababu hizi, matatizo mengine ambayo yanaweza kusababisha anemia ni kama vile kupata hedhi inayopitiliza kwa wanawake, ujauzito, vidonda vya tumbo, saratani ya utumbo mpana, matatizo mbali mbali ya  kurithi, ulaji wa vyakula ambavyo vina ukosefu wa madini ya chuma na vitamini B12,  na magonjwa yanayohusiana na damu kama vile ‘sickle cell’.
Daktari atakufanyia vipimo vya anemia kwa kutumia vipimo vya damu. Tiba itategemea na aina ya anemia uliyonayo. Pamoja na sababu hizo kuu, baadhi ya wagonjwa wa anemia pia wanapata ugonjwa huu na sababu hizi zifuatazo pia.

Upotevu wa damu kwa kiasi kikubwa
Upungufu wa damu unachangia ugonjwa wa anemia kwa kiasi kikubwa sana. Upungufu huu wa damu unaweza kuwa ni wa muda mfupi au ukawa wa muda mrefu kulingana na chanzo cha upungufu wenyewe. Kupata hedhi kupitiliza au kuvuja kwa damu kwenye njia ya mmeng’enyo wa chakula au njia ya mkojo, kunaweza kusababisha upungu wa damu.
Mgonjwa pia anaweza kupata upungufu wa damu baada ya kufanyiwa upasuaji, na hata pia saratani zinasababisha upungufu wa damu. Kama kiasi kikubwa cha damu kikipotea, mwili pia unaweza kupoteza kiasi kikubwa cha seli nyekundu za damu na kusababisha anemia.

Uzalishwaji hafifu wa seli nyekundu za damu
Matatizo yoyote ya kiafya ya kurithi na hata yale yanayopatikana baada ya kuzaliwa yanaweza kusababisha uzalishaji hafifu wa seli nyekundu za damu na hivyo kusababisha anemia. Matatizo haya ni kama vile aina ya vyakula, matatizo ya viwango vya vichocheo mwilini (abnormal hormone level), baadhi ya magonjwa sugu yanayodumu kwa muda mrefu ndani ya mwili, na ujauzito pia.

Mlo
Aina ya mlo wenye ukosefu wa madini ya chuma na vitamini B12 unaweza kuuzuia mwili kutengeneza seli nyekundu za damu kwa kiasi kinachohitajika. Mwili pia unahitaji kiasi fulani cha vitamini C ili kuzalisha seli nyekundu za damu. Pia matatizo yanayoweza kutokea kwenye mfumo wa utoaji takamwili yanaweza kusababisha mwili kushindwa kuzalisha seli nyekundu za damu za kutosha.

Vichocheo
Mwili unahitaji kichocheo cha ‘erythropoietin’ ili kuzalisha seli nyekundu za damu. Kichocheo hiki kinaenda kusisimua ule urojo unaopatikana ndani ya mifupa (bone marrows) ili kutengeneza seli nyekundu za damu. Kichocheo hiki kikiwa hafifu kinaweza kusababisha anemia.

Uwepo wa magonjwa mengine
Magonjwa ya muda mrefu kama vile ya figo na saratani, yanakuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa mwili kuzalisha seli nyekundu za damu. Hata baadhi ya tiba za saratani kama zile za mionzi zinaweza kuathiri ule urojo unaopatikana ndani ya mifupa na pia zinaweza kuharibu uwezo wa damu kusafirisha oksijeni kwenda sehemu za mwili.
Urojo unaopatikana ndani ya mifupa unapoathiriwa kwa namna yoyote ile, hauwezi tena kuzalisha seli nyekundu za damu kwa kazi ili kuzirudisha zile seli zilizoharibika au zilizokufa. Watu wenye maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi pia wanaweza kuugua anemia kutokana na maambukizi mengine au dawa wanazotumia kupunguza makali ya ukimwi.

Na Chris Peterson
Barua pepe: sonchrispeter@gmail.com
Simu: 0755-060 788

You may also like