*Masilahi binafsi ya vigogo yatajwa yaongeza bei za dizeli, petroli nchini

*Wapandisha usafirishaji kutoka Sh 110,000 hadi Sh 165,000 kwa tani

*Rais Samia ambana Waziri, Septemba ashusha usafirishaji hadi Sh 13,000 kwa tani

*EWURA yataka maelezo hasara ya Sh milioni 300 kwa taifa, yawalima barua PBPA


Na Deodatus Balile, Dar es Salaam

Bei za mafuta nchini zimepanda kwa kiwango cha kutisha katika miezi ya Julai na Agosti, 2021 kutokana na baadhi ya vigogo kupenyeza masilahi binafsi katika mfumo wa uagizaji mafuta nchini, ambapo gharama za kusafirisha mafuta zimeongezeka, JAMHURI linathibitisha.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa baadhi ya vigogo ndani ya Wizara ya Nishati, kwa nia ya kuvuna fedha wameandaa mpango wa kuzipa kazi kampuni zinazoongeza gharama ya usafirishaji wa mafuta kwa kigezo kuwa wanaziwezesha kampuni za wazawa, hali iliyopandisha bei za mafuta kwa kiwango cha kutisha.

“Kuna mambo ya ajabu katika nchi hii. Miaka yote tangu kuanzishwa kwa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) zabuni huwa zinatolewa kimataifa. Nchi zote duniani zinafanya hivyo kwa nia ya kupunguza gharama. Hapa kwetu zabuni ya Mei na Juni vigogo wameingiza mambo yao. Wamekuja na hoja kwamba wanazisaidia kampuni za wazawa nazo zishiriki biashara ya kuagiza mafuta.

“Uamuzi huu ambao unaelezwa kuwa unanufaisha mtandao mpana wa vigogo serikalini, umeleta sintofahamu. Bei za kusafirisha mafuta ya dizeli zimepanda kutoka wastani wa dola 24 (Sh 55,200) kwa tani hadi dola 47 (Sh 108,100) kwa tani katika Bandari ya Dar es Salaam. Bandari ya Tanga usafirishaji umepanda kutoka dola 48 (Sh 110,400) hadi dola 72 (Sh 165,600) kwa mwezi Agosti na inaendelea kupanda. Hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza bei za mafuta nchini kwa mtumiaji wa kawaida,” kimesema chanzo chetu kutoka serikalini.

Ongezeko hilo linamaanisha kuwa kwa mafuta ya dizeli yanayoshushwa kwenye boya namba 1,2 na 3 kwa mwezi Agosti, 2021, ambayo ni jumla ya tani 268,314, uamuzi huu umeongeza gharama ya kuingiza dizeli nchini kwa wastani wa Sh 13,415,700,000. 

“Hizi fedha zinakamuliwa kwa Watanzania kwenda kuwezesha ‘wazawa’, yaani kampuni zilizosajiliwa Tanzania,” kimesema chanzo chetu. Hata kwenye petroli na mafuta ya taa nako kumetokea madhara ya bei kwa uamuzi huu.

Kwa mwezi Julai, bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepanda kwa TZS 156/lita, TZS 142/lita na TZS 164/lita, mtawalia. Kwa mwezi Agosti, 2021 bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zitaongezeka kwa TZS 21/lita, TZS 36/lita na TZS 55/lita, mtawalia. 

Sehemu ya ongezeko hili inatajwa kuwa imetokana na utaratibu mpya wa kutumia waagizaji mafuta wa ndani ambao wanasafirisha mafuta kwa bei juu kuliko kampuni za kimataifa.

Hata hivyo, chanzo kingine kimetetea hali hii kikisema bei za kusafirisha mafuta hupanda au kushuka kutokana na upatikanaji wa meli zenyewe na ushindani wa kibiashara katika sehemu mbalimbali duniani kulingana na mahitaji ya wakati husika.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kwenye mtandao wa PBPA, uagizaji wa pamoja wa mafuta, meli ambazo zimeleta mafuta ya kutumika nchini kwa miezi ya Julai na Agosti, ndipo mchezo huu umeanzia. Hii ilitokana na zabuni zilizotangazwa Mei na Juni, ambazo kwa makusudi waliwaondoa waagizaji wa kimataifa na kuwapatia wafanyabiashara ‘wazawa’ ndio waingize mafuta nchini.

“Kwanza PBPA walipewa maelekezo ya mdomo. Inaonekana Mtendaji Mkuu akaona akitekeleza ipo siku atapandishwa kizimbani. Akawa mjanja, akawaandikia wizarani kutaka ufafanuzi ili naye awe na kumbukumbu likitokea la kutokea. Hapo ndipo mambo yalianza kuharibika,” kinasema chanzo chetu.

JAMHURI limefanikiwa kupata nakala ya barua ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard R. Masanja kwenda kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Simon yenye Kumb. Na. CAD. 290/308/01 ya Juni 11, 2021 inayowaelekeza PBPA kutenga asilimia 20 ya biashara ya mafuta yote nchini kwa ajili ya kuagizwa na wazawa.

“Yah: Ushiriki wa kampuni za wazawa zilizosajiliwa Tanzania katika zabuni za BPS [uagizaji mafuta kwa pamoja]. Rejea barua yako yenye Kumb. Na. PBPA/MOE/473/2021 ya tarehe 17 Mei, 2021 kuhusu somo tajwa.

“2. Nakubali maelezo uliyowasilisha wizarani yenye nia ya kutenga baadhi ya zabuni za BPS kushindaniwa na kampuni zilizoidhinishwa kuingiza mafuta nchini (pre-qualified suppliers) na zilizosajiliwa Tanzania.

“Kwa kuzingatia dhana ya kukuza ushiriki wa kampuni za ndani ili kuongeza ushindani katika biashara ya mafuta nchini, nashauri Wakala kutenga asilimia isiyopungua ishirini kwa kampuni zilizosajiliwa kuingiza mafuta nchini (pre-qualified suppliers) na kusajiliwa Tanzania mpaka utakapopata maelekezo mengine. Nakushukuru kwa ushirikiano wako. Mha. Leonard R. Masanja. Katibu Mkuu.”

Wakati Katibu Mkuu anatoa maelekezo haya, JAMHURI linafahamu kuwa hadi sasa hakuna kanuni iliyopitishwa kuongoza utaratibu huu na watendaji wamethibitisha hilo. Jumapili JAMHURI liliwasiliana na Katibu Mkuu Injinia Masanja kufahamu kwa nini alitoa maelekezo hayo kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa PBPA hata bila kuwapo kanuni inayoruhusu jambo hilo, akamsihi mwandishi kukutana naye ofisini kwake Dar es Salaam. Hadi tunakwenda mitamboni, JAMHURI lilikuwa halijakutana na Katibu Mkuu Masanja, lakini linaendelea kumtafuta.

Mtendaji Mkuu wa PBPA, Simon, amezungumza na JAMHURI na kusema uamuzi wa kuzipendelea kampuni za ndani umefanywa kwa nia njema ili kuwezesha kampuni za wazawa kushiriki biashara ya kuagiza mafuta nchini. “Kwa hali ilivyo, huwezi kuiachia kampuni ya wazawa ikashindana na hizi kampuni kubwa za kimataifa. Nia ya serikali ni njema kwamba kampuni hizi zipewe masharti yanayozijengea uwezo ili nazo zikue ziweze kushindana,” amesema.

Alipoulizwa wametumia kanuni ipi kutoa zabuni kwa kampuni zinazoitwa za ‘wazawa’ wakati hakuna kanuni, akasema: “Serikali imeunda timu na inayapitia yote hayo. Timu ipo inafanya kazi na itakuja na majibu ya maswali yote hayo unayouliza.”

JAMHURI linafahamu timu iliyoundwa kuchunguza kadhia hii inatokana na maofisa kutoka Wizara ya Fedha, EWURA, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Nishati na vyombo vingine ambavyo vinachunguza utaratibu uliotumika na taarifa kwamba kuna viongozi wanaonufaika na utaratibu huu wa kuzipa zabuni hizi kampuni zinazoitwa za wazawa.

“Hizi wanaziita kampuni za wazawa, ila ni shida. Unakuta kampuni ile ile ya kimataifa inajisajili hapa hapa Tanzania. Ikiomba kama kampuni ya kimataifa, inasema itasafirisha mafuta na kuyaleta nchini kwa dola 24 (Sh 55,200). Inapopewa zabuni kama kampuni ya wazawa inataka mafuta hayo hayo ilipwe dola 47 (Sh 108,100) kuyaleta Bandari ya Dar es Salaam au dola 72 (Sh 165,600) kuyapeleka Bandari ya Tanga. Hii ni shida.

“Ukiuliza unaambiwa kampuni za wazawa zinalipa kodi tofauti na kampuni za kimataifa. Ukiangalia ni kodi ipi ya tofauti iliyolipwa, wala huioni. Lakini huko mitaani unasikia taarifa kuwa watu wanasaka fedha za uchaguzi wa mwaka 2025. Wanasema biashara ni asubuhi na jioni ni mahesabu. Kumbe wanaumiza wananchi. Bei hizi zinavyoongezwa ndivyo bei ya mafuta inapanda kwa mtumiaji wa kawaida, hii haikubaliki,” kimesema chanzo chetu kingine.

JAMHURI limefahamishwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameusoma mchezo na kuamua kutoa maagizo mazito. “Rais amewasoma pale wizarani, anafahamu mchezo wote unaoendelea na ameagiza utaratibu huu usitishwe. Haikuwezekana kwa zabuni za Julai na Agosti kwani nchi ingeingizwa katika kesi nyingi mahakamani, ila ninakuhakikishia maagizo ya Rais Samia yametekelezwa.

“Baada ya agizo la Rais Samia, utaratibu huu umesitishwa kwa mwezi Septemba, 2021 na kuendelea. PBPA wamerejea katika utaratibu wa zamani. Cha ajabu, kwa meli itakayoleta mafuta wiki ya kwanza ya Septemba, kila tani moja itasafirishwa kwa dola 6 (Sh 13,800), badala ya dola 47 (Sh 108,100) za mwezi Agosti, 2021 kwa dizeli inayoletwa nchini. Sasa tunajiuliza kwa nini Julai na Agosti tulitwishwa mzigo wote huu? Kama wanataka kusaidia wazawa si wawaondolee hizo kodi wanazosema wanalipa?” kimehoji chanzo chetu kingine.

Hata hivyo, chanzo hicho kimesema kutokana na biashara kuanza kufunguka duniani baada ya nchi nyingi watu wake kutumia chanjo za corona, kwa meli itakayoleta dizeli mwishoni mwa Sepemba, bei ya kusafirisha tani moja ya mafuta itapanda hadi dola 26 (59,800) kwa tani, viwango vinavyoshabihiana na vilivyokuwapo kati ya Januari na Juni, 2021. Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani hakupatikana kuzungumzia sakata hili.

Wakati huo huo, Mamlaka ya Nishati na Maji (EWURA) imewapelekea PBPA hati ya kuwataka watoe maelezo kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kushindwa kusimamia meli za kuingiza mafuta nchini kwa wakati, hali iliyoliingizia taifa hasara ya karibu Sh milioni 300 kwa mafuta ya mwezi Julai, 2021.

Taarifa zilizolifikia JAMHURI zinaonyesha kuwa PBPA waliamua kuzipa mkataba wa nyongeza meli za Mt. JAG Pushpa na Mt. STI Galata ambazo zilipaswa kuleta mafuta kati ya Julai 23 – 25, 2021 na Julai 19 – 21, 2021, badala yake zikabadilisha muda wa kuleta mafuta na kuwa kati ya Agosti 2 na 8, mwaka huu.

EWURA kama msimamizi wa sekta ya mafuta wakiwamo PBPA kisheria ilitakiwa kupewa taarifa iwapo meli zitachelewa na msafirishaji kwa mujibu wa kanuni alipaswa kutoa taarifa siku 30 kabla kuwa kungekuwapo ucheleweshaji, lakini hawakupewa taarifa hizo kwa wakati.

Chanzo chetu kinasema katika hati hiyo ya kutaka maelezo EWURA inataka maelezo ya kina kwa nini wasafirishaji hawa wa mafuta waliongezewa muda wa kuleta mafuta ya Julai baada ya muda wa kikanuni kupita. Mikataba miwili iliyoongezwa ni PBPA/CPP/COMBI/DAR&TANGA/07/2021 uliobadilisha uletaji mafuta kutoka kati ya Julai 23 – 25 kwenda kati ya Agosti 2 – 4, 2021.

Mkataba wa pili ulioongezwa wanaotakiwa utolewe maelezo ni PBPA/CPP/COMBI/DAR&MTWARA/07/2021, uliobadili uingizaji mafuta nchini kutoka kati ya Julai 19 – 21, hadi Julai 24 – 26, 2021 kinyume cha kifungu cha 6.1 cha mkataba walioingia uitwao Shipping and Supply Contract. PBPA wasipojibu hati hiyo yenye nguvu sawa na hukumu ya Mahakama Kuu wanaweza kufikishwa mahakamani na watendaji wanaohusika wakafungwa jela kwa mujibu wa sheria.

Inaelezwa kuwa hatari ya kuziruhusu meli kuchelewesha mafuta kuingia nchini inaweza kuleta janga la taifa kukosa mafuta, hali itakayodhoofisha uchumi wa nchi. 

JAMHURI limemtafuta Meneja Mawasiliano wa EWURA, Titus Kaguo, ambaye amesema: “Haya ni mambo tunayoyashughulikia ndani kwa ndani serikalini, nadhani ukifika wakati suala lenyewe likiiva kama kutakuwapo uhitaji wa kuliandika vyombo vya habari mtajulishwa.”

By Jamhuri