*Adaiwa kuongoza genge la madalali feki wa mahakama

*Anaswa baada ya JAMHURI kuripoti taarifa za genge hilo 

DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala limewafikisha mahakamani watu sita akiwamo ofisa wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Rajabu Kinande, kwa makosa ya wizi.

Wakisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Cassian Mshomba, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Agatha Lumata, amedai kuwa wizi huo ulifanyika Desemba 15, mwaka jana.

Amedai kuwa wizi huo ulifanyika kwenye duka la mfanyabiashara Mohamed Soli lililopo eneo la Gerezani, Kariakoo na kuiba bidhaa kadhaa zikiwamo mabo, mabo zinazomeremeta, TV mbili, kompyuta, simu mbili, ‘grilling machine’ na ving’amuzi vya DStv na Azam.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Ashura Hussein, Farida Mwinshehe, Mohamed Miraj, Msafiri Marere na Rose Joseph.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Agosti 11, mwaka huu na washitakiwa wapo nje kwa dhamana.

Ilivyokuwa

Hatua ya kufikishwa mahakamani kwa watu hao imefikiwa baada ya Gazeti la JAMHURI la Juni 22, mwaka huu kuripoti malalamiko ya wafanyabiashara wa Gerezani kuvamiwa mara kwa mara na watu wanaojiita ‘madalali wa mahakama’ na kufanya uporaji.

Katika taarifa hiyo yenye kichwa cha habari ‘‘Wasiojulikana’ wageuza Gerezani shamba la bibi’, wakazi wa eneo hilo pamoja na uongozi wa mtaa walilalamika kuwa pamoja na taarifa zao kufikishwa Kituo cha Polisi Msimbazi, hawakupata msaada wowote.

Baadaye, JAMHURI lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Deborah Magiligimba, na kuahidi kulishughulikia suala hilo.

Miezi miwili baadaye, watuhumiwa hao wakakamatwa na wiki iliyopita wamefikishwa mahakamani, kitendo kinachochukuliwa na wakazi wa Gerezani kama ‘haki kutendeka’.

Katika taarifa hiyo, mfanyabiashara Mohamed Soli aliliambia JAMHURI kuwa kwa miaka zaidi ya mitatu amekuwa akiishi kwa shaka kutokana na hofu ya kuvamiwa na watu hao.

“Wamenivamia mara mbili dukani kwangu na hata niliporipoti Kituo cha Polisi Msimbazi sikupata msaada wowote,” anasema Soli akiomba mamlaka husika kuingilia kati.

Soli ni mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi mwenye miaka mingi katika eneo la Gerezani, maarufu kwa biashara za aina hiyo jijini Dar es Salaam; duka lake likiwa kwenye makutano ya mitaa ya Gerezani na Kongo.

Anasema tukio la kwanza lilitokea Juni 4, 2019 ambapo watu hao walifika dukani kwake wakisema wamepewa amri na mahakama kumhamisha katika eneo hilo.

“Nikawaomba wanionyeshe ‘court order’ (amri ya mahakama) lakini wakakataa! Badala yake wakachukua vitu vyangu kadhaa na fedha taslimu Sh milioni 30, wakaondoka,” anasema Soli.

Anasema uvamizi huo uliandamana na uharibifu wa mali na haukufuata utaratibu wa kisheria kama vile kutoa taarifa Ofisi ya Serikali ya Mtaa.

Siku chache baadaye, Soli aliwaona mtaani watu hao na kutoa taarifa Kituo cha Polisi Msimbazi ili apate msaada wa kuwakamata na ikiwezekana kumpa ulinzi yeye na mali zake.

“Walikataa kutoa ushirikiano, hawakunisikiliza wala kupokea taarifa zangu na kuziandika kwenye RB (Report Book). Nilihangaika wiki nzima, lakini nikakwama,” anasema Soli.

Soli anasema alilazimika kupeleka malalamiko yake kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO) wakati huo, Lazaro Mambosasa, ambaye alitoa maagizo Msimbazi kumsikiliza; amri iliyotekelezwa mara moja, akafungua kesi ya jinai namba 621/2019.

Kesi hiyo hadi inamalizika, ilikwenda kwa kusuasua kutokana na maofisa upelelezi wa Kituo cha Msimbazi kushindwa kuwapeleka mahakamani mashahidi 14 kwa visingizio mbalimbali.

Anasema hata vielelezo alivyowasilisha kituoni hapo kama ‘flash’ na rekodi za kamera ya CCTV inayoonyesha tukio zima la uhalifu lilivyofanyika, havijulikani vilipo.

“Ofisi ya Upelelezi ya Msimbazi haituelezi sababu za ushahidi kutojumuishwa kwenye jalada la kesi; hakukuwa na jibu,” anasema Soli.

Hata kabla kesi hiyo haijamalizika, mwishoni mwa mwaka jana ‘madalali’ hao wa mahakama, safari hii wakiambatana na askari polisi, wakavamia tena dukani kwa Soli.

“Safari hii tafrani ilikuwa kubwa zaidi kwani walifikia hatua hadi ya kumweka chini ya ulinzi ndugu yangu mmoja, huku vijana wao wengine wakitoa vitu dukani na kuvitupa nje, barabarani,” anasema.

Kama ilivyokuwa awali, uvamizi huu wa mara ya pili dukani kwa Soli haukufuata utaratibu wa kisheria; haukushirikisha Serikali ya Mtaa wala mjumbe, badala yake ulifanyika chini ya ulinzi wa polisi.

Uvamizi huo ulisababisha upotevu wa fedha taslimu Sh milioni 15 na mali nyingine za thamani.

“Niliripoti Msimbazi, lakini pia hakukuwa na ushirikiano, wala tukio hilo halikuingizwa kwenye RB kwa wiki tatu nzima.

“Tukaenda tena kwa Mambosasa. Akatoa maagizo kama awali kwenda Msimbazi. Wakatusikiliza, tukafungua kesi nyingine Mahakama ya Ilala, Kinyerezi,” anasema. Watuhumiwa katika kesi hiyo ni walewale wa kesi ya awali.

Anasema wapelelezi wakawa wanapiga chenga kupokea ushahidi wa CCTV ambao unaonyesha tukio la aina moja likifanywa na watu walewale, eneo moja, miaka tofauti.

“Tatizo ni kwamba, matukio yote hayo ya kihalifu yalikuwa yakipewa ‘ulinzi’ wa Jeshi la Polisi,” anasema.

Kutokana na matukio hayo, sasa Soli anasema anashindwa kufanya biashara kwa amani, hivyo kuathiri urejeshaji wa mikopo aliyochukua benki.

Kesi tayari imemalizika na washitakiwa kuachiwa huru kwa kukosekana ushahidi, mali za Soli zilizoporwa dukani kwake bado zinashikiliwa Kituo cha Polisi Msimbazi.

“Hawataki kuturejeshea kwa maelezo kwamba hazikuwamo kwenye kesi,” anasema Soli.

Uvamizi umekuwa ni kawaida

Akizungumzia malalamiko ya Soli dhidi ya polisi wa Msimbazi na ‘madalali’ wa mahakama, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Gerezani, Mohamed Ibrahim, anasema:

“Matukio ya wafanyabiashara wa hapa kuvamiwa bila sisi (serikali ya mtaa) kuwa na taarifa yamekuwa ni ya kawaida. Yametokea mara nyingi hapa.

“Wavamizi ni walewale, watu wasiojulikana, lakini wakiwa chini ya ya ulinzi wa polisi,” anasema Ibrahim.

Mwenyekiti huyo anasema siku ya tukio la uvamizi kwenye dula la Soli alikuwapo ofisini kwake na alipata taarifa hizo.

“Nilikwenda karibu na eneo la tukio kwa lengo la kutoa msaada, hasa kuwahoji wavamizi kujua ni nini hasa wanachohitaji, nilishindwa, kwa kuwa walikuwapo mabaunsa na askari polisi wakilinda eneo hilo.

“Niseme tu kwamba, walau nina taarifa za wananchi wangu watatu kunyanyaswa na kudhulumiwa mali zao na watu hao. Sasa kama kweli ni madalali wa mahakama, kwa nini hawafuati taratibu zilizopo?” anahoji Ibrahim.

Anaonyesha hofu yake kwamba iwapo mamlaka za ulinzi na usalama hazitaingilia kati, huenda kuna siku wananchi watachoka na kuamua kujichukulia sheria mkononi.

“Hapa mtaani nina watu zaidi ya 6,000. Hawa wakiamua kupambana na madalali hao na askari wanaowalinda itakuwa hatari sana,” anasema.

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa majirani wanaoishi karibu na duka la Soli, Alafa Useja, anasema alishuhudia matukio yote hayo yakiongozwa na mwanamke mmoja aliyekuwa akitoa maelekezo ya nini kifanyike.

“Baada ya dada yule kutoa amri, watu alioongozana nao wakaanza kutoa vitu vyote dukani huku wauzaji wakibaki wamepigwa butwaa.

“Kilichofanya watu wasiingilie kati, ni kuwapo kwa ‘Defender’ la Polisi likiimarisha usalama,” anasema Alafa.

Shuhuda mwingine wa tukio la pili ni mfanyabiashara mwenzake, Valence Mosha, akisema:

“Nilikuwa nimeweka TV yangu dukani kwa Soli ili baadaye niipeleke kwa fundi. Hata hiyo pia ilibebwa, nikawaomba wanirudishie, wakakataa,” anasema Mosha.

Mosha anaiomba serikali iangalie usalama wao, kwani hofu inazidi kutokana na polisi kuhusika katika kulinda uhalifu.

RPC Ilala aahidi kuingilia kati

Akizungumzia matukio hayo ya Gerezani, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Debora Magiligimba, ameahidi kuingilia kati na kuyamaliza.

“Kitu cha kwanza huyo anayelalamika aje ofisini kwangu akiwa na vielelezo vyote muhimu pamoja na hukumu ya kesi yake.

“Siwezi kuzungumza zaidi hadi nitakapoonana naye, ninachoweza kukisema ni kwamba, haki itatendeka,” anasema Afande Debora.

546 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!