Chanjo ya corona yagombewa

*Dar es Salaam, Moshi, Arusha waomba upendeleo

*Waongoza watalii waomba ruhusa kuagiza chanjo 

*Wananchi waweka kando propaganda na kuamua ‘maisha kwanza’

Na Waandishi Wetu

Maelfu ya wananchi wamejitokeza kupata chanjo ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu, COVID-19, unaosababishwa na virusi vya corona katika wiki ya kwanza ya kampeni ya kitaifa.

Utoaji wa chanjo umeanza rasmi Agosti 3, 2021 katika mikoa yote ya Tanzania Bara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua chanjo hiyo Julai 28, mwaka huu katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Jijini Dar es Salaam, JAMHURI limeshuhudia mamia ya watu wakijitokeza katika vituo kusaka chanjo, wengine wakizuiwa kutokana na kuwa na umri mdogo ingawa walikuwa tayari kuchanjwa.

Katika kituo cha Bochi, Kimara, Margareth Mwanicheta, mkazi wa Mbezi Kibanda cha Mkaa, ameliambia JAMHURI kuwa huduma inafanyika vema.

“Nimefika hapa pamoja na mama yangu (mwenye umri wa miaka 89) saa moja asubuhi. Tukapata namba 83 na 84. Tumepata chanjo lakini tatizo ni cheti. Wanasema tufuate baada ya wiki mbili,” anasema.

Mwitikio katika kituo hicho ni mkubwa na walau chanjo zote zinazopaswa kutolewa hapo kwa mujibu wa mtoa huduma mmoja humalizika.

Katika vituo vya Hospitali za Hindu Mandal, Aga Khan na Kairuki, mamia kwa mamia ya watu yamejitokeza, wengi wakionekana kuridhishwa na utoaji huduma.

“Hatupumziki. Mwitikio ni mzuri sana na inaonyesha namna gani wananchi wamepata uelewa katika suala hili,” anasema mhudumu mmoja katika Hospitali ya Aga Khan.

Awali, ilidhaniwa kwamba watu wasingejitokeza kwa wingi kutokana na propaganda zilizojitokeza kupinga chanjo.

Ingawa serikali imekuwa ikisisitizwa kuendelea kutoa elimu zaidi kwa umma, ni wazi kuwa hamasa imekuwa ikiongezeka kutokana na watu waliochanjwa kutuma picha kwa ndugu zao wakiwa na afya njema.

“Nilihamasika sana nilipoona picha ya rafiki yangu akiwa amepata chanjo. Nikaamua kuchanja. Hakukuwa na watu wengi katika Kituo cha Afya Toa Ngoma, lakini ninaamini watu watajitokeza kadiri hamasa inavyoongezeka,” anasema Efraim John, mkazi wa Toa Ngoma, Kigamboni.

Anasema katika mwaka mmoja na nusu uliopita ameshuhudia ndugu na marafiki wake wengi wakifariki dunia kutokana na corona.

“Huwa ninakasirika sana pale mtu asiyekuwa mtaalamu anapotumia jukwaa alilonalo kupingana na wataalamu wa afya. Ni makosa. Hivi kwa nini watu wanafanya utani na corona?” anahoji John.

Kilimanjaro inahitaji zaidi

Kutoka Kilimanjaro, inaripotiwa kuwa mamia ya wananchi wa mjini Moshi wamejitokeza kwa wingi kupata chanjo ya corona, huku mgawo ulioelekezwa mkoani humo na serikali ukidaiwa kuwa mdogo kuliko mahitaji halisi.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Uhuru Mwambe, ameliambia JAMHURI kuwa manispaa hiyo imepokea chanjo 2,000 na kusambazwa katika hospitali za Mawenzi, KCMC, St. Joseph na vituo vya afya vya Pasua na Majengo.

JAMHURI limeshuhudia mwitikio mkubwa wa wananchi wakati wa uzinduzi wa utoaji chanjo uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Said Mtanda, katika Kituo cha Afya Pasua.

“Watu wamehamasika. Tunahitaji chanjo zaidi tufikie mkakati wa serikali wa kutoa chanjo kwa aslimia 85,” anasema Mwambe.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ta TPC, Dk. Timizael Sumuni, akisema mahitaji ya wakazi wa eneo lake ni makubwa kuliko idadi ya chanjo walizopata.

“Kuna waliokuwa na shaka na chanjo, lakini sasa hali imebadilika. Watu wanaihitaji sana. Wamepuuza upotoshaji uliokuwapo.

“Niseme tu kwamba hakuna familia ambayo haijapoteza mtu na hakuna taasisi ambayo haijapoteza mfanyakazi kwa corona. Hivyo ni muhimu watu wakaacha uzushi,” anasema Dk. Sumuni.

Mkazi wa Mji Mpya, Moshi, Steven Massawe, anasema taarifa kwamba chanjo si salama inapaswa kupuuzwa kwa kuwa serikali haiwezi kukubali chanjo itakayoangamiza wananchi wake.

Arusha waomba kuagiza chanjo

Miongoni mwa makundi yanayohitaji kipaumbele katika kupata chanjo ni watoa huduma katika sekta ya utalii, na Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii nchini (TATO), Wilbrod Chambulo, anasema:

“Ni faraja kubwa kwa Watanzania kuanza kupata chanjo ya corona. Hii itafufua utalii ambao umeyumba kwa kiasi fulani. TATO tunaamini kila mtoa huduma kwa watalii anapaswa kuchanjwa hata kama chanjo ni hiari.”

Chambulo anasema iwapo mgawo wa chanjo kwa Mkoa wa Arusha ni mdogo, wao wanaiomba serikali iwape kibali cha kuagiza chanjo kwa ajili ya sekta ya utalii.

“Hatuna hofu na serikali. Tunafahamu kuwa wanajua umuhimu wa utalii. Lakini si vibaya na sisi tukatoa mchango wetu kama wataturuhusu, tutashirikiana na wadau ili kuagiza chanjo na kusimamia kuhakikisha watalii wanaokuja nchini hawana hofu wanapokutana na watoa huduma,” anasema Chambulo.

Kwa ujumla hamasa ni kubwa mkoani Arusha hasa katika miji ya Arusha na Arumeru.

JMHURI limeshuhudia misururu mirefu ya watu wakisubiri kupata chanjo katika vituo vilivyopo jijijini Arusha; hasa Hospitali ya Mount Meru na Kituo cha Levolosi.

Kujitokeza kwa vijana wengi kupata chanjo kunaelezwa kusababishwa na ukweli kuwa Arusha ni mkoa wa kitalii na vijana wengi hutegemea kazi hiyo kujipatia riziki.

“Ni sisi ndio hupokea wageni viwanja vya ndege na mipakani. Hawa wanakuja hapa wakiwa wamepata chanjo, kwa hiyo ni vema na sisi tuwe tumechanjwa,” anasema Dennis Mosha, mmoja wa waongoza watalii mkazi wa Kwa Morombo, Arusha. 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha hakuwa tayari kueleza idadi ya chanjo walizopata na namna walivyozigawa.

Maaskofu Kagera wazungumza

Katika hatua nyingine, maaskofu wawili maarufu nchini, Severine Niwemugizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge/Ngara na Benson Bagonza wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, wamechanja.

Akizungumza baada ya kuchanjwa, Askofu Niwemugizi amesema amefanya hivyo baada ya kuridhishwa na taarifa za ubora wa chanjo na umuhimu wake kwa afya ya binadamu.

Kwa upande wake, Askofu Bagonza amesema: “Nimechanja nikiwa wa kwanza katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Karagwe (Nyakahanga). Sababu za kuchanja ni hizi hapa:

“Nimetafiti kwa madaktari wetu nchini, USA, Ulaya na Canada. Nimeridhika na maelezo waliyonipa.

“Vita ya kibiashara kwa kampuni kubwa ni ya muda wote kwa bidhaa zote. Wanaokuuzia fulana ya kuzuia risasi, kesho wanatengeneza risasi ya kupenya katika fulana waliyokuuzia jana.

“Chanjo ya Johnson & Johnson inazuia kupata corona kwa asilimia 66. Ikitokea ukapata corona, chanjo hii inazuia kwa asilimia 86 usiingie katika ugonjwa mkali. Na chanjo hii inazuia kifo cha corona kwa asilimia 100.

“Nimewahi kuugua corona kwenye wimbi la kwanza. Nimezika wengi. Ratiba yangu imejaa kwa wiki nzima mbele kwa ajili ya kuzika. Nimechagua kufa kesho siyo leo.”

Habari hii imeandikwa na Mwandishi Wetu (Dar es Salaam), Hyasinti Mchau (Arusha) na Charles Ndagula (Moshi).

Soma habari zaidi kuhusu chanjo ukurasa wa 12 na 13.