Wazazi wamehimizwa kuwatibu watoto wanaopata ugonjwa wa mafindofindo (tonsillitis) kuwaepusha na hatari ya kupata magonjwa ya valvu za moyo.

Hayo yamesemwa na Daktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete wakati wa kambi maaluumu ya siku nne ya upasuaji wa moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Africa la nchini Marekani.

Dkt. Salehe alisema tatizo la valvu za moyo kuziba uanza na maambukizi ya kooni yajulikanayo kama mafindofindo (tonslight), na homa za utotoni za mara kwa mara ambazo huleta maambukizi yanayoathiri koo na wadudu wake kwenda kuharibu milango ya moyo (Valvu za moyo).

Aliongeza kuwa wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapougua mafindofindo ni muhimu wakamuona daktari ili waweze kutibiwa na dawa za antibiotics kwa usahihi kusaidia kuzuia uharibufu katika milango ya moyo.

“Katika kambi hii iliyomalizika jana tumewafanya uchunguzi wagonjwa 30 ambapo kati yao wagonjwa 10 tumewafanyia upasuaji wa kuzibua valvu za moyo kwa kupitia tundu dogo”, alisema Dkt. Salehe.

Dkt. Salehe alisema wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa tundu dogo katika kambi hiyo wana magonjwa ya valvu za moyo ambapo mlango mmoja katika upande wa kushoto wa moyo unakuwa umeziba au unavujisha damu.

“Dalili za awali za ugonjwa huu ni pamoja na kukosa pumzi, kuchoka, moyo kwenda mbio, kuzimia mara kwa mara, watu wanapopata dalili hizi wafike katika Taasisi yetu kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi wa moyo kwani itawasaidia kugundua tatizo mapema na kuwaepusha kufikia hatua ya kwenda kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua”, alisema Dkt. Salehe

Kwa upande wake  Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Benjamini alisema wataalamu wa upasuaji wa kufungua kifua wa JKCI na madaktari Afrika kupitia kambi hiyo wametoa huduma kwa wagonjwa ambao mishipa yao mikubwa ya damu (Aorta) imetanuka, kupasuka au imepata vyote viwili kwa pamoja.

Dkt. Alex alisema kupitia kambi hiyo wataalamu waamepata fursa ya kuongeza ujuzi na kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo ya mishipa ya damu kutanuka na kupasuka kutibiwa nchini.

“Matibabu haya ni makubwa na yanahitaji umakini wa hali ya juu, kupitia kambi hii tumepata fursa ya kujifunza na kuongeza ujuzi”, alisema Dkt. Alex.