Na Mwandishi Maalum

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wabunge Marafiki wa Umoja wa Afrika katika Bunge la Japan, Mhe. Yamagiwa Daishiro (Mb) tarehe 21 Agosti 2025 pembezoni mwa Mkutano wa TICAD 9 jijini Yokohama.

Mheshimiwa Waziri Kombo na Mheshimiwa Yamagiwa pamoja na wabunge wa jumuiya hiyo wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Japan katika sekta za teknolojia ili kuleta mabadiliko ya kidijitali; afya; jumuiya za kimataifa kwenye ajenda zenye manufaa kwa pande zote mbili; uendelezaji rasilimali watu; utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo nchini Tanzania kwa mfumo wa ubia wa sekta za umma na binafsi.

Vilevile, walijadili umuhimu wa Japan na Tanzania kushirikiana katika usalama wa chakula hususan kwenye kuongeza uzalishaji, uhifadhi wa mazao na kutafuta masoko ya mazao ya kilimo.

Tanzania itashiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo cha Bustani yajulikanayo kama International Horticulture Expo au Green Expo ambayo yatafanyika mwaka 2027 jijini Yokohama. Maonesho hayo yatatoa fursa kwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya bustani kushirikiana katika teknolojia ya kuzalisha mazao hayo na kupata masoko ya mazao hayo kwa Japan na nchi nyingine duniani ambazo zinaendelea na maandalizi ya ushiriki wa Maonesho hayo.