Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kinatarajia kuzindua kampeni za mgombea wake wa urais, Salum Mwalimu, pamoja na mgombea mwenza wake Devotha Minja, jijini Dar es Salaam leo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari na Taarifa kwa Umma wa CHAUMMA, John Mrema, uzinduzi huo utafanyika katika Viwanja vya Kinondoni Biafra, badala ya Temeke.

Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), leo pia chama cha AAFP kitazindua kampeni zake mkoani Morogoro. Uzinduzi huo utaongozwa na mgombea urais Kunje Ngombare Mwiru, akiwa na mgombea mwenza Chumu Abdallah Juma.

Aidha, vyama vya ADC na NRA vilivyopaswa kuzindua kampeni zao tarehe 28 Agosti 2025 viliahirisha kwa sababu mbalimbali. ADC imesema inasubiri uamuzi kuhusu pingamizi dhidi ya mgombea wake, na sasa inatarajia kuzindua kampeni zake tarehe 7 Septemba 2025. Kwa upande wake, NRA ilieleza kuwa ratiba ngumu ilisababisha mgombea wake wa urais, Hassan Kisabya, kukwama njiani kuelekea Kigoma, hivyo kurejea Dar es Salaam kwa maandalizi mapya.

Kwa mujibu wa INEC, vyama vya siasa viliruhusiwa kuanza kampeni rasmi kuanzia tarehe 28 Agosti 2025. Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kilichoongoza kuzindua kampeni siku hiyo kupitia mgombea wake rais wa sasa, Samia suluhu Hassan, katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, jijini Dar es Salaam.

Jana Chama cha Kijamii (CCK) nacho kilizindua rasmi kampeni zake jijini Dar es Salaam. Mgombea wake wa urais ni David Daud Mwaijojele, mwenyekiti wa chama hicho, akiambatana na mgombea mwenza Masoud Ali Abdala, ambaye pia ni katibu mkuu wa chama hicho. Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Mtoni Kijichi.