MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema Chama kinafanya kazi kubwa ya kuleta mabadiliko ili kuwaletea maendeleo wananchi.

Aidha, amesisitiza wananchi wandelee kukiamini na kukipa nafasi Chama kiendelee kudumisha amani kwa kuwa maendeleo hayatapatikana iwapo itatoweka.

Wasira alieleza hayo alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM kutoka Jimbo la Mbeya, akiwa katika ziara ya kumwombea kura mgombea urais wa CCM Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea wa ubunge na udiwani mkoani Mbeya, jana.

Alitumia mkutano huo kumwombea kura Dk. Samia, wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

“Kazi yetu ni kuleta mabadiliko katika maisha ya watu, maendeleo ni mabadiliko katika maisha ya watu, ukitengeneza barabara unamwezesha huyu mtu aweze kufikisha bidhaa zake sokoni kwa hiyo ataongeza kilimo na uchumi wake utaongezeka kwa sababu ana mahali pakuuza.

“Ukimnyima barabara analima chakula chake cha kula na kufa, anakula ashibe angojee kifo maana hakuna maendeleo hapo,” alisema.

Alisema kuwajengea wananchi miundombinu muhimu ikiwemo ya hospitali ni kuwapunguzia safari ya kwenda kutafuta dawa maeneo ya mbali kutoka katika makazi yao.

“Tumepiga hatua lakini maendeleo hayana kikomo na wala hayamalizi matatizo yote kwa mpigo kwa sababu hata ukifanya maendeleo makubwa zaidi unaweza ukazalisha matatizo mapya.

MIAKA MINNE YA MAFANIKIO

Alieleza kuwa, katika miaka CCM i.esimamiamaendeleo makubwa katika ngazi mbalimbali ambayo yamewagusa wananchi moja kwa moja.

“Tukisema Samia mitano tena ni kwa sababu kuna kazi amefanya na ameifanya kwa uzuri na ana uzoefu wa kuifanya, ametekeleza vema miradi mikubwa iliyoachwa na mtangulizi wake likiwemo bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere.

“Amejenga lile bwawa limefikia asilimia 100, sasa tuna megawati 4000 badala ya 16,000 alizoachiwa na mtangulizi wake na sasa hakuna shida ya umeme labda matatizo ya miundombinu lakini hakuna shida ya mahitaji ya umeme,” alisema.

Kwa miaka minne na nusu serikali imejenga shule tisa mpya za msingi hapa kwenye wilaya yenu na amejenga madarasa 280 mapya tena sio mapya tu bali mapya mazuri, amejenga sekondari mpya nane katika wilaya hii katika muda wa miaka minne na nusu, amejenga madarasa ya sekondari 218 na hamkuchangishwa kwa madarasa hayo.

KUHUSU AMANI
Alisisitiza Watanzania kulinda amani kwa kuwa ndiyo nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo ya sekta zote.

Wasira alisema ukipoteza amani unapoteza maendeleo kwa sababu hata maendeleo yaliyofikiwa hayawezi kuwa na msaada kwa maisha ya watu.

“Amani ikipotea hata madaraja tuliyojenga hayana maana, hata barabara zinachimbika kwa sababu amani imetoweka kwa hiyo kqzi yetu kama chama cha Mapinduzi pamoja na kulinda u.oja wa taifa tunataka kuhakikisha amani amani inakuwepo kwa sababu ikitoweka hakuna maendeleo na haya yote mnayosema hapa hayatakuja,” alieleza.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela alisema Chama mkoani humo kimejipanga vema kuhakikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu wagombea wake wote wanapata kura za kishindo.

Mwaselela alisema wamejipanga kumtafutia kura nyingi Dk. Samia zitakazomwezesha kuibuka mshindi aendelee kuiongoza nchi kwa mafanikio.

Mgombea ubunge katika Jimbo la Mbeya Vijijini, Patali Shida, alisema iwapo ataibuka mshindi ataendelea kusimamia vema kasi ya maendeleo kuendeleza iliyofanyika katika miaka mitano iliyopita.