
Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Kibaha
Waziri wa Viwanda na Biashara na mgombea wa ubunge Jimbo la Kisarawe, Dk Selemani Jafo (CCM) amesema Watanzania watamchagua mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa ya maendeleo aliyofanya kwa miaka minne iliyopita.
Dk Jafoo amesema hayo pembezoni mwa mkutano wa mgombea urais mjini Kibaha mkoani Pwani Septemba 28,2025.
Amesema Rais Samia amefanya maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali zikiwamo elimu, afya, miundombinu.

Amesema kazi hiyo kubwa ni kielelezo cha uongozi imara na dira ya maendeleo ya kweli kwa Watanzania wote bila kujali itikadi.
Amesema kwenye diplomasia ya uchumi iliyoimarishwa na Rais Samia, mauzo ya bidhaa katika Soko la Afrika Mashariki yameongezeka hadi Dola za Marekani bilioni 1.16.
Amesema hata upande wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), mauzo yakiwa ni dola bilioni 2.9 ikiwa ni rekodi ya kipekeee.
Kuhusu kazi zake jimboni, Jafoo amesema huduma ya umeme imesambazwa kwa asilimia 100 kutoka vijiji vinne tu vya awali hadi 83 vinavyounda Jimbo hilo.

Kwa upande wa sekta ya afya amesema zahanati 27 zimejengwa, na hospitali ya Wilaya ya Kisarawe imeboreshwa kwa kiwango cha kutoa huduma za kibingwa. Amesema miaka mitano ijayo, lengo ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati.
Kuhusu barabra amesema ujenzi wa barabara za lami unaendelea ili kuboresha usafiri na usafirishaji ndani ya jimbo hilo.
Kuhusu sekta ya kilimo, Serikali inaendelea kujenga kiwanda cha kuchakata korosho pamoja na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vingine ili kuongeza thamani ya mazao na kuchochea uchumi wa eneo hilo.
Sekta ya elimu pia imepewa kipaumbele, ambapo shule za msingi na sekondari zinaendelea kujengwa kila kata ili kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.

