CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimetangaza rasmi kuanzisha kampeni maalum inayojulikana kama ‘AFCON Kitaa 2027’, inayotarajiwa kuzinduliwa rasmi Oktoba 30, 2026 jijini Dar es Salaam.

Kampeni hiyo imelenga kuhamasisha wanataaluma ya habari pamoja na wananchi wote kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika nchini mwaka 2027, ambapo Tanzania itaandaa michuano hiyo kwa ubia na nchi za Kenya na Uganda.

Akizungumza kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Mwenyekiti wa TASWA, Amir Mhando, chama hicho kimeeleza kuwa kampeni hiyo inatarajia kufikia makundi mbalimbali wakiwemo wanahabari, wanamichezo, wanasiasa, wafanyabiashara, watumishi wa umma, wajasiriamali, vijana, wanawake, na wanafunzi, lengo likiwa ni kuhakikisha Watanzania wote wanaimba wimbo mmoja kwamba AFCON 2027 ni fursa ya kitaifa.

Sambamba na uzinduzi huo, TASWA itaendesha warsha na makundi ya wanahabari ya awamu tofauti, ikiwa ni mwendelezo wa mpango wake ulioanzishwa Aprili 2026 jijini Dar es Salaam ulijulikanao kama ‘Mustakabali wa Uandishi wa Habari za Michezo’ (The Future Of Sports Journalism).

Makundi hayo yatajumuisha waandishi wa habari chipukizi, waandishi wa habari waandamizi, wachambuzi na wahariri wa habari za michezo, huku yakikutana pia na viongozi wa michezo wa sasa na wa zamani ili kutazama mwelekeo wa uandishi huo na ujio wa AFCON Kitaa 2027.

Mpango huu unajengwa juu ya mafanikio ya Aprili 24, 2026 ambapo TASWA ilianza Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Mustakabali wa Uandishi wa Habari za Michezo kwa kuendesha warsha iliyowashirikisha wanahabari chipukizi, wahariri, na waandishi magwiji wa habari, ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo masuala ya rushwa kwenye michezo iliyotolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).