Na Mwandishi Wetu, Geita
ESEH Investment kampuni inayojihusisha na uuzaji wa vifaa na utoaji wa huduma za kitaalamu katika sekta ya uchimbaji imeanza kutumia teknolojia mpya za milipuko zinazolenga kuwasaidia wachimbaji kukabiliana na changamoto za mazingira na kufikia maeneo ambayo awali yalikuwa magumu kufikika.
Teknolojia hiyo, ikiwamo matumizi ya mashine za MMU, imeelezwa kuwa inaweza kutumika katika mazingira yenye kiwango kikubwa cha maji, hivyo kuwapa wachimbaji fursa ya kutumia teknolojia inayolingana na mazingira ya eneo husika.
Afisa Masoko wa ESEH INVESTMENT, William Sisty, ameeleza hayo kwenye maonesho ya tisa ya teknolojia ya madini yanayofanyika viwanja vya Dkt Samia Suluhu Hassan manispaa ya Geita.
Sisty amesema kampuni hiyo, imekuwa ikitoa huduma tangu mwaka 2014, imeendelea kuwekeza katika teknolojia na vifaa vya kisasa ili kukidhi mahitaji ya wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa.
“Tumekuwa tukijikita katika kuwahudumia wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa, huku tukiendelea kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya uchimbaji,” amesema Sisty.
Ameeleza kuwa matumizi ya mashine na vifaa vya kisasa yanaweza kusaidia kupanua wigo wa huduma za kampuni hiyo, hususan katika maeneo yenye changamoto za kimazingira yanayohitaji teknolojia maalumu.
Ameeleza kwamba mbali na uuzaji wa vifaa, kampuni hiyo pia imepanua huduma zake kwa kutoa utaalamu wa kiufundi kwa wachimbaji ambao wana vifaa lakini hawana timu yenye utaalamu wa kufanya tathmini ya eneo na kuandaa mipango ya milipuko.
“Kampuni hutoa timu za wataalamu wa kiufundi wanaosaidia wachimbaji katika shughuli mbalimbali zinazohitaji utaalamu maalumu,” amesema Sisty.
Amebainisha kuwa hatua hiyo inalenga kuwawezesha wachimbaji kutumia vifaa walivyonavyo kwa ufanisi zaidi, huku wakizingatia mahitaji ya eneo husika na taratibu za usalama katika shughuli za uchimbaji.
“Kampuni hii imeendelea kupanua shughuli zake katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwamo Chunya, Mbeya, Arusha, Mirerani na Lugoba mkoani Pwani, pamoja na maeneo ya ukanda wa Ziwa, ikiwamo Geita,” amesema Sisty.
Sisty amesema kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia katika sekta ya uchimbaji kunatoa fursa kwa wachimbaji kutumia mbinu za kisasa kulingana na mazingira wanayofanyia shughuli zao.
Amesema kuwa kampuni hiyo itaendelea kuongeza huduma na vifaa vya kisasa ili kukidhi mahitaji ya wachimbaji katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kwa hatua hii ESEH INVESTMENTS inaendelea kujitanua katika sekta ya uchimbaji kwa kuchanganya uuzaji wa vifaa na huduma za kitaalamu, huku ikilenga kuwafikia wachimbaji wa viwango mbalimbali,” amesema.



