*Asema Arusha ipo tayari kuwa mwenyeji wa bunge la dunia

*Aeleza kukamilika kwa maandalizi ya Bunge hilo

*Balozi Anda apongeza maandalizi yaliyofanyika

*Amshukuru Rc Makalla kwa ushirikiano wake katika maandalizi ya IPU

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, amemuhakikishia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Balozi Anda Cristina Filip kuwa Mkoa wa Arusha uko tayari na maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya Mkutano wa 153 wa Bunge la Dunia (IPU) utakaofanyika Tanzania kwa mara ya kwanza kuanzia Oktoba 05 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano AICC.

Akizungumza leo Alhamisi, Oktoba 01, 2026, ofisini kwake Jijini Arusha wakati alipokutana na Balozi Anda, Mhe. Makalla akisema Mkoa umejiandaa kwa muda mrefu na umeweka usalama kuwa kipaumbele kikubwa, huku akisisitiza kuwa taasisi mbalimbali zimeendelea kushirikiana kuhakikisha mkutano huo unafanyika na kumalizika kwa mafanikio.

Kwa upande wake Balozi Anda amemshukuru Mhe. Makalla kwa mapokezi na ushirikiano unaotolewa na Mkoa wa Arusha, huku akipongeza maandalizi makubwa yaliyofanyika na kueleza kuwa mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 2,000 kutoka mabunge 183 wanachama wa IPU, wakiwemo Maspika 65 wa mabunge mbalimbali duniani.

Aidha Balozi Anda amemueleza Mhe. Makalla kuwa mkutano huo utajadili ajenda mbalimbali za kimataifa, ikiwemo uongozi wa IPU na uchaguzi wa Rais mpya wa taasisi hiyo baada ya kumalizika kwa kipindi cha miaka mitatu cha uongozi wa Dkt. Tulia Ackson, huku akieleza matumaini yake kuwa mkutano huo utafanikiwa na kuwapa washiriki fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini Tanzania.