Do you like this personality?
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabiashara wa madini, wachimbaji na wasindikaji kuanzisha mifumo ya usimamizi wa ubora, mazingira, matumizi ya nishati pamoja na usalama na afya mahali pa kazi ili kuhakikisha shughuli zao zinaendeshwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa Magharibi, Joseph Makene, amesema hayo wakati akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, ambapo shirika hilo linatoa elimu kwa wadau kuhusu viwango, ubora na usalama wa bidhaa.
Makene amesema TBS imekuwa ikishiriki maonesho hayo tangu yalipoanza Septemba 23, mwaka huu, huku ikitumia fursa hiyo kuwafikia wajasiriamali na wadau mbalimbali wa sekta ya madini na sekta nyingine.
Amesema mifumo inayosisitizwa ni pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (Quality Management System), Mfumo wa Usimamizi wa Nishati (Energy Management System), Mfumo wa Usimamizi wa Mazingira (Environmental Management System) pamoja na mfumo wa usimamizi wa afya na usalama mahali pa kazi.
“Wadau hawa wakiwa na mifumo hii, hasa mifumo inayokidhi viwango vya kimataifa, wataweza kufanya shughuli zao katika mazingira yanayozingatia viwango vya kimataifa,” amesema.
Aidha Makene amesema , TBS pia hutoa elimu kuhusu namna ya kuanzisha na kusimamia mifumo hiyo na kufanya uhakiki na utoaji wa vyeti vya mifumo ya usimamizi (Management System Certification) kwa taasisi zinazokidhi matakwa ya viwango husika.
Aidha, amewataka wafanyabiashara wenye maabara zinazotumika katika upimaji wa madini kutumia huduma za maabara ya metrology ya TBS kwa ajili ya uhakiki na urekebishaji (calibration) wa vifaa vyao ili kuhakikisha vipimo vinavyofanyika vinakuwa sahihi.
Makene pia amewataka waingizaji wa bidhaa zinazotumika katika shughuli za uchimbaji madini kuhakikisha bidhaa hizo zinakaguliwa na kuthibitishwa ubora kabla ya kuziingiza nchini.
Amesema TBS ina mawakala wa ukaguzi wa bidhaa katika nchi mbalimbali ambao hufanya ukaguzi wa bidhaa kabla hazijasafirishwa kuja Tanzania.
Katika hatua nyingine, Makene amewataka wafanyabiashara wa vipodozi katika Kanda ya Ziwa Magharibi kuhakikisha wanauza bidhaa zinazokidhi viwango na zisizo na viambata sumu.
Ametaja maeneo yanayolengwa katika ukaguzi kuwa ni pamoja na Geita, Katoro, Runzewe, Kahama, Shinyanga na Bukoba, ambapo amesema TBS itaendelea kutoa elimu na kufanya ukaguzi wa bidhaa hizo.
Amesema wafanyabiashara wanapaswa kuhakikisha vipodozi wanavyouza havina viambata vilivyopigwa marufuku, huku akiwataka kutumia taarifa zinazopatikana kupitia tovuti ya TBS kujua bidhaa ambazo haziruhusiwi.
“TBS Kanda ya Ziwa Magharibi imejipanga kufanya operesheni kubwa katika masoko ya maeneo ya Geita, Katoro, Kahama, Shinyanga na Bukoba, kuweza kuviondoa vipodozi vyote ambavyo vina viambata sumu na kuviteketeza kwa mujibu wa sheria,” amesema Makene.



