Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Viongozi wanawake wanaopata fursa ya kuteuliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi, wametajwa kuwa mfano mzuri wa uwajibikaji na kujituma katika majukumu yao, jambo linalosababisha mamlaka za uteuzi kuendelea kuwaamini katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Hayo yamethibitishwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu (MCC), Mary Chatanda, alipohojiwa kwa njia ya simu, Septemba 30, 2026, akiwa visiwani Zanzibar.
Amesema, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa juu ya uwezo wa wanawake katika masuala ya uongozi na pale anapowapa majukumu wamekuwa wakithibitisha hilo, kwa utendajikazi uliotukuka.
“Katika teuzi mbalimbali anazofanya Rais wetu, wanawake wamekuwa wakipewa nafasi na hili si suala la kuwabeba kijinsia bali ni kutokana na uwezo wao usio na shaka katika kuwatumikia wananchi,” amesema Chatanda.
Ameongeza kuwa, hata uteuzi wa hivi karibuni uliofanywa na Rais, wanawake wameendelea kuaminiwa katika nafasi za wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji wa halmashauri na makatibu tawala wa wilaya.
“Viongozi wanawake wameendelea kuaminiwa serikalini na hata kwenye Chama, nafasi za makatibu wa CCM wa mikoa, kwa kweli idadi ya wanawake imeongezeka sana, kwani rekodi zao za utendaji zimekuwa chachu za kuaminiwa kwao,” amesisitiza.
Kimsingi, nguvu ya kiuongozi ya wanawake nchini imepata chachu ya kipekee kutokana na uongozi thabiti wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambapo amekuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini na kutokana na utendajikazi wake uliotukuka, ameondoa mzatamo hasi kwa baadhi ya watu juu ya uwezo wa wanawake kiuongozi.



