𝙆𝙖𝙩𝙞𝙗𝙪 𝙈𝙠𝙪𝙪 𝘿𝙠𝙩. 𝙈𝙞𝙜𝙞𝙧𝙤 𝙖𝙬𝙖𝙥𝙤𝙠𝙚𝙖 𝙑𝙞𝙤𝙣𝙜𝙤𝙯𝙞 𝙬𝙖 𝘾𝙃𝘼𝘿𝙀𝙈𝘼 𝙣𝙖 𝘼𝘾𝙏

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro amewapokea wanachama watatu (3) ambao mmoja ni Kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na wawili wa ACT Wazalendo wote wa Mkoa wa Manyara, leo tarehe 4 Oktoba 2025.

Dkt. Migiro amewakaribisha wananchama hao katika mkutano wa kampeni wa Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. 𝗦𝗮𝗺𝗶𝗮 𝗦𝘂𝗹𝘂𝗵𝘂 𝗛𝗮𝘀𝘀𝗮𝗻, uliofanyika katika Uwanja wa Stendi ya zamani ya mabasi ya Babati, mkoani Manyara.

Wanachama hao ni aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro kwa tiketi ya ACT Wazalendo Bw. Olekai Letion Laizer, Aliyekuwa Katibu wa Ngome ya Vijana ACT Wazalendo Simanjiro Bw. Daniel Lucas Pamoja na Bw. Abubakari Abdalah, aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Babati Mjini na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kupitia chama hicho.

Wakizungumzia sababu za kuhamia CCM, wanachama hao wamesema kuwa ni kutokana na kazi kubwa ya kuleta maendeleo kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla lakini kuepukana na upinzani usio wa staha wenye kupandikiza chuki, kuhamasisha vurugu, kebehi na matusi na wenye kuweka mbele maslahi binafsi badala ya Taifa na kuwa na uzalendo.