Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Uwekezaji uliofanywa na serikali ndani na nje ya nchi umeongezeka kwa asilimia 7 hadi kufikia Sh92.29 trilioni Juni 30, 2025 kutoka Sh86.3 trilioni katika mwaka wa fedha 2023/24.

Uwekezaji huu wa serikali unahusisha mashirika ya umma 255 na kampuni 45 ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache, na taasisi za kigeni 10, ambazo kwa pamoja zinatengeneza uti wa mgongo wa mapato yasiyo ya kodi ya Tanzania.

Katika kipindi cha miaka mitano uwekezaji wa ndani umeongezeka kutoka Sh67.01 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh90.61 trilioni mwaka 2024/25, jambo linalodhihirisha utendaji bora na usimamizi ulioboreshwa katika mashirika ya umma.

Hilo limeenda sambamba na kukua kwa thamani ya uwekezaji wa serikali katika taasisi za nje ambao ulitoka Sh722.94 bilioni hadi Sh1.68 trilioni.

Takwimu hizi zinazopatikana kwenye Taarifa ya Msajili wa Hazina ya mwaka ulioishia Juni 30, 2025, zinaeleza kuwa ukuaji huo umetokana na utendaji bora wa mashirika muhimu ya umma na ufanisi katika uendeshaji wa taasisi mbalimbali.

Msajili wa Hazina, Bw Nehemiah Mchechu, alisema ongezeko hilo linaonyesha juhudi endelevu za serikali katika kuimarisha usimamizi na utawala bora wa uwekezaji wa umma.

“Ukuaji huu wa uwekezaji unaonesha maboresho katika utawala wa mashirika umma, uhusiano wake na malengo ya maendeleo ya taifa,” alisema Bw Mchechu.

Kwa mujibu wake, mashirika makubwa kadhaa yamechangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la mtaji wa serikali.

Kwa mfano Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulirekodi ongezeko la asilimia 29 katika mali halisi, kutoka Sh7.2 trilioni hadi Sh9.3 trilioni.

Kichocheo kikubwa ni uandikishaji wa wanachama wapya kutoka sekta isiyo rasmi na ujumuishaji na mifumo mingine ya serikali kama Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Sanjari na NSSF, Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ulionesha ongezeko la asilimia 13 katika mali halisi, kutoka Sh8.12 trilioni hadi Sh9.2 trilioni.

Ukuaji huu ulichochewa zaidi na kuongezeka kwa michango ya wanachama kufuatia ajira mpya na vyeo kwa watumishi wa umma.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pia iliripoti ongezeko kubwa la mali halisi lililokuwa kwa asilimia 82 kutoka Sh1.3 trilioni hadi Sh2.36 trilioni ikiwa ni matokeo ya utendaji thabiti wa kifedha na usimamizi mzuri wa akiba.

Bw Mchechu alisema ongezeko la jumla la uwekezaji wa serikali limechangiwa pia na taarifa za kifedha zilizoboreshwa ambazo sasa zinaonesha thamani halisi ya hisa na mitaji ya serikali.

“Tumeona pia ongezeko la akiba na faida zilizokusanywa katika mashirika kadhaa, sambamba na kuongezeka kwa faida katika mashirika mengi ya umma,” aliongeza.

Hata hivyo, kwa baadhi ya mashirika hasa yale yaliyoko kwenye hatua za maendeleo kama kampuni za madini yalishuhudia kupungua kwa mtaji kutokana na matumizi makubwa ya uwekezaji na kuwa na mapato madogo.

Kwa ujumla, uwekezaji wa serikali unatawaliwa zaidi na mashirika yasiyo ya kibiashara, ambayo yanabeba asilimia 72 ya uwekezaji wa Sh65.44 trilioni, ikilinganishwa na Sh25.17 trilioni (asilimia 28) zilizowekezwa katika mashirika ya kibiashara.

Mapato yasiyo ya kodi yaongezeka

Utendaji mzuri wa mashirika ya umma haukuinua tu thamani ya uwekezaji wa serikali bali pia uliongeza ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi.

Taarifa ya OMH inaonyesha kuwapo kwa ongezeko la asilimia 34 katika mapato yasiyo ya kodi kutoka Sh767 bilioni mwaka 2023/24 hadi Sh1.03 trilioni mwaka 2024/25.

Ukuaji huo ni sawa na asilimia 92 ya lengo la mwaka huku faida kubwa na nidhamu bora ya kifedha katika mashirika ya umma zikitajwa kuwa sababu za ufanisi.

Asilimia 92.01 ya makusanyo ilitokana na gawio, na michango (inayokokotolewa kama asilimia 15 ya mapato ghafi), huku kiasi kilichobaki kikitokana na marejesho ya mikopo, faida za ziada na mfumo wa TTMS (Telecommunications Traffic Monitoring System).

Hiyo ikiwa na maana kuwa ofisi ilifanikiwa kukusanya zaidi ya asilimia 50 ya lengo kwa michango, gawio na marejesho ya mikopo.

Wakati huo, marejesho ya ziada na TTMS yalifikia asilimia 44 na 37 ya malengo yao husika, mtawalia.

“Utendaji bora wa kifedha wa mashirika ya umma umeongeza mapato kwa serikali, jambo linaloimarisha dhamira yetu ya kupunguza utegemezi wa mapato ya kodi na kukuza fedha endelevu kwa miradi ya maendeleo,” alisema Msajili wa Hazina.

Bw Mchechu aliongeza kuwa serikali itaendelea kuhakikisha ukuaji endelevu wa uwekezaji wake kupitia mageuzi, ufuatiliaji wa karibu na uwajibikaji mkubwa wa mashirika ya umma.

“Ukuaji huu ni ushahidi wa maendeleo tunayoyapata katika kuhakikisha uwekezaji wa umma unaleta thamani kwa wananchi,” alisema.

“OMH itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali kuboresha utendaji, uwazi na mchango wa mashirika ya umma katika uchumi wa taifa.”

Agosti 24, 2025 Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango alipokiwa akizungumza katika uzinduzi wa Mkutano wa Wakuu wa Taasisi na Wenyeviti wa Bodi (CEOs Forum 2025) alisema mageuzi katika taasisi za umma si hiari bali ni wajibu kutokana na uwekezaji mkubwa wa serikali katika taasisi hizo.

“Utawala bora wa taasisi za umma ni ajenda kuu ya serikali ili kuhakikisha uwekezaji huu mkubwa unaleta matokeo halisi kwa taifa, taasisi hizi lazima zitoe huduma bora, zikuze ajira, na zichangie kwa kiasi kikubwa mapato ya taifa,” alinukuliwa.

Uwekezaji wa nje

Uwekezaji wa serikali katika taasisi kumi za nje ulipanda kwa kasi, kufikia Sh1.68 trilioni kufikia Juni 30, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 98 kutoka Sh846.22 bilioni mwaka uliopita.

Ukuaji huu umetokana na mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji wa fedha, akiba zilizokusanywa na faida za uendeshaji katika taasisi muhimu.