Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwepo na mwenendo wa Kimbunga “CHENGE” katika Bahari ya Hindi, Kaskazini Mashariki mwa Kisiwa cha Madagascar umbali wa takribani kilometa 2400 kutoka Mashariki mwa pwani ya Mtwara.
Kimbunga “CHENGE” kilianza kujitengeneza Mashariki mwa Bahari ya Hindi mnamo tarehe 17 Oktoba, 2025 na kiliendelea kusalia katika eneo hilo huku kikiimarika.
Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa kwa sasa inaonesha kuwa Kimbunga “CHENGE” kinatarajiwa kuelekea Magharibi zaidi mwa Bahari ya Hindi ulipo ukanda wa pwani ya nchi yetu katika kipindi cha siku nne hadi tano zijazo (kati ya tarehe 26 hadi 27 ya Mwezi Oktoba, 2025), huku kikipungua nguvu yake.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “CHENGE” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.
USHAURI: Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.
