Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Said Johari, amemsifu Waziri Mkuu mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kuwa ni kiongozi mchapakazi, mwenye bidii na uaminifu wa hali ya juu katika kulitumikia taifa.

Amesema kuteuliwa kwake kunaonyesha uthabiti wa kiuongozi katika nyadhifa zote alizowahi kushika, akithibitisha kuwa ni mtu wa kazi anayeweka mbele maslahi ya Watanzania.

Johari ameyasema hayo Alhamisi, Novemba 13, 2025, Bungeni jijini Dodoma, wakati akimnadi mteule huyo na kusoma Azimio la Bunge la Tanzania, muda mfupi kabla ya Bunge kumuidhinisha kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, kufuatia uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Ameeleza kuwa Dkt. Mwigulu si mgeni kwa Wabunge na Watanzania, akisema uwezo wake wa kujituma usiku na mchana bila malalamiko ni miongoni mwa sifa zinazomtofautisha na viongozi wengine, jambo lililowapa Wabunge imani ya kumuidhinisha kwa kura nyingi.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, uteuzi wa Dkt. Mwigulu Nchemba (miaka 50) umetangazwa rasmi bungeni jijini Dodoma na kuthibitishwa kwa kura 369 za ndiyo kati ya kura 371 zilizopigwa, ambapo kura mbili ziliharibika.

Safari ya kisiasa ya Dkt. Mwigulu ilianza kung’aa mwaka 2010 aliposhinda ubunge wa Jimbo la Iramba Magharibi (CCM), nafasi aliyoirudia tena mwaka 2015. Ndani ya chama chake, amejipatia heshima kama kiongozi mwenye msimamo thabiti, nidhamu, na uadilifu katika utumishi wa umma, akiwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, mjumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu, na Sekretarieti ya chama kwa miaka mingi.

Katika Serikali, Dkt. Mwigulu alianza kama Naibu Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kisha Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi (2015), kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (2016).

Mwaka 2021, aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, nafasi aliyoishikilia hadi uteuzi wake kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.