Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Barabara za Machinjioni na Kilimahewa zimeelezwa kutotekelezwa katika kiwango kinachokidhi mahitaji ya wananchi, hali iliyosababisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Mji Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kutoa agizo la kurudiwa upya kwa kazi hiyo mara moja.
Aidha, ametoa rai kwa viongozi wa kata na mitaa kuhakikisha fedha za miradi ya maendeleo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, bila upotevu ama uzembe.

Dkt. Shemwelekwa alitoa agizo hilo Novemba 13, 2025, wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Tangini, ikiwa ni mwendelezo wa ukaguzi anaoufanya katika kata mbalimbali za manispaa hiyo.
Alisema kuwa uchongaji wa barabara hizo zinazogharimu sh.milioni 30 kupitia mapato ya ndani haujakidhi viwango, hivyo haujatimiza dhamira ya serikali ya kupunguza kero za wananchi.
“Nimekagua mradi huu na niseme wazi sijaridhishwa na kazi iliyofanyika, Lengo la serikali ni kutatua kero za wananchi, lakini hali hii haioneshi suluhisho,
Alimuagiza mtendaji wa kata kuhakikisha barabara hizo zinachongwa upya, na kuahidi kurejea kukagua utekelezaji wake.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo ameidhinisha ujenzi wa makaravati mawili ,moja eneo la Shule ya Msingi Mamlaka na lingine kivuko cha Kwa Kwembe ili kupunguza changamoto za mifereji ya maji na kuboresha mazingira ya wananchi.
Manispaa ya Mji Kibaha imetenga jumla ya sh.milioni 420 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za mitaa, ambapo kila kata imepatiwa sh. milioni 30 ili kutatua changamoto za miundombinu katika maeneo yao.

