Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imezindua Mkakati wa Mawasiliano na Uhamasishaji wa Mwaka 2025-2030 ili kuimarisha mawasiliano, uhusiano wa kikanda na maendeleo endelevu, kwa nchi wanachama.

Hafla ya Uzinduzi wa Mkakati huo imefanyika tarehe 17 Novemba, 2025 jijini Gaborone, Botswana na kushirikisha wadau mbalimbali wa mawasiliano, habari na washirika wa kimataifa wa maendeleo.

Akizindua mkakati huo, Naibu Katibu Mtendaji wa SADC anayeshughulikia Ushirikiano wa Kikanda Bi. Angele Makombo Ntumba amesema mkakati huo utasaidia kukuza mfumo wa mawasiliano katika karne hii ya kidigitali na kuwezesha ukanda wa Afrika ya Kusini kuimarisha miundombinu, uchumi, biashara na miradi ya maendeleo ya jamii, kwa manufaa ya nchi wanachama.

Bi. Ntuma amesema Mkakati huo wa Mawasiliano uliozinduliwa katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kireno, utatekelezwa kwa pamoja na nchi wanachama wa SADC chini ya Waratibu wa Kitaifa wa SADC na Waratibu wa Kitaifa wa Habari na Mawasiliano wa jumuiya hiyo, katika nchi wanachama 16 za SADC.

Amewataka waratibu hao kushirikiana na SADC na wadau mbalimbali katika kutekeleza Mkakati huo, wakiwemo Vyombo vya Habari na Taasisi za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika nchi zao na ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Aidha, Bi. Ntumba ameishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika lake la Maendeleo la GIZ kwa kudhamini maandalizi na uzinduzi wa mkakati huo, kwani umewezesha SADC kutekeleza majukumu yake kwa upana zaidi kupitia nyenzo muhimu ya Mawasiliano na Uhamasishaji.

Naye Mkuu wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani nchini Botswana, Bi. Simone Goertz ameelezea azma ya GIZ kuendeleza ushirikiano na SADC katika utekelezaji wa Mkakati wake Mawasiliano, hatimaye kuleta maendeleo endelevu kwa manufaa ya nchi wanachama; kulingana na mabadiliko ya utandawazi yanayoendelea kutokea duniani.