📌Wakandarasi wazawa wapewa kipaumbele

📌Wakandarasi watakiwa kufanya kazi kwa weledi, ubora na kasi

📌Watakiwa kuepukana na vitendo vya rushwa

📌Wahimizwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Nchi

📍Dodoma

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imesaini mikataba 30 yenye thamani ya shilingi Trilioni 1.2 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme katika Vitongoji 9,009 utakaonufaisha Wateja wa awali 290,300 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.

Akizungumza katika hafla hiyo leo, Januari 17, 2026 Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kusaini kwa mikataba ya Mradi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ifikapo 2030 vitongoji vyote nchini viwe vimefikishiwa nishati ya umeme.

“Serikali imedhamiria kuhakikisha hakuna Mtanzania atakayebaki bila umeme. Tumekamilisha vijijini na sasa ni zamu ya vitongoji na kwa mikataba hii iliyosainiwa hivi leo ni ushahidi wa dhamira hiyo ya Serikali,” amesema Mhe. Ndejembi.

Amebainisha kuwa kati ya mikataba 30 iliyosainiwa, mikataba 21 ni ya kampuni za Wazawa na mikataba mingine tisa ni ya kampuni kutoka Nje ya nchi ambazo zimesajiliwa hapa nchini.

Serikali ya Rais Samia inatambua Sekta ya Nishati ni injini ya kuchochea maendeleo na amekuwa akitoa fedha nyingi ili kuboresha maisha ya Wananchi wa vijijini.

Ameipongeza REA kwa kuendelea kuwa chombo imara cha Serikali kwa utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya kusimamia na kupeleka nishati bora kwa Wananchi na ameendelea kuhakikisha kuwa Taasisi zote za Umma ziunganishwe na umeme zikiwemo shule za msingi, sekondari na vituo vya afya.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema Serikali itaendelea na kasi yake ya kusambaza umeme ili kuleta tija inayokusudiwa.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu amepongeza jitihada za REA katika kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha nishati ya umeme inasambaa kote nchini.

“Hongereni REA mnafanya kazi kubwa, leo hii tumefurahi kushuhudia tukio la kihistoria la kusaini mikataba ya kusambaza umeme vitongojini,” amepongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Meja Jenerali Mstaafu, Mhe. Balozi Jacob Kingu aliwasisitiza Wakandarasi kuzingatia thamani ya fedha za umma zilizotolewa kutekeleza Miradi sambamba kujifunza kutoka kwenye Miradi iliyokamilika ili kutekeleza kwa ufanisi na kwa ubora unaotakiwa.

Akizungumzia utekelezaji wa Miradi mbalimbali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amesema REA inatekeleza azma ya Serikali ya kuhakikisha umeme unawafikia Wananchi kwa vitendo.

“Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2025, Serikali imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara. Hatua hii imeleta mapinduzi ya kweli ya kiuchumi na kijamii, ikichangia kuboresha maisha ya Wananchi wanaoishi vijijini,” amefafanua.

Amesema mwaka 2021 kati ya vitongoji 64,359 vilivyopo Tanzania Bara, vitongoji 28,258 pekee vilikuwa na umeme wakati vitongoji 36,101 vilikosa huduma hiyo muhimu.

Amefafanua kuwa kupitia utekelezaji wa Miradi mbalimbali kuanzia mwaka 2021 hadi Desemba 2025, Serikali imeunganisha umeme katika vitongoji 10,745, na hivyo kuongeza idadi ya vitongoji vyenye umeme kufikia 39,003.

Aidha, amesema vitongoji 2,435 vipo katika hatua za utekelezaji wa miradi inayoendelea na hivyo kufanya jumla ya vitongoji 41,438
kuwa tayari vimeunganishwa au vipo katika utekelezaji.

“Utekelezaji wa miradi hii ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha vitongoji vyote vinasambaziwa umeme,” amefafanua.

Amesema Mradi utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na aliwasisitiza Wakandarasi kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa na tabia zisizo na maadili.

“Mradi huu utahusisha ujenzi wa kilomita 13,180 za njia za msongo wa kilovolti 33, kilomita 14,016 za njia za msongo wa volti 415,
pamoja na ujenzi wa mashineumba 9,009 na utatekelezwa kupitia mafungu 30 ambapo mafungu 21 yakitekelezwa na kampuni za ndani, na mafungu 9 na kampuni za nje zilizosajiliwa nchini,” amefafanua.

Amebainisha kwamba kwa kuzingatia gharama na idadi ya vitongoji vitakavyofikiwa, Mradi huo, ndiyo mkubwa zaidi kwa usambazaji umeme kuwahi kutekelezwa nchini.