Serikali, kupitia Wizara ya Nishati, imeitaka jamii kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo uzalishaji, usambazaji na matumizi ya teknolojia za kupikia kwa kutumia umeme, gesi, bayogesi na majiko banifu, hatua itakayosaidia kuongeza kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo jamii na taifa kwa ujumla.

Akizungumza, jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, katika hafla ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambuliwa kama Kinara wa Nishati Safi Afrika na uzinduzi wa Taasisi ya Women and Youth Future Initiative (WYFI), Mkurugenzi wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, amewahimiza wanawake na vijana kutumia fursa zilizopo katika sekta ya nishati safi ya kupikia ili kuinua uchumi wao.
Mlay amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifanya ajenda ya nishati safi ya kupikia kuwa ajenda ya kitaifa, kikanda na kimataifa kupitia uongozi wake unaohamasisha matumizi ya nishati safi kwa maendeleo endelevu.

“Chini ya uongozi wa Rais Samia, matumizi ya nishati safi ya kupikia hayatazamwi tena kama suala la jikoni pekee, bali ni ajenda inayogusa afya ya jamii, uhifadhi wa mazingira, usawa wa kijinsia, elimu, uchumi, ajira na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu,” amesema Mlay.

Amesema juhudi hizo zimeifanya Tanzania kutambulika kimataifa kama nchi yenye dhamira thabiti na mwelekeo wa wazi katika kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku ikiendelea kuwa mfano kwa mataifa mengine barani Afrika.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Raya Majallah, amesema kuwa mikakati iliyopo inalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia.

Mhandisi Majallah amesema kuwa nishati safi ya kupikia ni ile yenye ufanisi, rahisi kutumia, inayopatikana kwa urahisi, salama na yenye gharama nafuu, huku isiyomuweka mtumiaji katika mazingira hatarishi yanayoweza kuathiri afya au kuchafua mazingira.

“Nishati safi ya kupikia inalinda afya. Kila mwaka watu takribani 33,000 hufariki kutokana na magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanayosababishwa na moshi. Wanaoathirika zaidi ni wanawake, watoto na wazee. Hivyo, matumizi ya nishati safi ya kupikia yatasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” amesema Mhandisi Majallah.

Ameongeza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia husaidia kulinda mazingira, kwani ukataji wa miti kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa usababisha ukame na kuongezeka kwa joto duniani.

Aidha, amesema REA inaendelea kutekeleza jitihada mbalimbali za kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanatumia nishati safi ya kupikia na kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa.

Naye Mkurugenzi wa WYFI na Mbunge, Mhe. Asha Baraka, ameishukuru Wizara ya Nishati kwa kupitia REA kwa kutoa msaada wa mitungi 250 ya gesi ambayo itawanufaisha wananchi wa Mkoa wa Pwani.