Na Theophilida Felician, JamhuriMedia, Dodoma

Chama cha waganga watiba asili nchini TAMESOT kimekemea na kulaani vitendo vyote vinavyotumika vibaya na baadhi watu wanaotumia vibaya jina la tiba asili kwa maslahi binafsi.

Kauli hiyo imetolewa naye katibu mkuu wa chama hicho Bw Lukas Joseph Mlipu wakati akizungumza a chombo hiki akiwa makao makuu ya ofisi za TAMESOT zilizopo Kibaigwa Dodoma.

Katibu mkuu Mlipu amesema kuwa chama hicho kimeendelea kupinga vitendo hivyo ambavyo vinakwenda kinyume na maadili, uadilifu, uwajibikaji na uzalendo katika taaluma hiyo ya tiba asili.

Amefafanua kuwa wao TAMESOT wanatambua kuwa tiba asili ni mwanzo wa maisha na hivyo wao wamekuwa mstari wa mbele kulinda na kuuthamini urithi huo ambapo amesema wamejizatiti kuilinda na kuienzi kwa vitendo lengo ikiwa ni kuiheshimisha na kudumisha usalama wake.

Ameyataja baadhi ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa ili kuiboresha taaluma hiyo ni pamoja na kuzingatia maarifa, tafiti za kisayansi na kuzingatia sheria za nchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Amesisitiza kwamba katika jitihada zao wanaendelea kutoa wito kwa wanachama wote wa TAMESOT na waganga kwa ujumla Tanzania kutoa huduma ya tiba kwa kudumisha umoja, mshikamano, kuheshimiana na kuunga mkono viongozi wao,kushiriki kikamilifu elimu ya mafunzo yanayoandaliwa na chama hicho kwa kushirikiana na mamlaka za serikali, kuupuza maneno ya upotoshaji na migawanyiko, wafanye kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo kwa maendeleo ya tiba asili.

Ameongeza kuwa yote hayo yakizingatiwa itasaidia kupunguza matukio yasiyo faa yakiwemo ya wananchi kutapeliwa na watu wasio waganga harali, ramuli chonganishi na imani za kishirikina.

Hata hivyo ameishukuru serikali kupitia wizara ya afya kwa namna inavyondelea kusimamia vyema tiba asili nchini jambo ambalo linawatia moyo na matumaini makubwa katika huduma hiyo huku akiwashukuru baadhi ya watendaji wa kata na vijiji wanaounga juhudi za chama hicho katika kuwahamasisha waganga kushiriki mafunzo ya tiba asili mafunzo yanayoendelea kutolewa kwa wataalamu hao nyakati tofauti tofauti.