Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Katika jitihada za kuwaandaa vijana kukabiliana na maisha, kujitegemea na kushiriki ujenzi wa taifa, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza kuanza kwa mafunzo ya kujitolea kwa mwaka 2026, hatua inayofungua fursa kwa maelfu ya vijana waliomaliza masomo yao katika ngazi mbalimbali kwa vijana wenye umri wa miaka 16 hadi 18 .
Akizungumza Januari 20, 2026 na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Dodoma, Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, amesema mafunzo hayo hayalengi kutoa ajira bali kuwajenga vijana kiakili, kimwili na kimaadi.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwaandaa vijana waliomaliza masomo yao katika ngazi mbalimbali ili wawe na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa.

“Lengo la mafunzo haya si kutoa ajira, bali kuwaandaa vijana kukabiliana na maisha kwa kuwajengea misingi ya kujitegemea, kufanya kazi kwa nidhamu na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa,” amesema Brigedia Jenerali Mabena.
Ameeleza kuwa washiriki wa mafunzo hayo watanufaika kwa kupata elimu ya uzalendo, nidhamu ya kazi, stadi za maisha pamoja na mafunzo ya vitendo yatakayowawezesha kujisimamia baada ya kuhitimu.
Brigedia Jenerali Mabena, amesema waombaji wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania wenye umri wa kuanzia miaka 16 hadi 18, ambapo kwa Tanzania Bara wanapaswa kuwa wamehitimu elimu ya darasa la saba na kwa Zanzibar wawe wamehitimu elimu ya kidato cha pili.
” Waombaji wanatakiwa kuwa wamehitimu masomo yao kati ya mwaka 2022 hadi 2025 na wawe na vyeti halisi vya kuhitimu elimu ya msingi au kidato cha pili, “amesisitiza
Ameongeza kuwa JKT linawahimiza pia vijana wenye taaluma mbalimbali, hususan waliobobea katika fani za teknolojia ya habari na mawasiliano, kujitokeza kuomba nafasi hizo kupitia mikoa yao.
Ametaja taaluma hizo ni pamoja na Diploma in Information Technology, Diploma in Business Information System, Diploma in Information Communication Technology (ICT) pamoja na Diploma in Cyber Security and Digital Forensics.
Nyingine ni Shahada ya Sayansi ya Kompyuta (Bachelor of Science in Computer Science), Shahada ya Teknolojia ya Habari (Bachelor of Science in Information Technology), Shahada ya Uhandisi wa Kompyuta, Shahada ya Business Information Technology, Shahada ya Cyber Security and Digital Forensics pamoja na Shahada ya Computer Networks na Information Security Engineering.

“Tunawahimiza pia vijana wenye vipaji mbalimbali kujitokeza kwa wingi. Usajili wa vijana kwa mafunzo ya JKT kwa kujitolea utaanza rasmi tarehe 26 Januari 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani,” amesema.
Amefafanua kuwa vijana watakaoteuliwa kujiunga na mafunzo hayo watatakiwa kuripoti katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa kuanzia tarehe 27 Februari 2026 hadi tarehe 4 Machi 2026.
Aidha, Brigedia Jenerali Mabena amewataka waombaji kufahamu kuwa JKT halitoi ajira wala halihusiki na utafutaji wa ajira katika asasi, vyombo vya ulinzi na usalama au mashirika ya Serikali na yasiyo ya Serikali, bali hutoa mafunzo yatakayowawezesha vijana kujiajiri na kujitegemea mara baada ya kumaliza mkataba wao na JKT.
Amesema sifa za waombaji pamoja na maelekezo ya vifaa vinavyotakiwa kwenda navyo vinapatikana kupitia tovuti rasmi ya Jeshi la Kujenga Taifa ambayo ni www.jkt.mil.tz.


