Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali imekabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi bilioni 23.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji , huku Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) ikipongezwa kwa kazi kubwa inayofanya kuhakikisha sekta ya Umwagiliaji inakuwa nguzo ya uchumi wa taifa. Vitendea kazi hivyo ni pamoja na mitambo mikubwa 19 ya kuchimba visima vyenye uwezo wa kufikia urefu wa mita 300 hadi 1800, magari 17 ya kubeba vifaa na malighafi, trela 2 na pikipiki 23.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, alisema hatua hiyo itaongeza chachu katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji kote nchini.


“Serikali iliongeza bajeti ya maendeleo kutoka shilingi bilioni 46.5 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 308.7 mwaka 2025/26. Wizara itaendelea kusimamia na kufuatilia upatikanaji wa fedha ili ikamilike kwa wakati,” alisema, huku akiielekeza Bodi ya Uongozi ya NIRC na watumishi wa NIRC kusimamia vizuri rasilimali hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa, alisema hafla hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa Agosti 8, 2022.


“Leo tunashuhudia jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kwa kukabidhi mitambo mikubwa ya visima 19, magari 16 ya kusaidia uchimbaji, trela 2 na pikipiki 23. Tume imepanga kuchimba visima 67,000 ndani ya miaka 5, vitakavyohudumia hekta 16,000.

Katika mwaka huu wa fedha pekee, visima 1,027 vimepangwa kuchimbwa na tayari visima 260 vimeshachimbwa kwa majaribio katika mikoa 12,” Ameeleza.

Mndolwa aliongeza kuwa Tume imenunua pampu 1,000 kwa ajili ya kutoa maji ziwani, ambazo zitagawiwa kwa makundi maalum ya wanawake na vijana.Tume inaendelea na utekelezaji wa miradi 146 ya Umwagiliaji , ambapo miradi 18 imekamilika na ipo tayari kukabidhiwa.


“Watumishi wa Tume wako tayari na tumejipanga kuongeza eneo linalomwagiliwa ili kufikia malengo ya ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030,” Amesisitiza .

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema asilimia 72 ya wananchi wa mkoa huo wanategemea kilimo, hivyo ujio wa vifaa hivyo ni mapinduzi makubwa ya kiuchumi. “Rais alishasisitiza kuwa shida siyo ukame bali ni maarifa ya namna ya kukabiliana na changamoto hiyo. Dodoma imejipanga kuwa mkoa wa kimkakati katika uzalishaji wa alizeti na kupitia umwagiliaji wananchi wanaweza kulima hadi mara tatu kwa mwaka,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile, pamoja na Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbaga, walipongeza Serikali na Rais Samia kwa kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji.


“Tume inafanya kazi nzuri, visima vinaendelea kuchimbwa na miradi mikubwa ya umwagiliaji inatekelezwa,” amesema Ditopile.

“Rais ametekeleza ilani ya CCM kwa vitendo na sasa Dodoma inakuwa mfano wa mapinduzi ya kilimo cha umwagiliaji.” Ameongeza Mbaga.