Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia,
Dodoma
Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limeendelea kuonyesha mchango wake katika kukuza ubunifu na teknolojia nchini baada ya kuiwezesha kampuni ya Afro Heal Group Limited kubadili mimea ya asili kuwa dawa za kisasa zinazokidhi mahitaji ya soko na kuchangia kuboresha huduma za afya.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nanenane Agosti 2026, mwakilishi wa Afro Heal Group Limited, Mashauriano Kishushu, amesema kampuni hiyo inajishughulisha na utafiti, ubunifu na utengenezaji wa dawa za binadamu zinazotokana na mimea ya asili.
Alieleza kuwa kabla ya kushirikiana na TIRDO walikuwa wakitengeneza dawa kwa mfumo wa jadi wa kutumia magome, lakini kupitia malezi ya biashara, ushauri wa kitaalamu na uwezeshaji walioupata kutoka shirika hilo, wamefanikiwa kuzalisha bidhaa za kisasa zenye ubora wa hali ya juu.
“Kabla ya kujiunga na TIRDO tulikuwa tunatengeneza dawa katika mfumo wa kawaida wa magome. Kupitia malezi ya biashara, ushauri wa kitaalamu na uwekezaji wa rasilimali tulioupata, tumefanikiwa kuzalisha bidhaa za kisasa zenye ubora mkubwa kwa matumizi ya binadamu. Tunawashukuru sana TIRDO kwa kutufikisha hapa,” alisema Kishushu
.
Aliongeza kuwa TIRDO imewapatia mwongozo katika kila hatua ya uchakataji wa mimea ya asili hadi kufanikiwa kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya ubora na zinazorahisisha matumizi kwa wananchi.
Kishushu amesema mazingira rafiki yaliyowekwa na TIRDO kwa wabunifu yameiwezesha Afro Heal kuongeza thamani ya malighafi za asili na kuzigeuza kuwa bidhaa zenye ushindani katika soko, huku zikitoa mchango mkubwa katika sekta ya afya na maendeleo ya uchumi.
Aidha, amewahimiza vijana wenye mawazo ya ubunifu na teknolojia kutokata tamaa, akieleza kuwa mafanikio yanahitaji uvumilivu, kujifunza na kuendelea kuamini katika wazo la ubunifu.
Amesema yeye binafsi hakupata changamoto kubwa kujiunga na TIRDO na kupata mwongozo uliomfikisha katika hatua ya sasa.
Akizungumzia malengo ya kampuni hiyo, alisema Afro Heal Group Limited inalenga kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dawa zinazotokana na mimea ya asili nchini Tanzania na kuzifikisha bidhaa zake katika masoko ya ndani na kimataifa.
Kwa upande wake, aliishukuru TIRDO kwa kuendelea kuwawezesha wabunifu wa Kitanzania, akisema uwekezaji unaofanywa na shirika hilo umefungua fursa kwa vijana wengi kubadili mawazo yao ya kibunifu kuwa bidhaa zenye thamani, zinazochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za afya nchini.



