Na OWM–TAMISEMI, Kilosa

Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa watanufaika na Shilingi Bilioni 1.2 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kisasa la chuma lenye urefu wa mita 30 katika Mto Nyameni, Kata ya Ulaya, mradi unaotekelezwa na TARURA wenye lengo la kuboresha usafiri na usafirishaji kati ya kata za Zombo, Nyameni na Ulaya.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, Agosti 6, 2026 alipokagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo katika ziara yake ya kikazi ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Kilosa.

“Mhe. Rais anawapenda wananchi wa Zombo, Nyameni na Ulaya. Ameonesha hilo kwa kutoa Bilioni 1.2 kujenga daraja hili litakalomaliza changamoto ya usafiri na usafirishaji iliyosababishwa na kuvunjika kwa daraja la zamani,” amesema Prof. Shemdoe.

Amesema ujenzi wa daraja katika barabara ya Zombo–Nyameni–Ulaya umefikia asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika Agosti 30, 2026, mara baada ya kuwasili kwa vyuma vya kukamilisha ujenzi, ambavyo vinatarajiwa kuingia nchini kwa njia ya meli.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Ndyamkama, amesema ufungaji wa vyuma hivyo utafanywa na wahandisi wa TARURA mkoa wa Morogoro wenye uzoefu wa kazi kama hiyo iliyotekelezwa Mlimba, wilaya ya Kilombero.

Ameongeza kuwa daraja hilo litakuwa na njia mbili za watembea kwa miguu pamoja na uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa zaidi ya tani 40. Pia, daraja la kamba lililopo litahamishiwa eneo jingine lenye uhitaji ili kuongeza huduma ya kuvuka mto Nyameni.

Naye, mkazi wa kata ya Ulaya, Bi. Fatuma Mwalimu Chaubwa, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa daraja hilo na kumpongeza Mbunge wa Jimbo, Mhe. Denis Londo, kwa ufuatiliaji wake wa karibu wa utekelezaji wa mradi huo.

Daraja hilo linatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa kwenda sokoni, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na elimu, kuongeza fursa za biashara na uwekezaji, pamoja na kuimarisha usalama wa wananchi wanaovuka mto Nyameni.