Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amevutiwa na maendeleo ya mradi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa na kufanya manunuzi ya ndani yenye zaidi ya dola milioni 740 ( trilioni 1.9) zilizotumika katika manunuzi ya bidhaa na huduma za ndani, hatua iliyochochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Mradi wa EACOP si tu unajihusisha na ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, bali pia umekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo kwa kutoa fursa za ajira kwa wazawa, wakandarasi wa ndani na kuwajengea uwezo Watanzania,” amesema.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo katika eneo la Chongoleani, mkoani Tanga, Dkt. Nchemba amesema mradi huo, ambao umefikia asilimia 81, pia umeajiri Watanzania wapatao 8,500 sawa na asilimia 78 ya wafanyakazi wote 11,155 waliopo, wakiwemo raia wa kigeni.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba (katikati) akizungumza na wafanyakazi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP),punde mara baada ya kuwasili kwenye mradi huo, uliopo eneo la Chongoleani mkoani Tanga ikiwa ni ziara yake ya kikazi mkoani humo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Bi. Salome Makamba na kulia ni Meneja Mradi wa EACOP, Bw. Emmanuel Blarez.

Waziri Mkuu amesema Serikali inajivunia mafanikio yaliyofikiwa na dhamira ya wabia kuhakikisha mradi unakamilika katikati ya mwaka huu ili kuanza rasmi usafirishaji wa mafuta ghafi kwenda soko la kimataifa.

Pia amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo ni kielelezo cha ushirikiano imara kati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda katika kuhakikisha wananchi wa nchi hizo mbili wananufaika.

Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Nishati, Bi. Salome Makamba, amesema Serikali , ambayo inamiliki hisa asilimia 15 katika mradi huo kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imeridhishwa na maendeleo ya mradi yaliyofikiwa mpaka sasa.

Amesema kabla ya utekelezaji wake hapa nchini, zaidi ya Watanzania 9,000 wameguswa na utekeleaji wa mradi huo na wamelipwa fidia mbalimbali, wakiwemo wananchi 1,688 wa Mkoa wa Tanga waliolipwa shilingi bilioni 10.49, huku wengine wakipatiwa nyumba mbadala na msaada wa chakula kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja.

Aidha, pamoja na mambo mengine, amesema kuwa maelfu ya Watanzania wamefaidika na mradi huo kwa kupewa mafunzo ya bure kupitia vyuo vya ufundi stadi nchini (VETA) katika mikoa mbalimbali, huku wengine wakinufaika na udhamini wa masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia ushirikiano wa mradi huo na taasisi hizo.

Amesema, kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii (CSR), mradi wa EACOP umefadhili miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 4.4, ujenzi wa Kituo cha Afya Donge mkoani Tanga, pamoja na mpango wa usambazaji umeme katika vijiji vilivyopitiwa na bomba katika mikoa nane, ambapo kupitia mpango huo, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linatarajiwa kuongeza mapato yake kwa kiasi kikubwa.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba ( wapili kushoto) akipatiwa maelezo kuhusiana na maendeleo ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), na Mhandisi Mussa Msafiri (katikati) kutoka EACOP wakati wa ziara yake ya kikazi iliyofanyika mkoani tanga. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Bi. Salome Makamba na Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bi. Batilda Buriani.

Lakini pia amesema kuwa Bandari ya Tanga kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kutokana na uwepo wa mradi huo mkoani humo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bi. Batilda Buriani, amesema mradi huo umeacha alama kubwa mkoani humo kwa kutoa ajira, mafunzo ya ufundi na ujasiriamali kwa wananchi ili waweze kuajiriwa na kujiajiri.

Ziara hiyo ya Waziri Mkuu ilijumuisha viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Matarajio, Wakuu wa Wilaya na wengine kutoka TPDC, ulipokelewa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa EACOP, Bw. Emmanuel Blarez, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Guillaume Dulout.

Maelezo ya kiufundi yalitolewa na Mhandisi Mussa Msafiri, akibainisha kuwa ujenzi wa matenki manne ya kuhifadhia mafuta kutoka Uganda yenye ujazo wa lita 500,000 kila moja umefikia asilimia 87, huku ujenzi wa ghati ya kupakia mafuta kwenye meli ukifikia asilimia 57. Ujenzi wa miundombinu mingine ikiwemo majenereta, mfumo wa umeme wa jua na vifaa vya kuzimia moto unaendelea.

Kwa upande wake, Bi Neema Kweka, anayesimamia maudhui ya ndani (Local Content) katika EACOP amesema mradi huo unajivunia kutoa ajira, kutumia masaa milioni 40 ya kutoa mafunzo kwa wazawa na kiasi hicho cha dola milioni 740 kwa ajili ya manunuzi katika ununuzi w bidhaa na utoaji huduma, hivyo kusaidia ukuaji uchumi wa ndani.

Bomba la EACOP lenye urefu wa kilometa 1,443 linaanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga, na limepita katika mikoa nane ya Tanzania Bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Wanahisa wa mradi huo ni TotalEnergies (asilimia 62), TPDC (asilimia 15), Uganda National Oil Company (UNOC) (asilimia 15) na China National Offshore Oil Corporation (CNOOC) (asilimia 8).

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba ( kulia) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Nishati, Bi. Salome Makamba (kushoto) mara baada ya kutembelea Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), uliopo eneo la Chongoleani mkoani Tanga ikiwa ni ziara yake ya kikazi mkoa humo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba (wanne kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali na wafanyakazi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), mara baada ya kutembelea eneo la mradi huo uliopo Chongoleani Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya kikazi mkoa humo. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bi. Batilda Buriani na kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Bi. Salome Makamba.