Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange ametoa rai kwa watendaji kulipa umuhimu suala la Uchumi wa Buluu kuwa sehemu ya agenda katika vikao vya pande mbili za Muungano.

Amesema hayo wakati wa kikao cha ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kilichoketi Zanzibar Februari 16, 2026.

Dkt. Dugange alisema kuwa Zanzibar imepiga hatua katika eneo la uchumi hivyo kuendeleza ushirikiano wake na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutaimarisha uchumi wa Taifa.

Alisema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais tayari imeanzisha Kitengo cha Usimamizi wa Uchumi wa Buluu ambacho ni fursa adhimu kwa wananchi kupata uelewa kuhusu sekta hiyo kupitia elimu inayotolewa.

Aidha, Naibu Waziri alisema kuwa ni muhimu kuzungumzia zaidi fursa zinazopatikana katika Muungano ikiwemo miradi mbalimbali inayotekelezwa katika pande zote mbili hatua itakayowawezesha kuzichangamkia na hivyo kuinua kipato na uchumi wa nchi.

Pamoja na mambo mengine, aliongeza kuwa Muungano umekuwa ni chachu ya uchumi kwakuwa umeimarisha mazingira kupitia miradi ya maendeleo ikiwemo biashara ya kaboni ambayo inafanyika katika maeneo mbalimbali yakiwemo misitu na hata bahari.

“Tuwapongeze viongozi wetu wa kitaifa yaani Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuimarisha huduma za kijamii na miundombinu, yote hii ni katika kuwanuia wananchi wa pande zote mbili za Muungano,” alisema.