Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kibaha
Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Kibaha imepitisha na kuidhinisha rasimu ya mpango wa bajeti ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa mwaka wa fedha 2026/2027 yenye jumla ya Shilingi Bilioni 66.7.
Kwa mujibu wa taarifa ya kikao hicho, kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 15.8 zinatarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo vya ndani vya Halmashauri, Shilingi Bilioni 39.8 ni kwa ajili ya mishahara kutoka Serikali Kuu, Shilingi Bilioni 1.9 zimetengwa kwa matumizi mengineyo, huku Shilingi Bilioni 1.9 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Kikao hicho kimeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mheshimiwa Nickson Simon, ambaye alimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa juhudi zake za kuhakikisha ukusanyaji wa mapato ya ndani unaongezeka kila mwaka pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya alieleza kuridhishwa na mwenendo wa makusanyo ya mapato na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuongeza ubunifu katika ukusanyaji ili kuiwezesha Halmashauri kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Wajumbe wa Kamati hiyo waliipongeza bajeti hiyo kwa kuonesha mwelekeo wa kuimarisha sekta za afya, elimu na uchumi, hususan kupitia utoaji wa mikopo ya asilimia kumi kwa makundi maalum. Aidha, walitaka Halmashauri kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kuwekeza zaidi katika sekta ya michezo kwa kuanzisha akademia za michezo na kujenga uwanja wa kisasa wa michezo ili kukuza vipaji vya vijana na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Manispaa hiyo.
Kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatarajiwa kuimarisha utoaji wa huduma na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa Kibaha.








