Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia Arusha.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, amefungua rasmi mkutano wa sita wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) leo jijini Arusha, akisisitiza umuhimu wa taasisi za umma na binafsi kuharakisha mageuzi ya kidijitali ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza katika mkutano huo, Balozi Dkt. Kusiluka amezitaka taasisi hizo kutangaza mifumo mbalimbali wanayobuni, ikiwamo teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence), ili ijulikane kwa wananchi na kuwasaidia kurahisisha shughuli zao za kila siku.

Amesema ni muhimu ubunifu wowote wa kiteknolojia unaofanywa na serikali au sekta binafsi kutangazwa kwa uwazi ili wananchi waweze kuuelewa na kuutumia ipasavyo kwa maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.

Mbali na hilo, amewataka wataalamu wa TEHAMA kuwasaidia vijana kutumia mitandao kwa mambo yenye tija badala ya kujihusisha na matumizi hasi yanayoweza kuhatarisha usalama na amani ya nchi.

“TEHAMA ni kipaumbele muhimu kwa Serikali ya Awamu ya Sita, hivyo nasisitiza huduma zake zipatikane kwa haraka na kwa urahisi, lakini pia ubunifu wowote utangazwe ili wananchi waweze kuelewa na kuutumia,” amesema Balozi Dkt. Kusiluka.

Amesema kutokana na TEHAMA kuwa nguzo muhimu ya maendeleo nchini, wakuu wa taasisi zote wanapaswa kuzingatia Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019 pamoja na kanuni na miongozo yake katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha amewataka wakuu hao kuzifanyia kazi kwa haraka taarifa na mapendekezo yanayotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) pamoja na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ili kuimarisha uwajibikaji na ufanisi.

Katika kulinda usalama wa taarifa, Katibu Mkuu Kiongozi amezitaka taasisi zote kujisajili kwenye taasisi ya ulinzi wa taarifa binafsi ili kuhakikisha taarifa zote zinahifadhiwa kwa usalama na kwa kuzingatia sheria.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo watumishi wa umma kwa kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara ili waendane na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani, akionya kuwa kukosa kufanya hivyo kutarudisha nyuma jitihada za maendeleo.

“Iwapo hamtawapa fursa za kuongeza ujuzi, wataendelea kufanya kazi kwa kutumia mifumo ya kizamani na mtashindwa kuendana na kasi ya kiteknolojia ya dunia,” ameonya.

Aidha.amewaonya watumishi wanaochezea mifumo kwa lengo la kufanya hujuma au kujinufaisha binafsi kuwa hawatavumiliwa, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinahujumu juhudi za serikali katika kufikia malengo ya maendeleo ya kidijitali.

Amesema kwa sasa Tanzania ipo miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika matumizi ya teknolojia, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya huduma zake zinapatikana mtandaoni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Benedict Ndomba, amesema wanaendelea kuhakikisha matumizi ya serikali mtandao yanakuwa salama na shirikishi licha ya changamoto ya uhaba wa wataalamu wa TEHAMA.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar, Dkt. Said Seif Said, amesema wataendelea kushirikiana na Serikali Mtandao Bara kuboresha huduma, huku Mwenyekiti wa Bodi ya e-GA, Mussa Kissaka, akieleza kuwa mkutano huo unalenga kukusanya maoni yatakayosaidia kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa njia ya kidijitali.

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao namba 10 ya mwaka 2019 inayofanya kazi ya kuimarisha na kuendeleza utoaji wa huduma za serikali mtandao kwa taasisi za Umma.